Ezekiel Mutua ataka Eric Omondi akamatwe

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya Daktari Ezekiel Mutua sasa anataka mchekeshaji Eric Omondi akamatwe.

Kulingana naye, Eric amekuwa akiendesha danguro kwenye kipindi chake cha mitandaoni kwa jina “Wife Material” huku akikisingizia kuwa mpango wa ushauri kwa wasichana hao.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mutua anamkosesha Eric kwa kuonekana wazi akibusu wasichana tofauti kati ya waliokuwa kwenye shindano hilo, ilhali kuna ugonjwa wa Covid 19.

Analaumu mmoja wa walioalikwa kufundisha wasichana hao kwa kuwafunza jinsi ya kujamiiana na Eric Omondi akitaja kitendo hicho kuwa cha kishetani.

Kulingana naye, studio ambazo Eric Omondi alizindua katika eneo la Lavington hazisaidii vijana jinsi alikuwa amepanga lakini zinatumika kudhulumu wasichana. Anahimiza makachero wa DCI kuzuru eneo hilo na kumkamata mmiliki .

Ezekiel pia analaumu makundi ya kutetea haki za wanawake akisema yako kimya wanawake wenzao wakidhulumiwa. Bwana Ezekiel Omondi huwa anaendesha kampeni ya kuhakikisha kwamba video chafu au ambazo zinavuruga maadili na hata muziki havionyeshwi hadharani.

Ezekiel na Eric wamewahi kujipata wakizozana tena pale ambapo Ezekiel alimkosoa Eric kwa kupiga picha akiwa nusu uchi.

Wakati huo Eric alikuwa anajitayarisha kufungua studio zake ambazo anasema zitahudumia vijana bure bila malipo kwa nia ya kuendeleza sanaa na talanta.
Baadaye Eric alimfokea Mutua akimwambia aache kutaja jina lake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *