Frank Lampard apigwa teke Chelsea huku Thomas Tuchel akimrithi
Chelsea imemrusha meneja Frank Lampard huku Thomas Tuchel akitarajiwa kutwaa nafasi yake ugani Stamford Bridge .
Kulingana na mmiliki wa klabu hiyo ya London Roman Abramovic wamelazimika kumpiga kalamu Lampard kutokana na matokeo mabovu msimu huu.
“Ni uamuzi mgumu kwa klabu licha ya kuwa na uhusiano mwema na Frank Lampard na ninamheshimu sana,lakini tumeona ni bora kufanya mabadiliko ya mkufunzi ,na ninamshukuru kwa kazi yake na kumtakia kila la heri “akasema Abromovic
Chelsea imeripotiwa kukaribia kukamilisha mazungumzo na Tuchel, ambaye kwa sasa hana kazi tangu atimuliwe kutoka Paris St Germain na anatarajiwa kusaini mkataba wakati wowote.
Lampard ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza amepoteza mechi 5 za ligi kuu Uingereza kati ya 7 licha ya kutumia kitita cha pauni milioni 220 kusajili wachezaji katika uhamisho wa Julai mwaka jana.
Lampard anaiacha Chelsea katika nafasi ya 9 ligini ,alama 11 nyuma ya viongozi Manchester United tangu ateuliwe Julai mwaka 2019.