Don Jazzy ataja wanamuziki anajuta kutosajili

Mtayarishaji wa muziki nchini Nigeria Don Jazzy kwa jina halisi Michael Collins Ajereh amefichua wasanii watatu wakubwa nchini Nigeria ambao anajuta kwa kukosa kuwasajili kwenye kampuni yake ya muziki.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, mmiliki huyo wa Mavin Records alisema anajuta kutosajili wanamuziki Simi, Falz na Teni.

Jazzy alielezea kwamba alikosa kusajili Falz wakati anaanza kazi ya muziki kwani alikuwa tayari amejitafutia usimamizi lakini alimezea mate talanta yake.

Simi naye, alikuwa mmoja wa walioshiriki shindano la Don Jazzy kwenye Twitter miaka mingi iliyopita ambapo hakuibuka mshindi lakini Jazzy anakiri aliimba vizuri. Alikosa kumsajili kwa kutomfahamu vyema jambo ambalo anajuta.

Kuhusu Teni au ukipenda Teniola Apata mwanadada ambaye anafanya vizuri kwa muziki nchini Nigeria kwa sasa, Don Jazzy anasema walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara lakini kampuni yake haikuwa imeafikia uwezo wa kumhamisha kutoka Marekani na kumrejesha Nigeria kwa ajili ya muziki.

Don alisema hajawahi kupata wazo la kumsajili Davido lakini anakiri kwamba alimwaminia tangu mwanzo kwamba atakuwa msanii mkubwa.

Kabla ya kuanzisha Mavin Records, Don Jazzy alikuwa mmiliki mwenza wa kampuni nyingine ya muziki iitwayo Mo’ Hits Records ambapo alishirikiana na mwanamuziki D’Banj.

Don Jazzy amewahi kufanya kazi na wanamuziki wa Marekani Kanye West na Jay Z.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *