Ghasia zashuhudiwa katika mkutano wa Ruto huko Murang’a

Ghasia zimezuka mapema Jumapili katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a, masaa machache kabla Naibu Rais William Ruto kuzuru eneo hilo.

Kufuatia ghasia hizo, mtu mmoja ameripotiwa kuaga dunia na wengine kujeruhiwa baada ya maafisa wa polisi kurusha vitoa machozi nje ya Kanisa la AIPCA Kenol ili kutuliza umati katika hafla ambayo Ruto alitarajiwa kuhudhuria kwa ajili ya mchango.

Ghasia hizo zimeanza baada ya kundi la vijana kuziba barabara katika eneo hilo na kuanza kufukuzana na kundi pinzani.

Hata hivyo, maafisa wa polisi wameapa kufanya uchunguzi wa kujua chanzo halisi cha ghasia hizo.

Magari kadhaa yameharibiwa huku barabara kuu ya kuelekea Nyeri ikikumbwa na msongamano mkubwa kwa masaa kadhaa.

Baadaye Ruto akawasili katika kanisa hilo wakati ghasia hizo zilipotulia na kuhudhuria ibada huku maafisa wa usalama wakishika doria katika sehemu mbali mbali karibu na kanisa hilo.

Ruto ameshtumu ghasia hizo huku akilaumu wapinzani wake kwa kusababisha hali hiyo.

“Nashtumu vikali hali hii. Hatupaswi kutumia vijana wetu kwa ajili ya vitendo hivyo vya kujinufaisha kibinafsi. Wanasiasa waache kuwaingiza vijana wetu katika hali hizi. Murang’a itajiamulia yenyewe,” amesema Ruto kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *