Eric Omondi na Sauti Sol wang’ara kwenye tuzo za AEAUSA

Wasanii wa Kenya Eric Omondi ambaye ni mchekeshaji na kundi la wanamuziki la Sauti Sol ndio wasanii pekee wa Kenya ambao walishinda tuzo kwenye tuzo za burudani Afrika huko Marekani au ukipenda African Entertainment Awards USA.

Erick Omondi ameng’aa kwenye kitengo cha mchekeshaji bora barani Africa ambapo alikuwa akishindana na mkenya mwenzake Eunice Mamito.

Omondi amekuwa akijirejelea kama Rais wa wachekeshaji wote barani Afrika na ushindi huu wake ni thibitisho kwamba kweli yeye ni kiongozi wa fani ya uchekeshaji barani humu.

Wengine ambao alikuwa akishindana nao ni Bovi wa Nigeria, Patrick Salvado na Anne Kansiime wa Uganda, Eddie Kadi wa Congo, Daliso Chaponda wa Malawi, Loyiso Gola wa Afrika Kusini, Gilmario Vemba na Calao show wote wa Angola.

Sauti Sol nao walishinda kwenye kitengo cha kundi bora la muziki Afrika huku wakiwabwaga, Best life Music wa Burundi, Weusi na Navy Kenzo kutoka Tanzania, B2C ya Uganda, R2 bees na Dope Nation wa Ghana, Toofan kutoka Togo, Calema wa nchi ya Sao Tome and Principe na mwisho Mobbers kutoka Angola.

Hafla ya kutuza washindi wa mwaka 2020 wa tuzo za AEAUSA ilifanyika jana tarehe 20 mwezi Disemba mwaka 2020 saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.

Wasanii wa Tanzania Diamond Platnumz na Rayvanny waling’aa kwenye vitengo vya wanaume vya msanii bora wa kiume barani Afrika na msanii bora wa kiume katika eneo la Mashariki, kusini na kaskazini mwa Afrika mtawalia.

Tazama picha ya orodha ya washindi wa tuzo hizo za AEUSA mwaka 2020 zenye vitengo 24. Hongera kwa washindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *