COVID-19: Watu 349 zaidi waambukizwa huku wagonjwa 6 wakiaga dunia

Wizara ya Afya imethibitisha visa vipya 349 vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kutokana na upimaji wa sampuli 5,025 katika muda wa masaa 24 yaliyopita.

Visa hivyo vimefikisha jumla ya maambukizi humu nchini hadi 94,500 baada ya jumla ya sampuli 1,008,518 kufanyiwa uchunguzi tangu kisa cha kwanza kuthibitishwa humu nchini mwezi Machi.

Kati ya visa hivyo, 334 ni vya Wakenya ilhali 15 ni raia wa kigeni, 230 kati yao wakiwa ni wanaume nao 119 ni wanawake, wote wa kati ya umri wa miezi 11 hadi miaka 98.

Kaunti ya Nairobi imeendelea kuongoza kwa kuripoti visa 156, ikifuatwa na Nyeri kwa visa 34, Kirinyaga 30, Meru 27, Uasin Gishu 25, Mombasa 17, Kiambu 15, Busia 13, Nandi 7, Murang’a 6, Nyandarua 4, Machakos 3, Garisa na Kisii visa viwili viwili, huku Tharaka Nithi, Turkana, Kajiado, Nakuru, Embu na Laikipia zikiripoti kisa kimoja kimoja.

Wizara hiyo pia imethibitisha kupona kwa wagonjwa 176. Kati ya hao, 155 walikuwa kwenye mpango wa kuhudumiwa nyumbani ilhali 21 walikuwa wakitibiwa hospitalini.

Hii imefanya idadi ya waliopona kuwa 75,735.

Hata hivyo, wagonjwa sita wamefariki kutokana na makali ya COVID-19 na kuifanya jumla ya waliofariki humu nchini kuwa 1,639.

Kulingana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, jumla ya wagonjwa 831 wanatibiwa katika vituo mbali mbali vya afya humu nchini nao 5,834 wanahudumiwa nyumbani.

Wagonjwa 52 wako kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi, 25 kati yao wakiwa wanasaidiwa kupumua huku 24 wakiwa wanapokea hewa ya ziada ya Oksijeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *