David the Student anaugua Corona

David Kangogo maarufu kama David the Student ametangaza kwamba alipimwa na akapatikana kuwa na virusi vya Corona na sasa amejitenga.

Kupitia Instagram David ambaye alikuwa mchekeshaji kwenye kipindi cha Churchill, alielezea kwamba alianza kujihisi mgonjwa ijumaa tarehe 20 mwezi huu, Jumamosi akakwenda hospitali kupimwa Covid – 19 na Jumapili akazidiwa.

Jumatatu tarehe 23 ndio alipata majibu ya vipimo ambayo yalidhibitisha kwamba alikuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Alisema kwamba ameanza kujitenga kwa siku 14 inavyohitajika huku akishukuru wote kwa usaidizi. Mchekeshaji huyo anakumbusha wote kwamba ni muhimu kufuata kanuni zote za kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono kila mara na kuhakikisha umbali unaohitajika kati ya watu.

Haya yanawadia siku chache baada ya David ambaye sasa anaishi na kufanya kazi Marekani kukumbwa na kisa cha ubaguzi wa rangi nchini humo.

Yeye ni mhudumu wa teksi na alidhulumiwa na abiria mmoja mzungu ambaye alikuwa ameandamana na mke wake. David anahudumu chini ya kampuni kwa jina “Lyft” na alibeba wawili hao kutoka mkahawa mmoja na pindi alipoingia kwenye gari mzee huyo akavua barakoa, na David akamsihi aivalie ndio mambo yakaanza.

Mzee huyo alimtusi na hata kutishia kukojoa kwenye gari lake. Video ya tukio ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na imesababisha mwanaume huyo mzungu afutwe kazi na kupigwa marufuku kwenye mkahawa alikotolewa siku hiyo. Hata hivyo Bwana huyo ameomba msamaha akisema kwamba alilewa sana hadi akajisahau.

Tunamtakia David afueni ya haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *