Chanjo dhidi ya Ebola yawasili nchini Guinea

Ndege maalum iliyobeba shehena ya chanjo za ugonjwa wa Ebola imewasili nchini Guinea, hatua ambayo itawezesha kuzinduliwa kampeni ya chanjo baadaye.

Shirika la afya duniani,WHO linasema dozi hizo elfu-11, ambazo zimewasili katika mji mkuu wa Conakry zitapelekwa karibu na mji ulioko kusini-mashariki wa Nzérékoré saa kadhaa kabla ya kuanza kutolewa chanjo hiyo.

Dhoruba ya vumbi katika jangwa la Sahara ililazimu ndege hiyo kubadili mkondo siku ya Jumapili na kuelekea nchini Senegal.

Watu watano walifariki hivi majuzi nchini Guinea baada ya kuugua ugonjwa wa Ebola hivyo vikiwa visa vya kwanza katika muda wa miaka mitano.

Kati ya mwaka 2013 na 2016 zaidi ya watu elfu -11 walifariki huko Afrika magharibi kufuatia chamko la ugonjwa huo ambalo lililoanzia nchini Guinea.

Lengo la kampeni hiyo ni kuwachanja wale waliotangamana na wagonjwa wanaougua Ebola na wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *