CHAN kutoa fursa kwa wachezaji wa nyumbani kung’aa

Makala ya 6 ya mashindano ya kombe la CHAN yatang’oa nanga Jumamosi usiku mjini Yaounde Cameroon huku mataifa 16 yakiwania kombe hilo ambalo kwa kawaida huwashirikisha wachezaji wa nyumbani pekee.

Kipute hiki kilipaswa kuandaliwa mwaka 2020 lakini kikaahirishwa baada ya kuzuka kwa janga la Covid 19.

Timu hizo 16 zitashindana katika kipindi cha wiki tatu katika miji ya Doula,Yaounde na Limbe huku Atlas Lions ya Moroko wakiwa mabingwa watatezi baada ya kutwaa kombe hilo katika makala ya mwaka 2018 wakiwa wenyeji.

Katika pambano la ufunguzi kundini A Indomitable Lions ya Cameroon watafungua ratiba dhidi ya The Warriors ya Zimbabwe saa moja usiku nao The Flying Eagles ya Mali wamenyane na The Stallions kutoka Burkinafasso saa nne usiku.

Baadhi ya timu zitakazotoa ushindani mkali ni wenyeji Cameroon walio  na wachezaji wawili walionyakua kombe la AFCON mwaka 2017 wakiwa nyumbani,mabingwa mara mbili DR Congo,Mali iliyoibuka ya pili mwaka 2016 nchini Rwanda,mabingwa watetezi Moroko na  Uganda .

Cameroon itakuwa na mashabiki wa nyumbani ambao wameruhusiwa kuingia uwanjani kwa mara ya kwanza  kutokana na ugonjwa Covid 19.

Historia ya CHAN

  • Mashindano ya kombe la CHAN yalianzishwa na shirikisho la soka Afrika mwaka 2009  kwa lengo la kuwakuza wachezaji wa ligi za nyumbani.
  • Makala ya 1  yaliandaliwa Ivory Coast mwaka 2009  na kushirikisha mataifa 8 ambapo DR Congo waliibuka mabingwa baada ya kushinda Ghana mabao 2-0 katika fainali.
  • Makala ya 2  yaliandaliwa Sudan mwaka 2011 ,idadi ya timu ikiongezeka hadi 16 nao Tunisia wakanyakua ubingwa kwa kuwalima Angola magoli 3-0 kwenye fainali.
  • Afrika Kusini ilikuwa mwenyeji wa makala ya 3 ,mwaka 2014 Ghana wakipoteza kwenye fainali magolo 3-4 kupitia Penati na Libya waliotawazwa mabingwa.
  • Rwanda ilijukumiwa kuandaa fainali za 4  mwaka 2016 na majirani DR Congo wakanyakua kombe la pii walipoishinda Mali mabao 3-0 katika fainali.
  • DR Congo wamenyakua mataji mawili ya CHAN huku Moroko,Libya na Tunisia wakishinda kombe 1 kila moja.
  • Kenya ilipaswa kuandaa makala ya 5 ya mwaka 2018 lakini ikatepetea na CAF kuhamishia mashindano hayo nchini Moroko nao wenyeji wakatwaa kombe  baada ya kuifedhehesha Nigeria mabao 4-0.

Timu zote mwaka huu zimeruhusiwa kuwa na vikosi vya wachezaji 33 ,10 zaidi ya wanaohitajika kufidia endapo kuna wale watakaopatikana na ugonjwa wa Covid 19.

Fainali ya kipute hicho itapigwa Februari 7 mwaka huu.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *