Categories
Michezo

FKF yapata pigo baada ya mahakama kuzirejesha Mathare United na Zoo Fc ligini

Shirikisho la kandanda nchini  FKF limepatwa na pigo baada ya mahakama ya kutatua migogoro michezoni  nchini SDT kuamuru kurejeshwa ligini timu za Mathare United na Zoo Fc   kusubiri uamuzi wa kesi  iliyowasilishwa dhidi ya FKF na  vialbu hivyo viwili wiki ijayo.

Mwenyekiti wa Mahakama hiyo maarufu kama SDT John Ohaga ametoa uamuzi huo mapema Alhamisi wa kuzirejesha timu hizo mbili kwenye ligi pamoja na kubatilisha uamuzi wa awali wa FKF wa kutamatisha kandarasi za wachezaji wote wa klabu  hizo mbili  .

Pia jaji Ohaga ameagiza Fkf iliruhusu wachezaji na maafisa wa vilabu hivyo kufanyiwa vipimo vya COVID 19 sawa na vilabu vingine  saa 72 kabla ya kuanza mechi zao za ligi kuu .

Wachezaji wa Zoo FC

Baraza kuu la FKF likikutana Desemba 9 na kuamuru kuzipiga marufuku timu hizo hadi pale zitakaposaini mkataba huo wa Star Times.

FKF ilizipiga marufuku timu hizo kushiriki ligi kuu ya FKF baada ya kudinda kusaini mkataba wa Star Times ambao ungewezesha mechi za timu hizo kupeperushwa mbashara na runinga hiyo ya China .

 Wachezaji Mathare United

Shirikisho hilo pia linamchunguza mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier  baada yake kaundika barua kwa Star Times kuondoa barua ya kwanza iliyoandikwa na aliyekuwa katibu mkuu Sam Ochola kusaini mkataba huo .

Zoo FC vs. Kenya Football Federation – Order (17 Dec 2020)

Mkataba wa FKF na Star Times umeibua hisia kali huku vilabu vya Ulinzi Stars,Mathare United ,Gor Mahia na Zoo Fc vikiupinga kwa kukiuka haki zao hatua iliyochangia kupigwa marufuku na kutimuliwa ligini kwa Mathare  United na Zoo Fc .

Timu za Mathare na Zoo zilizuiwa kucheza mechi zao za kufungua msimu wa ligi wiki jana wakati Gor na Ulinzi wakiwa tayari wamecheza mechi 2 na moja mtawalia katika ligi kuu.

Mahakama ya SDT itakutana wiki ijayo kusikiza kesi hiyo na kutoa maelekezo zaidi huku ligi ya FKF ikiangia mechi za mzunguko wa nne mwishoni mwa juma hili.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *