FKF yatozwa faini ya shilingi milioni 1 na CAF
Shirikisho la soka nchini FKF limetozwa faini ya shilingi milioni 1 na Caf kwa kukiuka sheria wakati wa mchuano baina ya Kenya na Comoros kufuzu kwa kombe la Afcon tarehe 11 mwezi uliopita uwanjani Kasarani.
Kulingana na Caf Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa waziri Mkuu Raila Odinga wakiwa na maafisa wao wa usalama waliingia na kukutana na wachezaji wa Harambee stars ndani ya uwanja , eneo ambalo ni kinyume cha sheria za mchezo kwa mtu yeyote asiye mchezaji kuingia na kupuuza maagizo ya walinda usalama wa Caf kuwazuia kutoingia katika eneo hilo la Zone 1 .
Kenya ilitoka sare ya bao 1-1 na Comoros katika mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Kasarani na kudidimiza matumaini ya Harambee Stars kufuzu kwa kipute cha Afcon mwaka 2022 nchini Cameroon.
Hata hivyo FKF iko na fursa ya kukata rufaa uamuzi huo katika kitengo cha rufaa cha CAF.