Chama cha Mawakili chashinikiza kuvunjwa kwa Bunge

Chama cha Mawakili humu nchini LSK kimemtaka Rais Uhuru Kenyatta azingatie ushauri wa Jaji Mkuu David Maraga wa kuvunja bunge kwa kushindwa kupitisha sheria ya usawa wa kijinsia.

Rais wa chama hicho Nelson Havi amesisitiza kuwa Maraga alifuata sheria kikamilifu alipomuandikia Rais kuhusu swala hilo.

Kulingana na Havi, ni wajibu wa Rais Kenyatta sasa kulivunja bunge kufikia tarehe 12 mwezi ujao ambapo itakuwa ni siku 21 tangu kutolewa kwa ushauri huo na Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa iwapo Rais hatafanya hivyo, basi atakuwa amekiuka matakwa ya kikatiba.

Chama hicho tayari kimeiandikia Wizara ya Fedha na kuitaka ikatize ulipaji wa mishahara kwa wabunge kufikia tarehe 12 Oktoba.

Nayo Wizara ya Maswala ya Ndani imetakiwa kuwaondoa maafisa wa usalama wanaowalinda wabunge kufikia siku hiyo iwapo bunge halitavunjwa.

Aidha, Chama cha Mawakili kimetishia kuwaongoza Wakenya katika hatua ya kuchukua nafasi katika majengo ya bunge ili wabunge wasipate nafasi ya kuendelea kuhudumu kwa lengo la kukomesha tabia ya kutoenenda kulingana na katiba ya nchi.

“Kumekuwa na tabia ya viongozi kukiuka matakwa ya katiba na sheria za Kenya. Katika juhudi za kuhakikisha Wakenya wanatekeleza mamlaka ya kikatiba, Chama cha Mawakili kitawaongoza kuchukua nafasi katika majengo ya bunge kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2020,” amesema Havi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *