Dr. Dre bado yuko hospitalini

Wiki moja baada ya mwanamuziki tajika wa mtindo wa Hip Hop nchini Marekani Andre Romelle Young kukimbizwa hospitalini kutokana na tatizo la kuvimba na kupasuka kwa mshipa wa damu kwenye ubongo, bado yuko hospitalini na katika kile chumba cha wagonjwa mahututi.

Duru zinaarifu kwamba afya ya Dr. Dre ni dhabiti na anajihisi lakini madaktari katika hospitali ya Cedars Sinai huko Los Angeles wameamua kumweka huko huku wakichunguza kilichosababisha tatizo lake la kuvuja damu kwenye ubongo.

Madaktari walielezea kwamba ni salama kumweka mwanamuziki huyokatika chumba hicho ili kuweza kumdhibiti ikiwa tatizo lake litarejea tena.

Wiki jana Dr. Dre aliweka picha yake kwenye akaunti ya Instagram inayomwonyesha akiwa studioni huku akihakikishia wote kwamba yuko salama na kuwashukuru watu wa familia yake na mashabiki kwa kumjali.

Alisema yuko salama na atarejea nyumbani karibuni. Dre alishukuru pia madaktari wanaomshughulikia hospitalini Cedar.

Huku haya yakijiri, washukiwa wanne wametiwa mbaroni kwa kujaribu kuingia na kuiba kutoka kwa makazi ya Dr. Dre hasa baada ya habari kuenea kwamba yuko hospitalini.

Taarifa nyingine ziliarifu kwamba Dr. Dre alikubali kumpa mke waliyetengana kwa jina Nicole Young dola milioni mbili kama usaidizi kwa mwanandoa.

Wawili hao wana watoto wawili pamoja na wanaendeleza mipango ya talaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *