Categories
Kimataifa

Maafisa watatu wa polisi Ufaransa wasimamishwa kazi kwa kumdhulumu mtu mweusi

Utawala wa Ufaransa umewasimamisha kazi maafisa watatu wa polisi baada ya kuonekana kwenye video wakimpiga mtu mmoja mweusi kati kati mwa Jiji la Paris.

Kisa hicho cha siku ya Jumamosi kimeibua malalamiko mengi nchini Ufaransa kuhusu mienendo ya maafisa wa usalama.

Hayo yanajiri huku serikali ikijaribu kuanzisha sheria itakayoharamisha kuonyeshwa kwa nyuso za maafisa wa polisi kwenye vyombo vya habari.

Wakosoaji wa sheria hiyo wanasema pasipo picha za aina hiyo, hakuna kisa hata kimoja ambacho kingefahamika wazi kati ya vile vilivyotokea juma lililopita.

Mnamo siku ya Alhamisi, mchezaji soka shupavu Kylian Mbappe, ambaye ni mweusi aliungana na wenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa na pia wana riadha katika kulaani kisa hicho cha hivi punde.

Picha za video kuhusu kisa hicho zinaonyesha maafisa watatu wa polisi wakimpiga kwa mateke, makondo na virungu mtu huyo baada ya kuingia kwenye studio yake ya kurekodi nyimbo.

Categories
Kimataifa

Salva Kiir atoa wito wa kudumishwa kwa amani duniani

Viongozi wa dunia wamehimiza amani miongoni mwa mataifa wakati wa mkutano wa tatu wa matumaini ulioandaliwa kupitia mtandao.

Mkutano huo uliofadhiliwa na Shirikisho la Amani Ulimwenguni, UPF, uliandaliwa kwa kumbukumbu ya mwaka wa 70 wa vita vya Korea.

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, ambaye nchi yake imeshuhudia mizozo amefanya juhudi nyingi za kufufua mashauri ya amani.

Alisema viongozi sharti daima waongozwe na matarajio ya watu, ambayo watawashinikiza kuafikia maamuzi magumu wakati wa mashauri ya amani.

Kiir alisema pasipo amani, dunia haiwezi kufaulu kwenye vita dhidi ya umaskini, majanga, athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mikasa ya kimaumbile.

Kwa upande wake Rais wa Liberia Dkt. George Weah alipongeza juhudi za UPF za kuongoza katika ukuzaji amani huku akikariri jinsi taifa lake lilivyokumbwa na vita na migawanyiko.

Muasisi mwenza wa shirikisho la UPF, Dkt. Hak Ja Han Moon, alitangaza kubuniwa kwa chama cha kimataifa cha wasanii wa amani.

Chini ya UPF, chama hicho kipya kinanuia kukuza maadili ya kutoa shukrani, amani na utulivu na kuanzia kwa kuwalea watoto wa kidini ambao wanaishi kwa uzingativu wa maslahi ya wengine.

Categories
Kimataifa

Nitatoka White House baadaye, Trump alegeza msimamo

Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kuondoka kwenye Ikulu ya White House iwapo Joe Biden atathibitishwa kirasmi na jopo la waamuzi kuwa Rais mpya.

Kufikia sasa Rais huyo hajakubali kushindwa kwenye uchaguzi wa Urais wa tarehe 3 mwezi huu.

Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba itakuwa vigumu kukubali matokeo ya uchaguzi huo yanayoashiria kwamba alishindwa na mpinzani wake Biden wa chama cha Democratic.

Kwa mara nyingine, amekariri madai ambayo hayajathibitishwa kuwa kulikuwa na udanganyifu wa kura kwenye uchaguzi huo.

Biden alimshinda Trump kwa kura 306 dhidi ya 232 chini ya mfumo wa jopo la waamuzi ambao hutumiwa kumchagua Rais wa Marekani.

Kura hizo zilizidi 270 ambazo mwaniaji anahitaji ili kutangazwa mshindi wa Urais kwa mujibu wa mfumo wa uchaguzi nchini humo.

Aidha, Biden alimshinda Trump kwa zaidi ya kura million sita za kawaida.

Jopo hilo la waamuzi litakutana mwezi ujao kuidhinisha rasmi matokeo hayo, huku Joe Biden akipangiwa kuapishwa tarehe 20 Januari.

Rais Trump na wafausi wake wamewasilisha kesi kadhaa mahakamani kuhusiana na uchaguzi huo, lakini nyingi kati yazo zimetupiliwa mbali.

Mapema wiki hii, Trump alikubali hatimaye kuruhusu shughuli za kuwaapisha maafisa wapya wa baraza la Biden baada ya sintofahamu iliyodumu kwa wiki kadhaa.

Categories
Kimataifa

Watu 337 wahukumiwa vifungo vya maisha gerezani nchini Uturuki

Mahakama moja nchini uturuki imewahukumu vifungo vya maisha gerezani maafisa 337 wa kijeshi pamoja na watu wengine katika mojawapo wa kesi kubwa zaidi zinazohusiana na jaribio la mapinduzi ya serikali mwaka 2016.

Marubani wa ndege za vikosi vya angani na makamanda wa kijeshi ni miongoni mwa takriban washtakiwa 500 walioshtakiwa kwa kujaribu kupindua serikali ya rais  Recep Tayyip Erdogan.

Yadaiwa kwamba waliongoza njama hiyo kutoka kwenye kituo cha jeshi la angani cha  Akinci viungani mwa jiji kuu Ankara.

Erdogan alisema kuwa mhubiri mmoja wa kiislamu aliye nchini marekani kwa jina Fethullah Gulen alipanga njama hiyo iliyowafanya watu wengi kukamatwa.

Gulen amekanusha kuhusika kwenye jaribio hilo la kupindua serikali lililotekelezwa mwezi Julai mwaka 2016 lililosababisha vifo vya watu 251 huku wengine zaidi ya elfu-2 wakijeruhiwa.

Kesi hiyo ilianza mwezi Agosti mwaka 2017 ambapo mashtaka ni pamoja na kutaka kumuua rais Erdogan na kuteka taasisi kuu za kiserikali.

Categories
Kimataifa

Joe Biden ahimiza utulivu msimu wa baridi unapoghubika Marekani

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kudumishwa kwa amani  nchini humo hasa wakati huu wa msimu wa baridi unaondamana na msambao wa  virusi vya  Corona.

Kwenye hotuba ya kuadhimisha likizo ya kutoa shukrani,Biden alisema  sasa ni wakati wa kupambana na virusi vya Corona na siyo kugawanyika.

Aliwahimiza raia wa nchi hiyo kuzingatia maagizo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Hayo yanajiri huku Rais Donald Trump akiwahimiza wafuasi wake kufanya kila juhudi kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais nchini humo.

Akiongea kwa njia ya simu kutoka ikulu ya White House wakati wa hafla ya wabunge wa chama cha Republican huko  Pennsylvania, Trump alirejelea madai yake kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari tele.

Trump alikuwa ametarajiwa kuhudhuria hafla hiyo lakini akaahirisha safari hiyo baada ya wandani wawili wa wakili wake Rudy Giuliani kuambukizwa virusi vya Corona, lakini Giuliani alihudhuria hafla hiyo.

Juhudi za Rais Trump za kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo zimegonga mwamba katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo.

Categories
Kimataifa

Ufaransa kulegeza masharti ya COVID-19 msimu wa Krismasi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake itaanza kulegeza masharti yaliyowekwa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona, kwa kuruhusu baadhi ya maduka kuendelea na biashara zao, kuanzia mwishoni mwa juma hili.

Macron ametangaza kuwa watu wataruhusiwa pia kutangamana na familia zao msimu ujao wa sherehe za Krismasi.

Hata hivyo, rais huyo amesema baa na migahawa zitaendelea kufungwa hadi tarehe 20 Januari mwaka ujao.

Ufaransa imeripoti zaidi ya visa milioni 2.2 vya watu walioambukizwa Corona na vifo vya zaidi ya watu elfu 50 tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa wa COVID-19 nchini humo.

Kupitia hotuba ya televisheni, Macron amesema nchi yake imepita kilele cha wimbi la pili la maambukizi ya Corona.

Amesema kwamba masharti mengi yaliyotangazwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo yatalegezwa kaunzia tarehe 15 Desemba kwa ajili ya sherehe za Krismasi, ambapo kumbi za sinema zitafunguliwa na masharti yaliyowekewa shughuli za usafiri kuondolewa iwapo kiwango cha maambukizi mapya kitakuwa chini ya visa 5,000 kwa siku.

Mnamo siku ya Jumatatu, Ufaransa ilitangaza visa vya watu 4,452 walioambukizwa ugonjwa wa COVID-19 katika muda wa masaa 24, hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi nchini humo tangu tarehe 28 Septemba.

Kiwango cha wastani cha maambukizi ya Corona kwa siku kilikuwa visa 21,918 ambapo kilele chake kilikuwa visa 54,440 mnamo tarehe 7 mwezi huu.

Categories
Kimataifa

Biden amteua John Kerry kuwa mjumbe maalum kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa

John Kerry ambaye wakati mmoja alikuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani,atahudumu kama mjumbe maalum wa Marekani kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa wakati rais mteule Joe Biden atakapoapishwa rasmi kuwa rais.

Kerry ni miongoni mwa maafisa kadhaa walioteuliwa siku ya Jumatatu na Biden kuhudumu katika serikali mpya atakayounda.

Miongoni mwa wengine walioteuliwa ni msaidizi wa muda mrefu wa Biden Antony Blinken atakayhudumu kama waziri wa mashauri ya kigeni.

Imearifiwa kuwa huenda  Janet Yellen akateuliwa  kuwa waziri wa fedha.

Haya yanajiri huku miito ikiendelea kutolewa ya kumtaka Donald Trump kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa urais.

Licha ya shinikizo hizo, Trump angali anasisitiza kuwa kulifanyika udanganyifu kwenye uchaguzi huo na maafisa wake wangali wanawasilisha kesi  mahakani kupinga matokeo hayo.

Hata hivyo Biden anatarajiwa kutangazwa kumshinda Trump kwa kura 306  ikilinganishwa na kura 232 za Trump wakati kundi la waakilishi wa majimbo litakapokutana kumthibitisha mshindi wa uchaguzi huo tarehe 14 mwezi Disemba.

Kura hizo za Biden zikijumlishwa ni zaidi ya kura 270 kutoka majimbo muhimu zinazohitajika kwa mgombea kutangazwa kuwa  mshindi.

Biden amesema kwamba anahitaji kundi lake la maafisa kuwa tayari kumsaidia na kuliwezesha  taifa hilo kukabiliana na changamoto  zinazolikabili na kuimarisha usalama,maadili na ustawi wa taifa hilo.

Categories
Kimataifa

China kusaidia mataifa yanayostawi kupata chanjo ya Covid-19

Rais Xi Jinping wa China amehakikishia kuhusu kujitolewa kwa nchi yake kuzisaidia nchi zinazostawi kote duniani kupokea chanjo ya ugonjwa wa COVID-19.

Akihutubia mkutano wa mwaka huu wa mataifa yenye ustawi mkubwa wa viwanda ulioandaliwa na Saudi Arabia, rais Xi alisema mataifa maskini yanahitaji usaidizi kuhimili athari za kiuchumi ambazo zimesababishwa na  janga hilo.

Alikariri kujitolea kwa China kuzisaidia nchi zinazostawi kwa kuwezesha chanjo za ugonjwa wa COVID-19 kupatikana kwa gharama nafuu kote duniani.

Rais Xi alisema kwamba China imetekeleza kikamilifu mpango wa kuahirisha ulipaji madeni ulioratibiwa na mataifa yenye ustawi mkubwa wa viwanda huku ikikabiliana na changamoto zake.

Alisema China itaongeza kiwango cha kuahirisha madeni na utoaji misaada kwa nchi zenye shida Fulani na kuhimiza tyaasisi zake za kifedha kutoa ufadhili mpya wa kifedha kwa hiari kulingana na kanuni za sekta hiyo.

Categories
Kimataifa

Chanjo ya Oxford dhidi ya COVID-19 yaonyesha kukinga kwa asilimia 70

Chanjo iliyotayarishwa na chuo kikuu cha Oxford inazuia watu asilimia 70 kupatwa na dalili za ugonjwa wa Covid-19, kwa mujibu wa majaribio ya hivi punde yaliyohusisha watu wengi.

Matokeo hayo yamelinganishwa na chanjo za Pfizer na Moderna ambazo hivi majuzi zilionyesha kuwa bora kwa asilimia  95 na 94.5 mtawalia.

Hata hivyo, chanjo hiyo ya Oxford ina gharama nafuu na ni rahisi kuhifadhi na kuisambaza katika maeneo mbali mbali duniani kuliko chanjo hizo zingine mbili.

Serikali ya Uingereza imeagiza vipimo milioni 100 vya chanjo hiyo ya Oxford, ili kuwachanja watu milioni 50.

Zaidi ya watu elfu 20 wa kujitolea walifanyiwa majaribio yake, ambapo nusu walitoka Uingereza na wengine Brazil.

Watafiti wanasema kwamba chanjo hiyo inatoa kinga ya asilimia 70.

Wanaotoa huduma za kuwatunza wagonjwa nyumbani pamoja na wafanyikazi wengine watakuwa wa kwanza kupewa chanjo hiyo wakifuatiwa na wahudumu wa afya.

Chanjo hiyo kwa jina AZD1222, ilizinduliwa na Chuo Kikuu cha Oxford kwa usaidizi wa kampuni ya dawa ya AstraZeneca.

Categories
Kimataifa

Trump ahimizwa na rafikiye akubali kushindwa

Rafiki wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump amemhimiza rais huyo aachane na harakati za kupinga ushindi wa rais mteule Joe Biden.

Chris Christie, aliyewahi kuwa Gavana wa jimbo la New Jersey amelitaka kundi la kampeini la Trump kusitisha kile alichokitaja kuwa fedheha ya kitaifa.

Rais Trump amekataa kukubali kwamba alishindwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika hivi majuzi nchini Marekani kwa madai ambayo hayajathibitishwa kwamba kulikuwa na visa vya udanganyifu.

Wafuasi wengi wa chama cha Republican wameunga mkono juhudi hizo za Trump za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Siku ya Jumamosi, juhudi za Trump zilipata pigo wakati Jaji katika jimbo la Pennysylvania  alipotupilia mbali kesi iliowasilishwa na Trump ya kutaka kubatilisha maelfu ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta katika jimbo hilo.