Categories
Michezo

Kenya wasajili ushindi wa kwanza kwa kuichakaza Msumbiji vikapu 79-62 mechi za kufuzu Fiba Afrobasket

Timu ya Kenya ya mpira wa kikapu maarufu kama Morans imekamilisha mechi za raundi ya kwanza katika kundi B kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket kwa ushindi baada ya kuwanyuka Msumbiji vikapu 79-62  Ijumaa jioni katika uwanja wa Kigali.

Morans walianza mchuano huo wakijua kuwa ni ushindi tu ungewaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu baada ya kupoteza mechi za kwanza mbili dhidi ya Senegal na Angola na wakalazimishwa kutoka sare alama 19-19 katika robo ya kwanza ya mchezo .

Hata hivyo Msumbiji waliimarika katika robo ya pili  na kuibwaga Kenya pointi 17-14 huku Kenya wakilipiza kisasi na kushinda robo ya tatu alama 23-17 na kudumisha ushindi kwenye  robo ya mwisho vikapu  23-14 .

Tyler Ongwae kwa mara nyingine tena aliibuka mfungaji bora wa vikapu kwa Kenya kwa kufunga 21 akifuatwa na Valentine Nyakinda aliyefunga vikapu 16  huku nahodha Erick Mutoro akirekodi vikapu 15.

Kenya inayofunzwa na kocha Cliff Owuor itarejea nchini mwishoni mwa juma hili ,kujiandaa kwa mechi tatu za raundi ya pili kundini B wakianza dhidi ya Senegal Februari 19 mjini Kigali Rwanda ,kabla ya kukutana na Angola Februari 20 na kufunga ratiba dhidi ya Msumbiji tena tarehe 21 mwezi Februari mwakani.

Timu tatu bora kutoka kundi hilo zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.

Categories
Michezo

Wana Mvinyo Tusker na Afc leopards kufungua msimu wa ligi kuu ya KFK Jumamosi

Ligi kuu ya shirikisho la soka nchini FKF msimu wa mwaka 2020/2021 utaanza rasmi Jumamosi hii  Novemba 28 ,kwa jumla ya mikwangurano mitatu Afc Leopards wakiikabili wagema mvinyo Tusker Fc katika uchanjaa wa Utalii saa tisa alasiri nao Vihiga United  wakaribishwe rasmi ligi na Kakamega Homeboyz katika uga wa Mumias Sports Complex saa tisa huku Bandari wakiwa nyumbani Mbaraki dhidi ya  Sofapaka  pia saa tisa.

Siku ya Jumapili Western Stima watafungua ratiba katika uwanja wa Moi kaunti ya Kisumu kwa kuwakaribisha rasmi ligini Bidco united saa saba adhuhuri kabla ya kupisha mechi nne sambamba kuanzia saa tisa mabingwa wa Nsl Nairobi City stars wakimenyana nyumbani Nyayo na Nzoia Sugar,Wazito Fc iwe ugenini kwa Kariobangi sharks katika uga wa Nyayo,nao kcb wazuru Sofapaka katika uwanja wa kaunti ya Narok.

Wanajeshi Ulinzi stars watafungua msimu Jumatano ijayo dhidi ya Mathare United huku Gor Mahia wakianza kutetea taji yao dhidi ya Zoo  Youth.

Msimu wa ligi kuu ulitamatishwa kighafla mwezi Machi mwaka huu kutokana na Janga la Covid 19 kabla ya msimu mpya ambao utaanza Jumamosi na kukamilika Mei mwakani.

Mabingwa wa ligi kuu  msimu huu watatunukiwa shilingi milioni 5 na kombe huku timu zote 18 ligini zikigawana shilingi milioni 5 nyingine kulingana na fasi yao ligini.

Pia kila timu itapokea shilingi milioni 10 kila msimu kutokana na ufadhili wa ligi.

 

 

 

 

 

 

Categories
Michezo

Kenya yaipiga kumbo Sudan na kutinga nusu fainali Cecafa

Timu ya taifa ya Kenya kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20, imefuzu kwa nusu fainali ya michuano ya Cecafa inayoendelea mjini Arusha

Tanzania, baada ya kuilaza Sudan mabao 2-1 katika pambano la mwisho la kundi C uwanjani Sheikh Amri Abeid .

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia kwa sare tasa ,Fortune Omoto aliondoa ukame  wa mabao kwa bao la dakika ya 62 kwa Kenya , lakini zikisalia dakika tano mechi ikatike Ali Gozoli Nooh akavunja nyoyo za wakenya kwa bao kusawazisha .

Hata hivyo Benson Ochieng alipachika bao la dakika ya 92  na kuhakisha Kenya maarufu kama rising stars ,wanamaliza kwenye nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 6 kutokana na mechi mbili na kufuzu kwa nusu fainali ya Jumatatu  dhidi ya Hippos kutoka Uganda huku Tanzania walioongoza kundi A wakiweka miadi ya kumenyana na  Sudan kusini katika nusu fainali ya pili pia Jumatatu.

Nahodha wa Kenya na Sudan wakiwa na waamuzi kabla ya mechi

Timu ya kwanza na ya pili katika michuano hiyo ambayo fainali yake  itapigwa Disemba 2 zitafuzu kushiriki mashindano ya kombe la Afcon kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka ujao nchini Mauritania.

Rising Stars walikuwa wamesajili ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Ethiopia.

 

Categories
Michezo

Ahly na Zamalek kuzindua uhasama wa jadi fainali ya ligi mabingwa Ijumaa

Fainali ya ligi ya mabingwa barani afrika itasakatwa Ijumaa usiku katika uwanja wa Cairo International ,ikiwa derby ya Cairo baina ya mabingwa mara 8 Al Ahly dhidi ya Zamalek kuanzia saa nne usiku.

Timu hizo zitakutana kwa mara ya 9 katika kombe hilo la ligi ya mabingwa, Ahly wakiibuka washindi mara  5 na nyingine 3  kuishia sare, lakini zote  zikiwa aidha mechi za makundi au nusu fainali.

Itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika fainali ya kombe  hilo  zikiwania dola milioni 2 nukta 5 na fursa ya kucheza kombe la dunia baina ya vilabu.

Katika mechi za nyumbani timu hizo zimepambana mara  215 Ahly maarufu kama  Red Devils wakishinda mechi  91 ,huku Zamalek wajulikanao kama White Knights wakisajili ushindi kwenye michuano  50  na kurekodi sare 74 .

Ahly wamenyakua ligi ya mabingwa mara 8  ikiwa timu iliyoshinda taji hiyo mara nyingi zaidi na kushinda mataji 4  ya kombe la shirikisho,4 ya African Cup winners cup   na lile la super cup mara 4  kwa jumla wakiwa na vikombe 19 vya Afrika.

Hata hivyo Red Devils wamekawia tangu mwaka 2014 ikiwa mara ya mwisho kwao kunyakua kombe la shirikisho huku yale ya ligi ya mabingwa yakiwakwepa na ndiyo timu iliyokawia muda mrefu zaidi kabla ya kushinda kombe la ligi ya mabingwa.

Al Ahly wakiwa mazoezini

Upande wa pili wa sarafu Zamalek wamewshinda mataji matano ya ligi ya mabingwa ,4 ya Super Cup na moja ya shirikisho na nyingine moja ya African cup winners cup wakiwa na vikombe 11 vya Afrika.

Zamalek iliibuka ya pili katika kundi A nyuma ya Toupiza Mazembe  kabla ya kuwatema waliokuwa mabingwa matetezi Esperance ya Tunisia jumla ya mabao 3-2 katika robo fainali na kuwabandua Raja Casablanca jumla ya mabao 4-1 kwenye nusu fainali.

Ahly nao waliibuka wapili kundini B nyuma ya Etoile du Sahel kabla ya kuibwaga Mamelodi Sundowns magoli 2-1 katika kwota fainali na hatimaye kuwadhalilisha mabingwa wa Moroko Wydad Casblanca  kwa kuwalabua mabao 5-1 katika nusu fainali.

Kocha wa Afrika Kusini Pitso Mosimane alishika hatamu za kuwanoa  Ahly  mwezi Septemba  mwaka huu akitokea Mamelodi Sundowns ya nyumbani ambao alishinda nao kombe hilo la ligi ya mabingwa mara moja .

Jaime Pacheco wa kutoka Ureno alirejea kuwafunza Zamalek pia mwezi Septemba mwaka huu  akiwa hana kazi tangu aigure timu hiyo mwaka 2014.

Zamalek wakiwa mazoezini

Misri itanyakua kombe hilo la ligi ya mabingwa Ijumaa usiku  kwa mara ya 15  likiwa taifa pekee kunyakua mataji mengi zaidi kwani awali Zamalek wameibuka mabingwa mara 5 nao Ahly wakashinda mara 8 wakati Ismaily ikishinda kombe moja.

Ahly wameshinda kombe la ligi ya mabingwa mwaka 1982 ,1987,2001,2005,2006,2008,2012 na 2013  na kupoteza fainali mara 4 ,ya mwisho ikiwa mwaka 2018.

Zamalek wametawazwa mabingwa miaka ya 1984 ,1986 ,1993,1996 na 2002  na kushindwa katika fainali mara mbili  ya mwisho ikiwa 1996.

Fainali hiyo kati ya Al Ahly  na Zamalek itapeperushwa mbashara kupitia KBC Channel one kuanzia saa nne usiku

 

 

 

Categories
Michezo

Tanzania waikomoa Somalia 8-1 na kutinga nusu fainali ya Cecafa

Mabingwa watetezi wa kombe la Cecafa Tanzania  wametinga nusu fainali ya makala  ya mwaka huu kwa vijana walio na umri usiozidi miaka 20  ,baada ya kuidhalilisha Somalia  mabao 8-1 katika mechi ya  kundi A iliyosakatwa Alhamisi jioni katika uwanja  Black Rhino Academy Complex mjini Arusha Tanzania.

Ngorongoro Heroes wanavyojulikana wenyeji Tanzania walipata mabao yao kupitia kwa   Abdul Hamisi Suleiman kunako dakika ya 4, kabla ya Sahal Muhammed kuwarejesha Somalia mchezoni kwa bao la kusawazisha  na  dakika mbili baadae Ben Starki akapachika la pili dakika ya 15 huku  Kelvin John akifunga bao la tatu  na la nne na kipindi cha kwanza kumalizika kwa uongozi wa Tanzia wa mabao 4-1.

Wachezaji wa Tanzania wakisherehekea bao

Wabongo walianza kipindi cha  pili kwa makeke na kufumania nyavu za Somalia  katika dakika ya 47 kupitia kwa Kasim Shaaban kabla ya Kelvin Jonh kuhitimisha Hatrick kwa abo la dakika ya 60  nao Frank George na Anuar Jabir wakiongeza mabao mengine mawili.

Tanzania wameongoza kundi  A kwa alama 6 baada ya awali kuwaadhibu Djibouti mabao 6-1 katika mechi ya ufunguzi .

Timu mbili bora katika mashindano hayo zitafuzu kwa mashindano ya Afcon mwaka ujao nchini Mauritania.

 

Categories
Michezo

Morans wapakatwa na Angola michuano ya kufuzu kwa Fiba Afrobasket

Matumaini ya timu ya taifa ya Kenya katika mpira wa kikapu almaarufu the Morans  kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao yalididimia baada ya kuambulia kichapo cha pointi 66-83 kutoka kwa Angola katika mechi ya pili ya kundi B  ya  kufuzu, iliyosakatwa Alhamisi Alasiri  katika uwanja wa Kigali  Rwanda.

Morans walipoteza robo ya kwanza ya mchezo pointi 10-18 na ya pili 15-21, lakini wakanyong’oyea zaidi katika robo ya tatu walipocharazwa alama 13-29.

Mabadiliko kadhaa  ya kiufundi kutoka kwa kocha Cliff Owuor yaliimarisha mchezo wa Wakenya  waliojizatiti na kunyakua ushindi katika kwota ya mwisho ya mchezo alama 28-15 ingawa tayari maji yalikuwa yamezidi unga.

Reuben Mutoro na Tyler Ongwae walikuwa wafungaji bora wa pointi kwa Kenya ,kila mmoja akizoa alama 18 .

Nahodha wa kenya Mutoro amesema walicheza vizuri dhidi ya Angola kuliko dhidi ya Senegal huku akiahidi kwamba wataimarisha mchezo wao zaidi dhidi ya Msumbiji Ijumaa “Tulicheza vyema katika mechi ya leo kinyume na  mechi ya Jumatano ,naamini kuwa  tutarudi kufanya utafiti na kujitayarisha vyema dhidi ya Msumbiji  ambao nina imani tutaimarika zaidi na kupata ushindi”akasema Mutoro

“Kwetu sisi mechi ya Msumbiji ni kama fainali tutajituma kwa asilimia 100 kwani hatuna kingine cha kuhofia au kutuzuia na baada ya hapo tutangoja raundi ya pili mwaka ujao”akaongeza Mutoro

Kwa upande wake kocha Owuor amesema kuwa alijaribu kurekebisha makosa mengi waliyofanya dhidi ya Senegal ,walipochuana na Angola na ameahidi kwamba analenga ushindi katika mechi ya mwisho Ijumaa dhidi ya Msumbiji kabla ya kurejea kwa raundi ya pili Februari mwaka ujao.

”Tumekuwa na makosa mengi uwanjani ,ukiangalia tumekuwa tukipoteza mpira kwa urahisi na pia walinzi wetu hawajamakinika ipasavyo,lakini nafurahia mchuano wetu wa leo umekuwa bora kuliko ule dhidi ya Senegal.Kwa sasa tunajiandaa kucheza na Msumbiji tutafute matokeo bora halafu turejee tena Februari mwaka ujao kwa raundi ya pili”akasema kocha Owour

Ushinde wa Morans  dhidi ya Angola ulikuwa wa pili mtawalia katika kundi B kwenye mashindano hayo ,baada ya kulazwa pointi 54-97 katika pambano la ufunguzi siku ya Jumatano.

Hii ina  maana kuwa Kenya ni sharti waishinde Msumbiji katika mchuano wa mwisho Ijumaa hii kuanzia saa kumi na mbili jioni ,ili kuwa na fursa ya kutinga mashindano ya Fiba Afrobasket mwakani nchini Rwanda.

Angola wanaongoza kundi hilo baada ya kushinda mechi ya pili walipowaangusha  Msumbiji Jumatano usiku katika mechi ya kwanza.

Katika mechi ya pili Alhamisi Nigeria imeibwaga Sudan Kusini pointi 76-56  katika kundi D.

Mkondo wa kwanza wa mechi za makundi   utakamilika Jumapili ijayo kabla ya mkondo wa pili kuanza Februari 19 mwaka ujao.

Timu tatu bora kutoka kila kundi baada ya mechi 6 za makundi zitafuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mwaka ujao nchini Rwanda.

Categories
Michezo

Maombolezo ya siku tatu yatangazwa Argentina kufuatia kifo cha Maradona

Maombolezo  ya kitaifa ya siku tatu yameanza leo nchini Argentina kufuatia kifo cha gwiji wa soka Diego Maradona Jumatano jioni.

Maelfu ya watu wamejitokeza katika kasri ya Rais kuutazama mwili wa marehemu na kutoa heshima zao za mwisho mapema Alhamisi, huku wengine wakiingia barabarani Jumatano usiku kuomboleza kwa kulia ,kuimba nyimbo ,kuwasha baruti huku wengine wakisherehekea maisha ya marehemu kwa kunywa pombe kwenye  barabara za mji mkuu wa Argentina Beunos Aires.

Mashabiki wengi walikusanyika katika uwanja wa Bombonera ambao hutimika na kilabu cha Boca Juniors kuomboleza  kifo cha nguli huyo kati ya jumatano usiku na Alhamisi.

Maradona alifarika Jumatano jioni akiwa na umri wa miaka 60  kutokana na mshtuko wa moyo na ameacha kumbukumbu ulimwenguni kwa bao la hand of God lililoipa Argentina ushindi dhidi ya Uingereza kwenye fainali za kombe la dunia mwaka 1986  huku akiiwezesha timu yake kunyakua kombe la dunia kwa mara ya kwanza akiwa nahodha.

 

 

Categories
Michezo

Mvutano kati ya FKF na timu 4 watishia kuathiri msimu mpya wa ligi kuu

Shirikisho la kandanda nchini Fkf litaziadhibu  timu ambazo hazitasaini mkataba wa  kupeperusha mechi za ligi kuu inayotazamiwa kuanza Jumamosi hii.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi  mapema Alhamisi ,mwenyekiti wa Fkf Nick Mwendwa amesuta vilabu vinne ambavyo havijasaini mkataba huo wa matangazo ya runinga akisisitiza kuwa vimepewa nafasi ya mwisho kubatilisha misimamo yao mikali na kuruhusu ligi kuanza bila tashwishwi.

Rais wa FKF Nick Mwendwa akizungumza wakati wa kuzindua mkataba baina ya FKF na Star Times

“Sisi tuko tayari kuanza ligi Jumamosi bila hizo timu nne ambazo hazijasaini mkataba huo,lakini pia tunawapa nafasi ya kufikiria upya kuhusu uamuzi wao ,la sivyo tutachukua hatua kama shirikisho wiki ijayo,hakuna vile timu hizo zitazuia ligi kuanza”akasema Mwendwa

Mwendwa amekariri kuwa haki zote za ligi ya Kenya zinamilikiwa shirikisho na wala sio za vilabu inavyodaiwa .

“Fkf ndio wameliki wa haki zote za soka humu nchini na pia ligi ya Fkf Premier League,kwa hivyo tusidanganyane ,si bado tunaomba timu za Zoo Fc,Gor Mahia ,Mathare United na Ulinzi Stars kutafakari na kubadilisha msimamo wao ligi ianze vijana wapate doo”akaongeza Mwendwa

Nick mwendwa akiwa na CEO wa Star Times  Hanson Wang katika uzinduzi wa mkataba ligi kuu FKF

Fkf imezindua mkataba wa miaka 7 na kampuni ya Star Times ya kutoka China ili kupeperusha mechi za ligi kuu ambapo inatarajiwa kuwa angaa mechi 100 zitarushwa kwenye runinga kila msimu .

Hata hivyo kwenye mahojiano na Kbc kwa njia ya simu mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier ameapa kuelekea mahakamani kusimamisha mkataba huo wa runinga na kupinga hatua ya Fkf Kumiliki haki zote za vilabu.

“Mimi kwa sasa sina wakati wa kujibizana na Fkf lakini nitafuata mkondo wa sheria ambapo nitaelekea mahakamani kutaka kusimamishwa kwa mkataba huo kwa sababu haki za vilabu hazipaswi kutwaliwa na shirikisho”akasema Rachier

Utata huo huenda ukaibuka mvutano mkubwa kwenye ligi kuu ambayo iliratibiwa kuanza Jumamosi hii ambapo jumla ya mechi 3 zimeratibiwa kupeperushwa kupitia Runinga ya Star Times.

 

Categories
Michezo

Diego Maradona aaga dunia akiwa na umri wa miaka 60

Nguli wa soka  Diego Armando kutoka Argentina amefariki dunia Jumatano jioni  kutokana na mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 60.

Maradona ameaga dunia akiwa nyumbani kwake kwa mjibu wa wakili wake ikiwa wiki mbili tangu aondoke hospitalini alikofanyiwa upasuaji wa ubongo .

Maradona anatambulika kama mmoja wa wanasoka maarufu na shupavu wa karne hii alipoisaidia Argentina kunyakua kombe la dunia  mwaka 1986 akiwa nahodha .

Pia marehemu anakumbukwa kwa kufunga bao kwa mkono bao lililoibandua Uingereza katika robo fainali ya kombe la dunia  mwaka 1986  na kuliita bao hilo ‘Hand of God’ .

Maradona akifunga bao kwa mkono kwenye robo fainali ya kombe la dunia mwaka 1986 dhidi ya Uingereza

Anakumbukwa pia kwa kutimuliwa kwenye fainali za kombe la dunia mwaka 1994 kwa kupatika kuwa mtumizi wa dawa zilizoharamishwa zinazopatika katika dawa ya kulevya ya Cocaine.

Masaibu yake yalianza kuongezeka  baada ya kusataafu kutoka soka iliporitowa kuwa alikuwa mraibu wa dawa za kulenya haswa Cocaine na pia mlevi wa starehe zilizochangia  matatizo ya yake mengi ya kiafya ikiwemo tatizo la mshtuko wa moyo .

Maradona akibeba kombe la dunia akiwa nahodha wa Argentina mwaka 1986

Katika enzi zake za usakati kambumbu Maradona alinyakua taji ya ligi kuu Italia Serie  A akiwa na kilabu cha Napoli miaka ya 1987 na  1990, kombe la Italia mwaka  1987 na lile la  Uefa Cup mwaka  1991.

Hadi kifo chake Maradona amekuwa mkufunzi wa kilabu cha Argentina Gymnasia Esgrima na alikuwa tayari amefanyiwa upasuaji mara mbili.

MOLA AILAZE ROHO YAKE MAHALA PEMA

 

 

 

Categories
Michezo

Morans wanyanyaswa na Senegal 54-92 Fiba Afrobasket nchini Rwanda

Timu ya taifa ya Kenya ya mpira wa kikapu, ilianza vibaya mechi za kufuzu kwa mashindano ya Fiba Afrobasket mjini Kigali Rwanda baada ya kucharazwa pointi 92 -54 katika mchuano uliosakatwa katika uwanja wa Kigali Arena Jumatano jioni.

Kenya maarufu kama Morans walianza vyema pambano hilo ,huku wakilazimisha sare ya alama 19-19 katika robo ya kwanza ya mchezo ,kabla ya kulegea katika robo ya pili walipopoteza alama  14-28  na kisha Morans wakasajili ushindi wa pointi  19-14 katika robo ya tatu ikiwa robo pekee ya mechi iliyoshindwa na Kenya.

Hata hivyo  Morans wanaofunzwa na kocha Cliff Owuor walizidiwa maarifa kwenye robo ya mwisho walipozabwa alama 2-34 wakiwa na makosa mengi ya safu ya ulinzi huku pia wakikosa kumakinika wakati wa kufunga na pia zikiwa alama za chini zaidi walizosajili katika robo moja na pia kufungwa pointi nyingi zaidi .

Licha  ya kocha Owuor kuitisha muda wa mapumziko ili kujaribu kuimarisha mchezo, dau la Kenya lilionekana kuzama kila wakati haswa wakipoteza nafasi nyingi za kufunga alama tatu maarufu kama 3 pointer na pia alama 2.

Katika mchuano huo uliorushwa mbashara na runinga ya Kbc Channel 1 , Tyler Ongwae aliibuka mfungaji bora wa Kenya kwa kuzoa pointi 13 huku Ibrahim Faye akiizolea Senegal alama za juu zikiwa 19.

Vijana wa Morans sasa watakuwa na muda wa chini ya saa 24 kujitayarisha na kurekebisha makosa yao, kabla ya kurejea uwanjani kukabiliana na miamba wa Afrika Angola Alhamisi alasiri na  kufunga ratiba dhidi ya Msumbiji Ijumaa.

Kenya hawana budi kushinda angaa mechi moja ili kuwa na nafasi ya kufuzu kwa fainali za mwaka ujao, ambapo timu tatu bora kutoka kila kundi zitacheza kipute cha Fiba Afrobasket.