Google kutoa msaada wa shilingi bilioni 10 kwa kenya kupiga jeki ufufuzi wa uchumi

Kampuni kubwa zaidi ya maswala ya teknolojia ya Marekani ya Google imetangaza kutoa msaada wa shilingi bilioni 10 kuisaidia Kenya katika juhudi za kufufua uchumi baada ya athari za janga la virusi vya Corona.

Tangazo hilo lilitolewa siku ya jumatano jioni na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Google Sundar Pichai wakati wa mkutano wa mtandao na Rais Uhuru Kenyatta pembeni mwa mjadala wa umma kuhusu mabadiliko yaliyoletwa na mfumo wa dijitali barani Afrika uliotayarishwa na shirika la Corporate Council on Africa-CCA.

Kando na msaada huo wa shilingi bilioni kumi ambao inajumuisha shilingi bilioni tatu za kusaidia biashara ndogo ndogo, shilingi bilioni tano za taifa hili kuanzisha miradi mbalimbali na shilingi bilioni mbili za kutoa misaada, Pichai alitangaza mipango ya miradi kadhaa ya uwekezaji inayopangwa na kampuni yake humu nchini.

Pichai alisema kuwa kampuni yake itaimarisha huduma zake nchini mwaka huu na kusaidia biashara laki moja na wastawishaji elfu 150 humu nchini.

Katika sekta ya elimu, kampuni hiyo ya teknolojia ya Marekani inatarajiwa kuwapa mafunzo wanafunzi elfu 29 na walimu 1,800 kuhusiana na masomo katika maeneo ya nyanjani ikitumia mfumo wake wa Google Classroom.

Rais Kenyatta alikaribisha msaada huo kutoka kwa kampuni hiyo ya Google na akaishukuru kampuni hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali ya Kenya kuboresha mfumo wa dijitali humu nchini kwa miaka 13.

Shirika la Corporate Council on Africa ni shirika la kibiashara lenye makao yake jijini Washington DC ambalo linalenga kuimarisha biashara na ushirikiano wa kibiashara baina ya Marekani na mataifa ya bara Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *