Categories
Kimataifa

Ufaransa yaapa kuimarisha juhudi za kupambana na Corona hadi mwaka ujao

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema taifa hilo litaendelea kupambana na janga la korona hadi katikati ya mwaka ujao.

Tangazo hilo limetolewa huku visa vya maambukizi nchini humo vikipita watu milioni moja.

Siku ya Ijumaa Ufaransa ilirekodi zaidi ya visa 40,000 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na jumla ya vifo 298.

Mataifa mengine ambayo yamerekodi ongezeko la visa vipya vya ugonjwa huo ni Urusi, Poland, Italia na Uswizi.

Shirika la Afya duniani WHO limesema huu ni wakati muhimu kwa mataifa ya Ulaya kuimarisha mbinu za kuzuia msambao wa ugonjwa huo na kuhakikisha kuwa mitandao ya huduma za afya inakabiliana vilivyo na janga hilo.

Idadi ya wastani ya kila siku ya maambukizi ya ugonjwa huo imeongezeka mara dufu katika muda wa siku kumi zilizopita.

Bara la Ulaya sasa limerekodi visa  milioni 7.8 vya ugonjwa huo na karibu  vifo vya watu 247,000.

Kimataifa, jumla ya visa milioni 42 vya mambukizi ya ugonjwa huo vimerekodiwa na vifo milioni 1.1.

Akiongea katika hospitali moja jijini Paris, Rais Macron amesema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa magonjwa nchini humo, ugonjwa huo huenda ukasalia nchini humo hadi katikati ya mwaka ujao.

Ufaransa imeongeza tena muda wa makataa ya kutotoka nje usiku kwa majuma sita.

Categories
Kimataifa

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aagiza kukomeshwa kwa ghasia nchini humo

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia zinazokumba taifa hilo.

Hata hivyo Rais huyo hakugusia madai ya mauaji ya waandamanaji yaliotekelezwa na maafisa wa polisi ambayo yameshtumiwa na jamii ya kimataifa na kuibua machafuko Jijini Lagos.

Rais Buhari aliwatahadharisha waandamanaji dhidi ya kuvuruga usalama.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Buhari kuzungumzia kuhusu ghasia hizo ambapo aliwalaumu watu aliosema wameteka maandamano hayo na kuendeleza ajenda zao.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 77 aliwahimiza vijana kukomesha maandamano na kushauriana na serikali ili kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo.

Jiji la Lagos limeshuhudia visa vya milio ya risasi, uporaji mali na kuteketezwa kwa gereza moja tangu maafisa wa usalama walipokabiliana na waandamanaji wanaoshinikiza mabadiliko ya uongozi na kukomeshwa kwa dhuluma za polisi katika jiji hilo lenye wakazi milioni 20.

Marekani, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyoshutumu matumizi ya nguvu kuwatawanya waandamanaji.

Categories
Kimataifa

Waathiriwa wa maandamano nchini Nigeria kutendewa haki

Naibu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo, ameahidi kutendewa haki kwa waandamanaji waliouawa au kujeruhiwa wakati wa maandamano ambayo yamefanyika nchini humo kwa kipindi cha siku chache zilizopita.

Mashahidi walisema kwamba wanaume waliokuwa wamevalia sare za kijeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji Jumanne jioni mjini Lagos.

makamu huyo wa Rais amesema maafisa kadhaa wa polisi pia waliuawa wakati wa makabiliano na waandamanaji hao.

Hakikisho lake limejiri kufuatia shutuma dhidi ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waandamanaji ambao awali walikuwa wakitaka mabadiliko kutekelezwa kwenye kikosi cha polisi lakini sasa wanataka mabadiliko ya uongozi nchini humo.

Wakati huo huo Muungano wa Afrika umeshutumu vikali mashambulizi dhidi ya waandamanaji wanaolalamikia dhuluma za polisi nchini Nigeria.

Mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki, amezihimiza pande husika kwenye mzozo huo kuheshimu haki za binadamu na sheria.

Categories
Kimataifa

Polisi nchini Nigeria washtumiwa kwa mauaji ya waandamanaji Lagos

Watu kadhaa waliokuwa wakiandamana kulalamikia dhuluma za maafisa wa polisi wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa jijini Lagos, Nigeria.

Walioshuhudia wanadai kuwa watu 12 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi wakati wa maandamano hayo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty, limesema limepokea taarifa za kuaminika kuhusu mauaji hayo.

Rais Muha-Mmadu Buhari amewahimiza raia wa nchi hiyo kuwa watulivu huku amri ya kutotoka nje ikitangazwa katika jiji la Lagos na maeneo mengine.

Hali ya wasi wasi imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbali mbali ya mji wa Lagos baada ya polisi kulazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji wanaokaidi amri hiyo.

Maandamano dhidi ya kikosi cha kukabiliana na wizi wa mabavu, SARS, ambacho tayari kimevunjiliwa mbali, yamekuwa yakiendelea nchini Naijeria kwa majuma kadhaa.

Categories
Kimataifa

Mpenzi wa Jamal Khashoggi amtaka Mohammed bin Salman kufidia mauaji ya mwanahabari huyo

Mpenzi wa mwanahabari wa Saudi aliyeuawa Jamal Khashoggi na shirika la kutetea haki za binadamu aliloanzisha aliwasilisha kesi katika mahakama moja ya marekani jana akidai kwamba mridhi wa ufalme wa Saudi Arabia ndiye aliyeamuru kuuawa kwa mwanahabari huyo.

Kesi hiyo inayomtaka mridhi wa ufalme Mohammed bin Salman afidie mauaji ya mwanahabari huyo,pia imewaorodhresha mashahidi 20 wa Saudia.

Kesi hiyo imewasiishwa wakati ambapo uhusiano kati ya marekani na Saudi umezorota kufuatia mauaji ya Khashoggi mwaka 2018,ukiukaji wa haki za binadamu na kuhusika kwa saudia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini nchini Yemen.

Mridhi huyo wa ufalme amekanusha madai ya kuagiza kuuawa kwa  Khashoggi.

Afisa wa uchunguzi wa umoja wa mataifa awali alisema kuwa Salman anapaswa kuchunguzwa akitaja kuna ushahidi kuwa yeye na maafisa wengine wa Saudi walihusika.

Categories
Kimataifa

Trump atoa masharti ya kuiondoa Sudan katika orodha ya wanaofadhili ugaidi

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ataoindoa Sudan kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi ikiwa taifa hilo litakubali kulipa fidia ya dola milioni 335 kwa familia za raia wa Marekani walioathiriwa na mashambulizi ya kigaidi.

Hatua hii pia inatarajiwa kuanzisha utaratibu wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Sudan na Israel kufuatia makubaliano sawia kati ya taifa hilo na Muungano wa Milki za Kiarabu na Bahrain.

Hata hivyo mazungumzo hayo bado yanaendelea kuhusu mkataba huo.

Sudan iliorodheshwa miongoni mwa mataifa yanayofadhili vitendo vya kigaidi wakati wa enzi ya aliyekuwa rais Omar al- Bashir aliyeondolewa mamlakani.

Hatua hiyo bado inainyima serikali ya sasa ya mpito ruzuku na ufadhili wa kigeni inayohitaji kuendeleza shughuli zake.

Categories
Kimataifa

Maandamano ya amani yatibuka Chile baada ya wahuni kutumia fursa hiyo kutekeleza uhalifu

Mandamano ya kupinga hali ya kutokuwepo kwa usawa nchini Chile yamegeuka kuwa ghasia baada ya wahuni kutumia fursa hiyo kuchoma makanisa mawili.

Aidha makao makuu ya polisi yameshambuliwa kwa bomu la petroli na maduka kadhaa kuporwa.

Maandamano hayo yanaadhimisha mwaka mmoja tangu maasi ya umma kutokea katika taifa hilo kwa miezi miwili mfululizo.

Waandamanaji hao wamewataka raia kupiga kura ya kubuni katiba mpya wakati wa kura ya maamuzi itakayoandaliwa mwishoni mwa juma lijalo.

Maafisa 18 wa polisi walijeruhiwa kwenye ghasia hizo, huku Waziri wa Mashauri ya ndani Victor Perez akihimiza raia kuwasilisha matakwa yao kupitia kura ijayo ya maamuzi.

Ghasia zilitokea nchini humo mara ya kwanza mnamo mwezi wa Oktoba mwaka jana ambapo maandamano yalifanywa kila siku kisha yakapungua kutokana na mchipuko wa virusi vya korona.

Maandamano hayo yalitokana na gharama ya juu ya maisha kufwatia ongezeko la gharama ya usafiri katika mji mkuu wa nchi hiyo Santiago.

Hata hivyo maandaamano hayo yaliongezeka kutokana na gharama kubwa ya huduma za afya na bajeti duni kwa sekta ya elimu

Categories
Kimataifa

Mwanaharakati aachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa miaka miwili Misri

Mwanablogu na mchoraji vibonzo mmoja nchini Misri, ameachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa zaidi ya miaka miwili.

Shadi Abu Zeid, mwenye umri wa miaka 27, alikamatwa mwezi Mei mwaka wa 2018 kuhusiana na madai ya kueneza habari za uongo na kuwa mfuasi wa kundi la kigaidi.

Shughuli zake ziliangazia maswala ya kidini, jinsia na familia nchini misri.

Katika miaka ya hivi karibuni, mamia ya wanaharakati na wanablogu wamepatikana na hatia ya kueneza habari za uongo, na kulisaidia kundi la Muslim Brotherhood lililopigwa marufuku.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yamemshtumu Rais Abdul Fattah Al-Sisi kwa kuruhusu msako mkali dhidi ya waasi, baada ya kuongoza jeshi kupindua serikali ya kiongozi wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini humo mwaka wa 2013.

Abu Zeid alianza kuchapisha kipindi chake cha vibonzo cha ‘The Rich Content’ kwenye mitandao ya YouTube na Facebook mwaka wa 2015.

Kipindi hicho kilijumuisha matamshi ya dhihaka na mahojiano yasiyo rasmi yaliyoangazia maswala mbalimbali ya kijamii kama vile mitazamo isiyofaa ya kidini na dhuluma za kimapenzi.

Categories
Kimataifa

Wananchi wa Guinea wapiga kura kumchagua rais

Raia wa Guinea wanapiga kura kwenye uchaguzi wa urais leo huku Rais Alpha Condé mwenye umri wa miaka 82 akitaka awamu ya tatu.

Muda wa kampeni ulikamilika Ijumaa usiku wa manane katika nchi hiyo huku kukiwa na wasi wasi wa kuzuka kwa vita baada ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia kambi ya kijeshi nchini humo na kumwua kwa kumpiga risasi afisa mkuu wa kijeshi.

Rais Condé alishinikiza kupitishwa kwa katiba mpya mwezi Machi akisema katiba hiyo itaboresha nchi hiyo, hatua ambayo pia ilimwezesha kukwepa sharti la rais kuhudumu kwa hatamu mbili.

Baada ya kuwa mwanaharakati wa upinzani kwa miongo kadhaa , Condé aliibuka kuwa rais wa kwanza  Guinea kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia mwaka 2010 na akashinda uchaguzi mwingine ulioandaliwa mwaka  2015.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakimkosoa rais huyo huku wakimtuhumu kwa kuwa dikteta.

Condé anakabiliana na mpinzani wake wa muda mrefu Cellou Dalein Diallo, ambaye tayari amemshinda katika chaguzi mbili.

Diallo, mwenye umri wa miaka 68, ambaye sasa ndiye kiongozi wa upinzani nchini  Guinea alikuwa waziri mkuu chini ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Lansana Conté.

Takriban wapiga kura mlioni 5.4 wanashiriki katika zoezi hilo huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa baada ya siku chache.

Ili kushinda urais moja kwa moja, mgombea anatakiwa kupata zaidi ya nusu ya kura hizo, vyenginevyo kutakuwa na awamu ya pili ya kura ya urais mnamo tarehe 24 Nonvemba mwaka huu.

Categories
Kimataifa

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ashinda hatamu ya pili mamlakani

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amepata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Huku kura nyingi zikiwa zimepigwa chama cha Leba cha Arden kimeshinda asilimia 49 ya kura na anatarajiwa kushinda viti vingi bungeni.

Chama cha upinzani cha  National Party, ambacho hadi sasa kina asilimia  27 ya kura kimekubali kushindwa.

Matokeo tangulizi yanaashiria kuwa  Ardern anaelekea kushinda hatamu ya pili mamlakani.

Hakuna chama kimewahi fanikiwa kupataa ushindi wa aina hiyo nchini New Zealand tangu nchi hiyo ilipoanzisha mfumo wa uongozi wa bunge mwaka 1996.

Zaidi ya asilimia 30 ya kura imepigwa na chama cha Leba cha Ardern kimeshinda takriban asilimia 50 ya kura hizo kulingana na tume ya uchaguzi.

Ushindi huo utawapa zaidi ya nusu ya viti katika bunge la kitaifa.