Categories
Michezo

Dimba la AFCON kwa chipukizi chini ya miaka 20 kuanza Jumapili Mauritania

Makala ya 16 ya michuano ya AFCON kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20 yataanza kutimua vumbi nchini Mauritania Jumapili usiku kwa mkwangurano wa ufunguzi wa kundi A baina ya wenyeji dhidi ya Cameroon kuanzia saa tano katika kundi A  .

Uganda watashuka uwanjani  Jumatatu kuwajulia hali  Msumbiji katika pambano la kundi A ,kabla ya Burkina Faso kufungua ratiba ya kundi B pia Jumatatu dhidi ya Tunisia nao Namibia wakwangurane na Jamhuri ya Afrika ya kati.

Mabingwa mara tatu Ghana ndio walioshiriki kipute hicho mara nyingi ikiwa mara 12 wakifuatwa na Cameroon  ambao ni mabingwa wa mwaka 1995 walioshiriki mara 10  ,nao  Moroko wanashiriki kwa mara ya 5 huku Burkina Faso ikishiriki kwa mara ya 4.

Hata hivyo mataifa 7 yanashiriki michuano hiyo mwaka huu kwa mara ya kwanza yakiwa:wenyeji Mauritania,Tanzania,Uganda,Namibia,Msumbiji,Jamhuri ya Afrika ya kati na Tunisia .

Mashindano hayo yatakayokamilika tarehe 6 mwezi ujao yanashirikisha mataifa 12  huku Afrika Mashariki ikiwakilishwa na Uganda na Tanzania waliofuzu kupitia michuano ya CECAFA mwaka uliopita nchini Tanzania.

Mali ambao hawakufuzu kwa mashindano ya mwaka huu walinyakua kombe hilo katika makala ya mwaka 2019 walipoishinda Senegal penati 3-2 kufuatia sare ya bao 1-1 katika dakika 120 .

Michuano yote ya kipute hicho itarushwa mbashara kupitia KBC Channel one .

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *