Categories
Burudani

Cindy Sanyu azungumzia tuzo za MAMA

Mwanamuziki wa Uganda wa mtindo wa dancehall Cindy Sanyu amesema kwamba hasumbuliwi na hatua ya waandalizi kukosa kumteua kuwania tuzo za MAMA mwaka 2021.

Cindy ni mmoja wa wasanii wa muziki walioinuka sana hivi karibuni hasa kuanzia mwisho wa mwaka 2019 na wengi walitarajia kwamba atakuwa mmoja wa wawaniaji wa tuzo hizo ambazo zitaandaliwa nchini Uganda.

Mwanamuziki huyo sasa anasema kwamba hatua ya yeye kukosa kuteuliwa kuwania tuzo za MAMA haibadilishi chochote katika kazi yake kama mwanamuziki kwani tayari ashakuwa msanii mkubwa na ameafikia mengi.

“Sikukasirika nilipokosa kuteuliwa kwa tuzo hizi kwani mimi ni msanii mkubwa sana ambaye hahitaji tuzo la MAMA kunisongesha mbele. Tayari nimeshinda tuzo la AFRIMMA kwa hivyo sihitaji uteuzi wao.” alisema Cindy wakati alihojiwa na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda.

Cindy ni mmoja wa wale ambao waliomba kwamba tuzo za MAMA ziahirishwe kwani watu wa nchi hiyo walikuwa na maambo mengine mengi ya maana ya kushughulikia na mengi yalitokana na janga la Corona.

Alionekana pia kutokubaliana na hatua ya kuchaguliwa kwa mwanamuziki wa Marekani DJ Khaled kuongoza au kuwa mtangazaji mkuu wa hafla ya tuzo za MAMA.

Watu wengi nchini Uganda walionelea kwamba haingekuwa vyema kuandaa hafla ya kutuza wshindi wa MAMA wakati ambapo wengi hawawezi kujimudu baada ya kupoteza ajira na vitega uchumi kutokana na Janga la Corona.

Wanaharakati pia hawakufurahishwa na hafla hiyo ambayo ingeandaliwa wakati ambapo wanamuziki wengi wamefungiwa na hawawezi kuandaa tamasha nchini Uganda.

Tuzo za MAMA zingeandaliwa mwezi huu wa pili mwaka 2021 nchini Uganda lakini zikaahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na malalamishi ya wengi nchini humo.

Mwanadada Cindy ndiye naibu rais wa chama cha wanamuziki wa Uganda almaarufu “Uganda Musicians Association” na amesema kwamba hatawania urais wa chama hicho baada ya Ykee Benda kujiuzulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *