Don Jazzy azindua mwanamuziki Ayra Starr

Mtayarishaji wa muziki nchini Nigeria ambaye pia ni mwanamuziki Michael Collins Ajereh maarufu kama Don Jazzy ametangaza ujio wa mwanamuziki mwingine kwa jina Ayra Starr.

Chini ya kampuni ya muziki ya Don Jazzy kwa jina Mavin Records Ayra Starr tayari ana nyimbo tano ambazo zilizinduliwa rasmi kwenye majukwaa mbali mbali ya mitandao usiku wa kuamkia leo.

Nyimbo hizo ni ‘Away’, ‘Ija’, ‘DITR’, ‘Sare’ na ‘Memories’ na ni za urefu wa kati ya dakika mbili na tatu.

Akitangaza uzinduzi wa nyimbo hizo, Don Jazzy alisema kwamba alikutana na Ayra mwaka mmoja uliopita akiwa na umri wa miaka 18 tu na wakaanza kazi mara moja.

Don Jazzy ambaye sikuhizi hujihusisha na maigizo kwenye mitandao ya kijamii anasema ameweza kuelewa ulimwengu wa vijana kupitia macho ya Ayra.

Kulingana naye, safari hiyo ya mwaka mmoja ya kuunda nyimbo na Ayra imekuwa ya kufana sana. Awali Ayra alikuwa akiimba nyimbo za wanamuziki wengine mashuhuri na kuweka video hizo kwenye akaunti yake ya Instagram.

Kampuni hiyo ya Don Jazzy, Mavin Global iliwahi pia kuandikisha mwanamuziki wa umri wa miaka 18 mvulana kwa jina Divine Ikubor maarufu kama Rema mwezi wa tatu mwaka 2019.

Don Jazzy alisisimua mitandao ya kijamii pale alipoanzisha muungano wa wanaume ambao wana mkono ghamu nchini Nigeria maarufu kama “Stingy Men Association of Nigeria”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *