Gavana Mvurya ampigia debe mgombea huru Abdalla Feisal kwenye uchaguzi mdogo wa Msambweni

Gavana wa Kwale Salim Mvurya amekariri kwamba anamuunga mkono mwaniaji huru Abdhala Feisal kwenye uchaguzi mdogo ujao wa ubunge wa Msambweni.

Mvurya amewahimiza wakazi wawachague viongozi kwa misingi ya uadilifu wao na ajenda ya maendeleo.

Gavana huyo amekariri haja ya kuishi pamoja kwa amani ili kuleta maendeleo.

Ameyasema hayo alipokutana na baadhi ya viongozi na wafuasi wa kanisa katoliki huko Msambweni.

“Nataka kuwahakikishia kwamba mimi pamoja na Naibu Gavana tunamuunga mkono [Abdalla Feisal] na tunawauliza mumuunge mkono,” akasema Mvurya.

Kwa upande wake Abdhala amewahimiza wakazi wajiepushe na viongozi wanaonuia kuwagawanya katika misingi ya kidini na kikabila.

Amesema ataendeleza ajenda ya maendeleo ya marehemu aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori kwa vile alikuwa msaidizi wake wa kibinafsi.

“Kila mmoja wetu yuko na jukumu la kuhakikisha kuwa uongozi utakaochaguliwa hapa utakuwa wa kisawasawa, utaleta haki kwa watu wote, utaunganisha jamii na dini zote ili tupate utulivu na amani,” amehimiza Abdalla

Uchaguzi mdogo wa eneo hilo utafanyika tarehe 15 mwezi huu na unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Suleiman Dori.

Abdalla hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mwaniaji wa ODM Omar Boga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *