Chama cha Ekeza chawafidia wanachama wake pesa walizowekeza

Wanachama wa Chama cha Ushirika cha Ekeza wameanza kurejeshewa pesa walizowekeza chamani humo zinazokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni mia saba.

Pesa hizo zimerejeshwa kufuatia agizo la serikali kuwa wanachama wafidiwe kabla ya chama hicho kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake mwaka ujao.

Chama cha Ekeza kimekuwa kikifanyiwa uchunguzi mwaka uliopita kufuatia ripoti kwamba takriban shilingi bilioni moja zilikuwa zimeporwa, hali iliyoleta wasi wasi kwamba huenda wanachama walioekeza pesa zao wakakosa kulipwa.

Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa chama hicho, Jimmy Kagoni, amethibitisha kuwa baadhi ya wanachama wamepokea pesa zao kupitia M-PESA na wale ambao hawajapokea watazipata hivi karibuni.

Wanachama wengine wamepatiwa vipande vya ardhi katika Kaunti mbali mbali kama njia ya kuwafidia.

Kulingana na Kagoni, zaidi ya asilimia 70 ya wanachama waliokuwa wanadai chama hicho wamelipwa.

“Tunataka kumaliza kuwalipa wanachama wetu wote kufikia mwezi Desemba ili mwaka ujao, Chama cha Ekeza kiweze kurejelea shughuli zake za kibiashara,” amesema Kagoni.

Kagoni amesema amewasilisha katika Idara ya Upelelezi wa Jinai majina ya watu 18 wanaoaminika kufuja mali ya chama hicho kwa ushirikiano na baadhi ya wafanyakazi wa chama hicho.

Amesema majina zaidi yatawasilishwa katika idara hiyo pindi uchunguzi utakapokamilika.

Mwaka uliopita, Idara ya Upelelezi iliwataka Wakenya waliokuwa wameekeza pesa zao chamani humo kuandikisha malalamishi yao ili chama hicho kishinikizwe kuwalipa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *