Chama cha Wiper chamteua Agnes Kavindu kuwania Useneta Machakos

Chama cha Wiper Democratic Movement kimemteua Agnes Kavindu Muthama kuwa mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa kiti cha Useneta wa Kaunti ya Machakos.

Kavindu amekabidhiwa cheti cha uteuzi na kuidhinishwa rasmi kupeperusha bendera ya chama hicho katika hafla iliyohudhuriwa na Kinara wa chama hicho Kalonzo Musyoka huko Karen.

Chama hicho kimeelezea matumaini ya kushinda uchaguzi huo, huku kikimsifu Kavindu kuwa mwanamke mwenye sifa za uongozi, mcha Mungu na mwenye kujitolea katika kuhudumia watu.

Agnes Kavindu akabidhiwa cheti cha uteuzi na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka

Kavindu aligombea kiti cha Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Machakos kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 na akaibuka nafasi ya pili.

Mnamo mwaka wa 2018, aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika kamati ya Mpango wa Maridhiano nchini, BBI.

Uchaguzi mdogo wa kiti cha Useneta katika Kaunti ya Machakos unatarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi Machi mwaka huu.

Kiti hicho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Seneta wa kaunti hiyo Boniface Kabaka mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita.

Kwenye hafla hiyo, chama cha Wiper pia kimemteua Sebastian Muli Munguti kuwa mgombea wa uchaguzi mdogo wa Mwakilishi Wadi ya Kitishe/Kithuki, katika Kaunti ya Makueni.

Hii ni baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Wadi hiyo Kelvin Mutuku Mutiua, aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama hicho cha Wiper, kujiuzulu mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita na kukiacha kiti hicho wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *