Gabrielle Union aandika kitabu cha watoto

Muigizaji wa Hollywood nchini Marekani Gabrielle Union kwa ushirikiano na mume wake Dwayne Wade wameandika kitabu cha watoto kwa jina, “Shady Baby”.

Kitabu hicho cha picha, kinatokana na maisha ya mwanao wa miaka mitatu kwa jina “Kaavia James”.

Union alitangaza ujio wa kitabu hicho kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo alipachika picha ya kitabu na kuandika, “Kaavia James ana maoni na hivi karibuni atayatoa kwa ulimwengu mzima. Dwayne na mimi tuna furaha kutangaza “Shady Baby” kitabu chetu cha picha ambacho kinafunza watoto jinsi ya kutumia dira ya maadili na uwezo wao wa ndani kuchagua fadhili na huruma na kujisimamia na kusimamia wengine.”

Michoro ya kitabu hicho imefanywa na Tara Nicole Whitaker.

“Shady Baby” ni hadithi kuhusu msichana mdogo ambaye anakwenda kwenye bustani moja na kukumbana na wanyanyasaji. Anajifunza kujitetea na kutetea watoto wenzake.

wazazi hawa wanatumai kwamba kupitia kwa hadithi hii watabadili maana ya neno “Shady” na kuonyesha wasichana na wavulana wadogo weusi ni muhimu kusimama kujitetea na kutetea wengine.

Union anasema pia kwamba ni muhimu kwa watoto wenye asili ya afrika au ukipenda weusi kujiona kwenye hadithi za watoto na watoto wengine wapate kuona watoto weusi katika nafasi za uongozi.

Kitabu hicho kitazinduliwa rasmi tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu wa 2021 na kampuni ya uchapishaji kwa jina “HarperCollins Publishing” lakini watu wanaendelea kuagiza kabla.

Gabrielle Union, Dwayne Wade na Kaavia James

Kaavia James ndiye mtoto wa kwanza wa Gabrielle Union na Dwayne Wade lakini Dwayne ana watoto wengine watatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *