Cheptegei na Gidey wavunja rekodi za dunia
Bingwa wa dunia Joshua Cheptegei alidhihirisha umahiri wake na kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 10000 katika mashindano ya NN Woeld Record Day mjini Valencia Uhispania Jumatano usiku.
Cheptegei aliye na umri wa miaka 22 alivunja rekodi ya mita 10000 alipotumia dakika 26 sekunde 11 nukta 02 akivunjilia mbali rekodi ya miaka 15 iliyopita iliyokuwa ikishikiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia ya dakika 26 sekunde 17 nukta 53 .
Mganda huyo alivunja rekodi ya mita 10000 zikiwa siku 54 tangu avunje rekodi ya mita 5000 ya katika mkondo wa Diamond league wa Monaco .
Cheptegei ambaye alikuwa amefanya mazoezi yake kwa zaidi ya wiki 6 huko Kapchorwa alianza kupigiwa kasi na Matthew Ramsden aliyepiga mzunguko wamita 3000 kwa dakika 7 sekunde 52 nukta 79 kabla ya Nicolas Kimeli kushika usukani na kukamilisha mita 5000 kwa dakika 13 sekunde 7 nukta 73.
Cheptegei ni mwanraidha wa 10 wa kiume kushikilia rekodi mbili za dunia katika mita 10000 na 5000.

”Nilitaka kutimiza ndoto yangu na ni fahari yangu ,nilitaka kuandikisha historia ili kuwapa watu kitu cha kufurahia ”akasema Cheptegei baada ya ushindi huo .
Chptegei sasa atasalia mjini Valencia kujiandaa kwa mashindnao ya dunia ya nusu marathon mjini Gdynia Poland Oktoba 17 ikiwa mara yake ya kwanza kukimbia mbio za barabarani.
Katika mbio za Jumatano usiku Letesnet Gidey ambaye ni mshindi wa nishani ya fedha ya dunia ya mita 5000 na kuweka rekodi mpya ya dakika 14 sekunde 6 nukta 62 na kufuta rekodi ya awali ya Tirunesh Dibaba ya dakika 14 sekunde 11 nukta 15 mwaka 2008 .

Gidey waEthiopia aliingia katika historia kuwa mwanariadha wa tatu mtawalia kutoka Ethiopia kushikilia rekodi ya dunia ya mita 5000 baada ya Meseret Defar na Tirunesh Dibaba wote kutoka Ethiopia
Bingwa na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 3000 kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech alikuwa mmoja wa wapiga kasi wa Gidey .
“nimekuwa nikiota kuhusu kuweka rekodi ya dunia tangu miaka 6 iliyopita”akasema Gidey