Categories
Kimataifa

Marekani yatilia shaka matokeo ya uchaguzi nchini Guinea

Marekani imeibua wasiwasi kuhusiana na kutofautiana kwa matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Guinea.

Kwenye taarifa ubalozi wa marekani umesema hakuna uwazi katika ujumlishaji wa kura na pia tofauti katika matokeo yanayotangazwa na yale ya  hati zinazowasilishwa kutoka kwa vituo vya kupigia kura.

Kiongozi wa Guinea mwenye umri wa miaka  82 Alpha Condé alishinda kipindi cha tatu uongozini kwa njia tata kulingana na matokeo ya awali huku maandamano yakizuka kote nchini humo.

Marekani imehimiza pande zote kusuluhisha kwa amani mizozo ya kiuchaguzi kupitia taasisi husika.

Marekani ilisema  imeunga mkono juhudi za kidiplomasia zinazotekelezwa na jumuia ya Ecowas,muungano wa Afrika pamoja na umoja wa mataifa wa kurejesha amani katika taifa hilo.

Kinara mkuu wa upinzani Cellou Dalein Diallo alijitangaza kuwa mshindi kwenye uchaguzi huo na alizuiwa kuondoka kwenye nyumba yake hadi Jumatano wakati ambapo alisema maafisa wa usalama waliokuwa nje ya nyumba yake waliondolewa.

Categories
Kimataifa

Rais wa Afrika Kusini ajitenga baada ya mtu waliyekutana kupatikana na Corona

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amejitenga baada ya mgeni aliyetangamana naye Jumamosi kupatikana na virus vya Corona.

Kulingana na taarifa kutoka afisi ya rais nchini humo, Rais Ramaphosa hajaonyesha dalili zozote za ugonjwa wa COVID-19 na atapimwa iwapo ataanza kuonyesha dalili hizo.

Siku ya Jumamosi, rais huyo alihudhuria hafla ya kuchangisha pesa iliyoandaliwa na Wakfu wa Adopt-a-School, ilihudhuriwa na jumla ya wageni 35 katika hoteli moja mjini Johannesburg.

Jumapili, mmoja kati ya wageni waliohudhuria hafla hiyo alionyesha dalili za ugonjwa huo, akapimwa Jumatatu na Jumanne akapokea matokeo ya kuonyesha kuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Wageni wote waliohudhuria hafla hiyo walifahamishwa kuhusu kisa hicho jana na wakalazimika kujitenga, akiwemo Rais Ramaphosa.

Kulingana na taarifa hiyo kutoka afisi ya rais, kanuni za kuzuia mamabukizi ya virusi vya Corona zilizingatiwa kikamilifu kwenye hafla hiyo.

“Hafla hiyo ilizingatia kanuni za COVID-19 ikiwemo uchunguzi wa joto la mwilini, wageni kukaa mbali mbali na uvaaji wa barakoa. Kama wageni wengine wote, Rais alivua barakoa wakati wa chakula na alipokuwa akihutubia wageni tu,” inaeleza taarifa hiyo.

Rais huyo ametuma jumbe za kheri kwa mgeni aliyepatikana na virusi hivyo ambaye anapokea matibabu, akimuombea uponyaji wa haraka na pia kuwatakia wageni wengine afya njema.

Ramaphosa ataendelea kutekeleza majukumu yake kutoka mahali alipojitenga na atazingatia muongozo wa kuhusu karantini kikamilifu.

Categories
Kimataifa

Vikwazo viliyowekewa Sudan vyaondolewa na Marekani

Serikali ya Marekani imeondoa vikwazo vya muda wa miaka 23 vilivyowekewa Sudan baada ya nchi hiyo kutoa hakikisho kwamba haitaunga mkono vitendo vya ugaidi wa kimataifa siku za usoni.

Rais Donald Trump kwenye taarifa alisema hatua hii inajiri baada ya Sudan kulipa fidia ya dolla milioni 325 kwa waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi.

Vikwazo hivyo vilizuia shughuli zozote kutekelezwa kwa kutumia sarafu ya Marekani.

Hii ilimaanisha kwamba kampuni yoyote ya kibiashara iliyokuwa nchini Marekani haingelifanya biashara na Sudan.

Kutokana na hatua hii, Sudan sasa iko huru kuafikia mikataba ya kibiashara na Marekani na makampuni makubwa ya mataifa ya magharibi tangu mwaka wa 1997 wakati ilipowekewa vikwazo hivyo.

Hatua hii pia inamaanisha kuwa Sudan sasa inaweza kutafuta mikopo kutoka mashirika ya kimataifa ya utoaji mikopo, kuwaalika wawekezaji nchini humo na kununua vipuri vya kukarabati viwanda na ndege zake za kale za shirika lake la kitaifa la ndege.

Sudan chini ya serikali ya mseto ya waziri mkuu Abdalla Hamdok ililazimika kulegeza msimamo wake ili kuafikia maridhiano na serikali ya Marekani.

Categories
Kimataifa

Jaji Amy Coney Barrett aidhinishwa kuwa jaji wa mahakama ya juu Marekani

Bunge la Seneti nchini  Marekani limeidhinisha uteuzi wa  Jaji Amy Coney Barrett kuwa  jaji wa  Mahakama ya Juu, hatua ambayo ni  ushindi kwa Rais Donald Trump wa  nchi hiyo  wiki moja kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo.

Maseneta wanachama wa  chama  cha Rais Trump cha Republican walipiga kura 52 dhidi ya 48 kuimuidhinisha jaji huyo  na  kuwashinda wapinzani wao wa chama cha Democrat.

Jaji huyo wa umri wa  miaka 48 alikula kiapo  katika  Ikulu ya Whitehouse mbele ya  Rais Trump.

Ni  seneta mmoja pekee wa chama cha Republican, Susan Collins, ambaye anakabiliwa na  ushindani mkali wa uchaguzi huko Maine, aliyepiga kura dhidi ya mteule huyo wa rais Trump  katika kura hiyo ya jana jioni.

Jaji Barrett ndiye jaji wa tatu aliyeteuliwa na rais  Trump kuhudumu katika mahakama ya juu, baada ya Neil Gorsuch aliyeteuliwa mnamo  2017 na Brett Kavanaugh mnamo 2018.

Categories
Kimataifa

Uhispania yatangaza hali ya hatari kutokana na awamu ya pili ya maambukizi ya Corona

Uhispania imetangaza hali ya hatari ya kitaifa na kuweka kafyu ya usiku katika juhudi za kudhibiti kuzuka upya kwa virusi vya Corona nchini humo.

Waziri Mkuu wa taifa hilo Pedro Sánchez amesema kuwa kafyu hiyo itakuwa kati ya saa tano usiku na saa kumi na mbili asubuhi.

Chini ya mikakati hiyo ya dharura, maafisa wa utawala wanaweza pia kupiga marufuku usafiri baina ya maeneo mbalimbali.

Sánchez alisema kuwa ataliomba bunge kuidhinisha kuongezwa kwa muda wa sheria hizo mpya kutoka siku 15 hadi miezi sita.

Uhispania iliathiriwa vibaya na awamu ya kwanza ya maambukizi ya virusi hivyo mapema mwaka huu na kusitisha shughuli zote.

Kama maeneo mengine Barani Ulaya, hata hivyo, taifa hilo pia limeathiriwa vibaya zaidi ya awamu ya pili ya maambukizi.

Uhispania imepitisha visa milioni moja tangu kuanza kwa janga hilo huku ikiripoti zaidi ya vifo elfu 35.

Categories
Kimataifa

Polisi nchini Nigeria waamriwa kukomesha ghasia nchini humo

Mkuu wa Polisi nchini Nigeria ameamuru kutumiwa rasilimali zote za idara ya polisi kukomesha ghasia na wizi wa ngawira nchini humo.

Mohamed Adamu amesema wahalifu wanatumia nafasi ya maandamano ya kupinga ukatili wa polisi kusababisha ghasia, jambo ambalo halikubaliki.

Maafisa wa polisi wameamriwa kukomesha ghasia, mauaji, uporaji na uharibifu wa mali ya umma.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi yalianza tarehe 7 mwezi Oktoba.

Maandamno hayo ambayo yalijumuisha hasa sana vijana, yalitaka kikosi maalum cha polisi cha kukomesha wizi wa kimabavu SARS  kibanduliwe.

Rais Muhamaddu Buhari aliamuru kubanduliwa kwa kikosi hicho, ambacho kimelaumiwa kwa kusababisha mauaji ya kiholela, mateso na unyang’anyi wa mali.

Hata hivo baada ya siku kadhaa maandamano ya kutaka marekebisho makubwa yafanywe  yangali yanaendelea nchini humo.

Categories
Kimataifa

Addis Ababa yashtumu matamshi ya Washington dhidi ya bwawa tata la Nile

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed  amesema kuwa taifa lake halita-itikia shinikizo zozote hasa baada ya rais wa Marekani  Donald Trump kupendekeza kuwa huenda Misri ikaharibu bwawa tata la Nile.

Bwawa hilo la the Grand Ethiopian Renaissance linazozaniwa na mataifa ya  Ethiopia, Misri na  Sudan.

Trump alisema kuwa Misri huenda isiweze kuishi na bwawa hilo na huenda ikalilipua.

Hata hivyo Ethiopia inaamini kuwa Marekani inaiunga mkono Misri katika mzozo huo.

Marekani ilitangaza mwezi Septemba kuwa itakatiza misaada kwa  Ethiopia baada yake kuanza kujaza eneo moja lililo nyuma ya bwawa hilo mwezi Julai.

Misri inategemea zaidi  mto Nile kwa mahitaji yake mengi ya maji na inahofia kuwa huenda huduma hizi zikakatizwa na uchumi wake kuathirika iwapo  Ethiopia itatwaa udhibiti wa mto huo.

Pindi baada ya kukamilika, bwawa hilo la gharama ya dola bilioni 4 katika eneo la  Blue Nile magharibi mwa Ethiopia litakuwa mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha kawi kutoka kwa maji barani Afrika.

Ujenzi wa bwawa hilo ulianza mwaka 2011 huku kitendawili kikuu kikiwa muda utakaotumiwa kujaza bwawa hilo.

Categories
Kimataifa

Ufaransa yaapa kuimarisha juhudi za kupambana na Corona hadi mwaka ujao

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema taifa hilo litaendelea kupambana na janga la korona hadi katikati ya mwaka ujao.

Tangazo hilo limetolewa huku visa vya maambukizi nchini humo vikipita watu milioni moja.

Siku ya Ijumaa Ufaransa ilirekodi zaidi ya visa 40,000 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 na jumla ya vifo 298.

Mataifa mengine ambayo yamerekodi ongezeko la visa vipya vya ugonjwa huo ni Urusi, Poland, Italia na Uswizi.

Shirika la Afya duniani WHO limesema huu ni wakati muhimu kwa mataifa ya Ulaya kuimarisha mbinu za kuzuia msambao wa ugonjwa huo na kuhakikisha kuwa mitandao ya huduma za afya inakabiliana vilivyo na janga hilo.

Idadi ya wastani ya kila siku ya maambukizi ya ugonjwa huo imeongezeka mara dufu katika muda wa siku kumi zilizopita.

Bara la Ulaya sasa limerekodi visa  milioni 7.8 vya ugonjwa huo na karibu  vifo vya watu 247,000.

Kimataifa, jumla ya visa milioni 42 vya mambukizi ya ugonjwa huo vimerekodiwa na vifo milioni 1.1.

Akiongea katika hospitali moja jijini Paris, Rais Macron amesema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa magonjwa nchini humo, ugonjwa huo huenda ukasalia nchini humo hadi katikati ya mwaka ujao.

Ufaransa imeongeza tena muda wa makataa ya kutotoka nje usiku kwa majuma sita.

Categories
Kimataifa

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aagiza kukomeshwa kwa ghasia nchini humo

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia zinazokumba taifa hilo.

Hata hivyo Rais huyo hakugusia madai ya mauaji ya waandamanaji yaliotekelezwa na maafisa wa polisi ambayo yameshtumiwa na jamii ya kimataifa na kuibua machafuko Jijini Lagos.

Rais Buhari aliwatahadharisha waandamanaji dhidi ya kuvuruga usalama.

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Buhari kuzungumzia kuhusu ghasia hizo ambapo aliwalaumu watu aliosema wameteka maandamano hayo na kuendeleza ajenda zao.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 77 aliwahimiza vijana kukomesha maandamano na kushauriana na serikali ili kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo.

Jiji la Lagos limeshuhudia visa vya milio ya risasi, uporaji mali na kuteketezwa kwa gereza moja tangu maafisa wa usalama walipokabiliana na waandamanaji wanaoshinikiza mabadiliko ya uongozi na kukomeshwa kwa dhuluma za polisi katika jiji hilo lenye wakazi milioni 20.

Marekani, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyoshutumu matumizi ya nguvu kuwatawanya waandamanaji.

Categories
Kimataifa

Waathiriwa wa maandamano nchini Nigeria kutendewa haki

Naibu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo, ameahidi kutendewa haki kwa waandamanaji waliouawa au kujeruhiwa wakati wa maandamano ambayo yamefanyika nchini humo kwa kipindi cha siku chache zilizopita.

Mashahidi walisema kwamba wanaume waliokuwa wamevalia sare za kijeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji Jumanne jioni mjini Lagos.

makamu huyo wa Rais amesema maafisa kadhaa wa polisi pia waliuawa wakati wa makabiliano na waandamanaji hao.

Hakikisho lake limejiri kufuatia shutuma dhidi ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya waandamanaji ambao awali walikuwa wakitaka mabadiliko kutekelezwa kwenye kikosi cha polisi lakini sasa wanataka mabadiliko ya uongozi nchini humo.

Wakati huo huo Muungano wa Afrika umeshutumu vikali mashambulizi dhidi ya waandamanaji wanaolalamikia dhuluma za polisi nchini Nigeria.

Mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki, amezihimiza pande husika kwenye mzozo huo kuheshimu haki za binadamu na sheria.