Gor Mahia waangukia wanajeshi wa Rwanda APR katika mchujo wa ligi ya mabingwa
Mabingwa wa ligi ya Kenya Gor Mahia watapambana na wajeshi APR ya Rwanda katika mchujo wa kwanza wa ligi ya mabingwa Afrika CAF.
Kulingana na droo iliyoandaliwa Jumatatu jijini Cairo Misri Gor Mahia wataanzia ugenini mjini Kigali Novemba 28 kwa mkumbo wa kwanza huku mechi ya marudio ikisakatwa hapa Nairobi .
Mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi baina ya mabingwa wa Algeria CR Belouizdad na El Nasr ya Libya katika mchujo wa pili .
Katika ratiba hiyo ya mchujo wa kwanza mabingwa wa Uganda Vipers watakutana na El Hilal ya Sudan huku atakayeshinda akimenyana na mshindi kati ya Fc Nouadhibou ya Mauritania na Asante Kotoka kutoka Ghana katika mchujo wa pili.

Simba SC ambao ni mabingwa wa Tanzania watakuwa na miadi dhidi ya Plateau United ya Nigeria na atakayesonga mbele akipambana na mshindi kati ya CD Dol Sol kutoka Msumbiji na Fc Platinum ya Zimbabwe katika mchujo wa pili.
Mechi za awamu ya mchujo kuwania ligi ya mabingwa Afrika kusakatwa baina ya Novemba 27 na 29 mwaka huu na mwishoni mwa wiki ya kwanza ya Desemba .