Categories
Habari

COVID-19: Watu 396 zaidi waambukizwa huku wagonjwa 397 wakipona

Watu 396 zaidi wamebainika kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 na kufikisha jumla ya visa vilivyothibitishwa humu nchini kuwa 88,380 tangu kisa cha kwanza kuripotiwa mwezi Machi mwaka huu.

Kwenye taarifa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema visa hivyo 396 vimetokana na sampuli 4,717 zilizopimwa katika muda wa saa 24 zilizopita. Hii inafikisha jumla ya sampuli zilizopimwa kuwa 931,799.

Nairobi ingali inaongoza kwa visa 154 ikifuatiwa na Kiambu kwa visa 40 , Busia 31, Bungoma 30, Mombasa 23, Murang’a 19, Nakuru 14, Garissa 14 na Kakamega visa 12, miongoni mwa kaunti nyingine.

Kati ya visa hivyo vya maambukizi vilivyonakiliwa, 373 ni vya Wakenya na 23 ni vya raia wa kigeni. Visa 254 ni vya wanaume na 142 ni vya wanawake. Muathiriwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa miaka miwili ilhali yule mwenye umri mkubwa zaidi ana miaka 85.

Wagonjwa 397 wamepona kutokana na ugonjwa huo, 318 chini ya mpango wa kuhudumiwa nyumbani, ilhali wengine 78 waliruhusiwa kuondoka kutoka hospitali mbali mbali. Jumla ya waliopona sasa ni 68,929.

Hata hivyo waziri Kagwe amesema wagonjwa wanane zaidi wamefariki kutokana na ugojwa huo na kufikisha jumla ya vifo kuwa 1,526.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *