Filamu kuhusu maisha ya Kanye West kuonyeshwa kwenye Netflix

Watayarishaji filamu nchini Marekani wanaonekana kugeukia filamu kuhusu maisha halisi ya watu maarufu nchini humo na wa hivi karibuni zaidi ni mwanamuziki Kanye West.

Filamu hiyo inayoangazia miaka 20 ya maisha ya Kanye West imenunuliwa na Netflix na ni kazi ya waelekezi wa filamu Clarence “Coodie” Simmons na Chike Ozah kwa ushirikiano na studio za TIME.

Waelekezi hao wawili wamewahi kufanya kazi na Kanye West, kwenye video za nyimbo zake ambazo ni “Jesus Walks” na “Through the Wire”.

Ripoti za awali zilidai kwamba Netflix ilinunua kazi hiyo kwa bei ya dola milioni 30 lakini duru za kuaminika zinasema hiyo bei sio sahihi.

Studio za TIME zimewahi kutayarisha kazi sawia kama vile filamu kwa jina “John Lewis: Good Trouble” ambayo inaangazia maisha ya mwanasiasa huyo na ambayo ilishinda tuzo la filamu bora ya matukio halisi yaani “Best Documentary Film” kwenye tuzo za mwaka 2021 za NAACP.

NAACP au National Association for the Advancement of Colored People ni shirika la kuendeleza harakati za watu wasio wazungu na tuzo hizo ni mojawapo ya mipango yake ya kuinua vipaji vya watu hao.

Kazi hiyo kuhusu maisha ya Kanye itaanza kuonyeshwa wakati wowote mwaka huu na inahusisha picha ambazo hazijawahi kuonyeshwa hadharani za Kanye na kuangazia pia kazi yake kama mwanamuziki na hatua yake ya kuwania Urais mwaka 2020 nchini Marekani.

Inasemekana kwamba Kanye West hahusiki kwa vyovyote na kazi hiyo lakini amekubalia walioitayarisha kuifanya.

Watu wengine maarufu huchukua jukumu la mtayarishi mkuu wanapoangaziwa kwenye filamu kama hizo ili kujihakikishia kiasi kikubwa cha malipo iwapo kazi hiyo itauzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *