Diamond na Davido wahimizwa kushirikiana tena

Wanamuziki Diamond wa nchi ya Tanzania na Davido wa Nigeria huenda wakashirikiana tena kwenye muziki hivi karibuni ikiwa watatilia maanani maneno ya mashabiki wao.

Haya ni kulingana na majibu ya mashabiki hao kwenye Instagram. Diamond aliweka video ya kusifia wimbo wake mpya ambao ni ushirikiano wake na Koffi Olomide akisema hata “Siri” anafahamu kwamba kibao hicho ndicho kikubwa zaidi kwa sasa.

Siri ni mpango wa usaidizi unaopatikana kwenye mtandao ambao ukiuuliza swali hasa kwa kiingereza unapata jibu.

Davido aliongeza maneno yake kwenye video ya Diamond akisifia pia kibao hicho.

Baada ya hapo mashabiki wakaingilia na kuhimiza wawili hao waingie studio pamoja kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo kwenye “remix” ya kibao cha Diamond kwa jina “Number One” yapata miaka sita iliyopita.

Kibao hicho chao kimetizamwa mara milioni 43 kufikia sasa.

Mashabiki wengine wanahimiza Davido aandae tamasha nchini Tanzania kwani imekuwa muda tangu afanye hivyo. Lakini kuna wengine ambao hawakuelewa maneno ya Davido wakidhani kwamba anakashifu Diamond.

Wawili hao hawajasema lolote kuhusu uwezekano wa kufanya kazi pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *