Categories
Habari

Wahudumu wa Afya ya Jamii Murang’a wapokea mafunzo ya uhamasisho kuhusu COVID-19

Wahudumu wa afya ya jamii wa kujitolea katika Kaunti ya Murang’a wamepokea mafunzo ambayo yatawasaidia katika vita dhidi ya kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 katika viwango vya mashinani.

Haja ya kuwapa mafunzo wahudumu hao wa kujitolea wa afya iliafikiwa baada ya kubainika kuwa watu wengi vijijini walikuwa wakikiuka masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19.

Afisa wa afya ya umma katika eneo la Murang’a Kusini Bedan Kamau, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wahudumu hao ni wafanyikazi wa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wanakijiji kuhusu hatari za virusi vya korona na njia bora za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Akiongea baada ya kufunga warsha ya siku tatu ya mafunzo kwa wahudumu hao kutoka eneo la  Murang’a  mjini  Kenol, Kamau alisema kuwa wahudumu hao wa kujitolea wanafahamika vyema katika maeneo ya mashinani na wanaweza kufika vijijini kwa urahisi na kuwaelimisha wanakijiji nyumbani.

Kamau alisema kuwa wahudumu hao pia wanaweza kushughulikia maswala kama yale ya kupanga uzazi, afya ya uzazi ya vijana na maswala kuwahusu akina mama wajawazito na kuwatunza watoto wanaozaliwa.

Categories
Habari

Polisi wasaka genge la wahalifu walioteka gari la mkazi wa Ruaka

Maafisa wa Upelelezi katika Kaunti ya Kiambu wanasaka wanachama wa genge moja hatari la wahalifu ambalo liliteka gari aina ya Toyota Premio la mkazi mmoja wa eneo la Ruaka mnamo Ijumaa alipokuwa akielekea nyumbani kwake.

Kulingana na taarifa ya Idara ya Upelelezi kuhusu Uhalifu, mwathiriwa alikuwa amefika kwenye lango la kuingia anakoishi katika makazi ya Ruaka One River, bila kujua kwamba genge la wahalifu watatu lilikuwa likimngojea.

Lango lipofunguliwa, dirisha la gari hilo la upande wa dereva lilibomolewa ghafla kwa chuma, kabla ya risasi mbili kupigwa hewani kutoka kwa bastola kwa jaribio la kumtisha.

Hata hivyo, alifanikiwa kuingia kwa nguvu kwenye eneo la maegesho, lakini kabla ya kuruka nje ya gari na kutorokea usalama, watatu hao walimshika na kumshambulia kisha wakanyakua funguo za gari na simu.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, maafisa wa upelelezi walioko Kiambaa walianzisha msako wa kuwatafuta washukiwa.

Gari hilo lilipatikana limetelekezwa katika kijiji cha Kagongo, baada ya kuharibiwa.

Maafisa wa upelelezi wanaamini kuwa washukiwa hao watatu ni sehemu ya kundi kubwa la wahalifu linaloendesha shughuli za wizi katika kaunti ya Kiambu.

Wamekuwa wakilenga madereva wa teksi huku wakijifanya kama wateja na baadaye kuwageukia katika sehemu zisizo na watu na baadaye kuharibu magari yao.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi wamewataka wananchi kuwa makini kutokana na mwenendo huo wa uhalifu.

Categories
Habari

Mfanyibiashara wa Nyeri aliyetuhumiwa kwa mauaji ya mwanawe ameaga dunia

Mfanyibiashara mashuhuri wa Nyeri ambaye ameshutumiwa kwa kuwakodisha watu kumuua mwanawe wa kiume mwaka jana kuhusiana na mzozo wa kifamilia amefariki.

Stephen Wang’ondu mwenye umri wa miaka 74 ambaye alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji kuhusiana na mauaji ya mwanawe Daniel Mwangi mwenye umri wa miaka 32, akiwa pamoja na watu wengine wanne, aliaga dunia Ijumaa katika hospitali ya Outspan mjini Nyeri.

Mfanyibiashara huyo ambaye amekuwa akizuiliwa korokoroni tangu mwezi Januari mwaka huu, alishutumiwa kwa kupanga mauaji ya mwanawe usiku wa tarehe 31 mwezi Disemba mwaka uliopita katika kijiji cha Mwiyogo katika eneo la Kieni mashariki kaunti ya Nyeri.

Alishtakiwa pamoja na James Mahinda, Eddy Kariuki, Raphael Wachira na Geoffrey Warutumo ambao anadaiwa kukodisha kwa kuwalipa shilingi elfu 160 ili kumuua mwanawe.

Upande wa mashtaka ulikuwa umeiambia mahakama kuwa ulikuwa umekusanya ushahidi muhimu dhidi ya mfanyibiashara huyo ambaye wanadai kuwa alipanga na kutekeleza mauaji ya mwanawe kuhusiana na shilingi milioni 2.5 walizopaswa kulipwa na kampuni moja ya bima miongoni mwa maswala mengine.

Familia yake akiwemo mkewe, mabinti zake watatu na mke wa marehemu ambaye walikuwa wamezozana Scholastica Wachuka walikuwa wamejumuishwa katika kesi hiyo.

Kesi hiyo ilitarajiwa kutajwa tarehe kumi mwezi huu.

Categories
Habari

Waislamu wahimizwa kuzingatia kanuni za kudhibiti covid-19 wakati wa sherehe za Idd-ul-fitr

Kamati ya kitaifa ya waislamu ya kushughulikia janga la Covid-19, imewashauri waislamu nchini kuzingatia kwa makini masharti yaliyowekwa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19 wakati wa sherehe za Idd- ul-fitr juma lijalo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof Mohamed Karama, alitoa wito kwa waislamu nchini kuzingatia masharti hayo wakati wa sherehe hizo ili kujikinga kutokana na maambukizi ya virusi hivyo hatari.

Prof Karama aliongeza kuwa waislamu na wakenya wote kwa jumla wanapaswa kuwa makini na kujikinga kila wakati huku akiongeza kuwa aina ya virusi vya corona vilivyogunduliwa nchini India vinapaswa kumpa kila mmoja nchini wasiwasi.

Alitoa wito kwa misikiti yote ambayo inapanga kufanya sala za Idd, kuhakikisha kuwa masharti yote ya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 yanazingatiwa.

Alipendekeza kuwa maombi yafanywe mahala palipo wazi huku umati ukidhibitiwa ipasavyo.

Aidha aliwahimiza waislamu kuchanjwa dhidi ya ugonjwa wa Covid19 huku akiongeza kuwa hali hii itasaidia kupunguza athari za maambukizi.

Waislamu kote ulimwenguni watasherehekea siku kuu ya Idd-ul-fitr juma lijalo tarehe 13 au 14 mwezi huu baada ya mwezi kuandama na kukamilika kwa siku 30 za kufunga.

Serikali kupitia arifa nambari 4205 kwenye gazeti rasmi la serikali imetangaza Ijumaa tarehe 14 mwezi huu, kuwa siku kuu ya kuadhimisha sherehe za Idd-ul-fitr.

Categories
Habari

Kenya yanakili visa 572 vipya vya Covid-19

Kenya imenakili visa 572 zaidi vya maambukizi katia muda wa saa 24 zilizopita baada ya sampili 4,624 kupimwa.

Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo humu nchini sasa kimefikikia asilimia 12.4.

Kutokana na visa vya hivi punde jumla ya idadi ya visa vya maambukizi ambavyo vimethibitishwa humu nchini sasa ni 163,238.

Katika visa hivyo vipya vya maambukizi ,526 ni wakenya ilhali 46 ni raia wa kigeni. 218 ni wanawake na 354 wanaume.

Mwathiriwa wa umri mdogo zaidi ni motto wa umri wa miezi minane na wa umri wa juu zaidi ni mkongwe wa miaka 97.

Nairobi ingali inaongoza kwa visa 148 ikifuatiwa na Kisumu kwa visa 46 na Kericho kwa visa 36.

Wagonjwa 18 hata hivyo wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kuongeza idadi ya wagonjwa walioaga dunia kufikia 2,883.

Wagonjwa 476 wamepona, 219 kutoka utunzi wa nyumbani na 257 kutoka hospitali mbali mbali kote nchini.

Jumla ya wagonjwa 111,129 wamepona kufikia sasa.

Kwa wakati huu wagonjwa 1,103 wamelazwa katika hiospitali mbali mbali nchini huku 6,295 wakiwa chini ya utunzi wa nyumbani.

Wagonjwa 131 wamelazwa katika wodi za wagonjwa mahututi huku 26 wakiwekewa mitambo ya kuwasaidia kupumua na 80 kuwekewa hewa ya Oxygen.

Kufikia sasa wakenya 915,968 wamepokea chanjo ya COVI 19.

Categories
Habari

Gavana wa Laikipia Nderitu Muriithi alalamikia ongezeko la stakabadhi bandia za ardhi

Gavana wa kaunti ya Laikipia Ndiritu Muriithi ametoa tahadhari kuhusu ongezeko la stakabadhi bandia za mipango ya ustawi wa vipande vya ardhi katika kaunti hiyo.

Akiongea alipozuru afisi za kuhifadhi maelezo kuhusu ardhi mjini Nanyuki ambazo zilizinduliwa hivi majuzi na idara ya muundo msingi, nyumba na ustawi wa miji, Muriithi alitoa wito kwa wakazi kutumia afisi hizo kubaini hali ya vipande vyao vya ardhi kabla ya kutekeleza shughuli zozote za ustawi.

Alisema visa vya wizi wa ardhi katika kaunti hiyo vimekithiri na kwamba idara ya upelelezi wa jinai DCI inafanya uchunguzi kuhusu baadhi ya visa hivyo ili kuwakamata wahusika.

Alisema maafisa wa DCI wanachunguza kundi moja la watu wanaojifanya kuwa wanatekeleza shughuli zao kwa niaba ya waziri wa ardhi na ambao wanahusika katika kughushi stakabadhi za mipango ya ustawi wa ardhi na kutayarisha stakabadhi ghushi za ardhi ya umma.

Kwa mujibu wa gavana huyo, walaghai hao wanalenga mashamba ya serikali pamoja na ardhi ya shirika la reli nchini.

Categories
Habari

Rais Kenyatta amwomboleza spika wa zamani wa kaunti ya Nairobi Alex Magelo

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambi rambi kwa familia, ndugu na marafiki wa aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Alex Ole Magelo aliyeaga dunia usiku wa kuamkia jumamosi katika hospitali moja jijini Nairobi.

Kwenye risala yake, Rais Kenyatta alimtaja marehemu Ole Magelo kuwa kiongozi wa kweli aliyejikakamua kuboresha Kenya kwa manufaa ya wote.

Rais alisema kujitolea kwa marehemu Ole Magelo kuhudumia Wakenya kulimwezesha kuteuliwa mwaka uliopita kuwa mwanachama wa baraza la ustawi wa sekta ya ngozi hapa nchini.

Rais ameomba Maulana kuipa nguvu familia ya marehemu wakati huu wa majonzi.

Spika huyo wa zamani wa bunge la kaunti ya Nairobi Alex Magelo aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi. Kulingana na mkewe Lucy Muthoni, Magelo alikuwa amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii, seneta wa kaunti ya Narok Ledama Ole Kina alimtaja Magelo kama rafiki wa kweli na mwana mzalendo katika jamii ya Maa.

Mwaka uliopita, Magelo alijiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kumrithi aliyekuwa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi na kumuunga mkono spika wa sasa Benson Mutura. 

Categories
Habari

Tume ya kuwaajiri walimu TSC yawapandisha vyeo walimu 16,000

Tume ya kuajiri walimu humu nchini, TSC imewapandisha vyeo walimu 16,000 waliosailiwa kati ya mwezi Disemba mwaka jana na mwezi Februari mwaka huu.

Kwa mujibu wa afisa mkuu mtendaji wa tume ya TSC, Nancy Macharia shughuli hiyo ya usaili ni sehemu ya mkataba wa makubaliano kati ya serikali na walimu wa mwaka 2017-2021.

Waliopandishwa vyeo ni pamoja na wale watakaohudumu kama manaibu walimu wakuu (T- scale 13-D3), (T-scale 12-D2) wahadhiri wakuu (T-scale 12-D2), (T-Scale 11-D1) na maafisa wa utekelezaji mtaala (T-Scale 10-C5).

Wengine ni walimu wakuu (T-Scale 10-C5), walimu wa shule za upili, wale wanaohudumu chini ya mpango wa utoaji ushauri kuhusu taaluma na wale wanaohudumu katika maeneo kame.

Macharia aliwatahadharisha walimu dhidi ya kuhadaiwa na walaghai wanaodai wanaweza kushawishi matokeo ya usaili.

Mwaka uliopita, chama cha walimu cha KNUT kilipinga mpango wa kuwapandisha vyeo walimu 15,000 mnamo mwezi Januari mwaka huu.

Categories
Habari

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya afisa wa tume ya ardhi Jennifer Itumbi amekamatwa

Mshukiwa wa mauaji ya aliyekuwa kaimu  mkurugenzi wa tume ya kitaifa kuhusu ardhi Jennifer Itumbi ametambuliwa na kutiwa nguvuni na polisi.

Kulingana na idara ya upelelezi-DCI, Peter Mwangi Njenga ambaye kwa jina lingine anafahamika kama Ole Sankale ametambuliwa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo, miongoni mwa wengine ambao hawajakamatwa.

Mshukiwa huyo alionekana na marehemu mara ya mwisho tarehe 12 mwezi Machi mwaka 2021. Mahala palipopatikana mwili wa marehemu Jennifer panachunguzwa ili kupata vidokezo zaidi.

Kwa mujibu wa polisi mshukiwa huyo mkuu amefungwa mara kadhaa gerezani kwa makosa mbali mbali kwa mujibu wa rekodi za magereza. Mwaka 1996 mshukiwa huyo alishtakiwa kwa wizi na baadaye akashtakiwa mara tatu kwa wizi wa kimabavu na ubakaji.

Eneo hilo ni maarufu sana kwa watu wanaokwenda kwa maombi. kwa mujibu wa polisi, mshukiwa huyo alimvizia Jennifer alipokuwa akisali kabla ya kumbaka na kisha kumuua.

Uchunguzi wa maafisa wa upelelezi ulithibitisha kuwa mshukiwa huyo awali alitekeleza uhalifu kutumia mbinu aliyoitumia kwa Jennifer ambapo huwaibia, kisha anawabaka waathiriwa wake na kuwaua.

“Wapelelezi walipata kesi zingine ambazo ziliripotiwa dhidi ya mshukiwa huyo kutumia mbinu aliyoitumia na katika eneo hilo hilo alikopatikana Jennifer,” idara ya DCI ilisema.

Mwili wa Jennifer Wambua ulipatikana katika msitu wa Ngong mwezi Machi mwaka huu baada yake kuripotiwa kutoweka.

Categories
Habari

Serikali yatangaza Ijumaa tarehe 14 kuwa Siku Kuu kuadhimisha Idd-Ul-Fitr

Serikali imetangaza Ijumaa tarehe 14 kuwa siku kuu kuadhimisha sherehe za Idd-ul Fitr. Hayo yalitangwa na waziri wa usalama wa taifa  Dkt. Fred Matiang’i kupitia kwa arifa katika gazeti rasmi la serikali.

Waumini wa dini ya kiislamu wanakaribia kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa  Ramadhan.

Waumini hao walifanya sala ya mwisho ya mwezi huo mtukufu siku ya Ijumaa tarehe 7 Mwezi Mei katika sehemu mbalimbali nchini kabla ya kuadhimisha sherehe za Idd-ul-Fitr wiki ijayo.

Ili kuwawezesha waislamu kusherehekea mwisho wa mfungo wa  Ramadhan,  serikali imetangaza siku ya ijumaa ijayo kuwa sikuu kuu ya kuadhimisha sherehe za Idd-ul-Fitr.

Siku kuu ya Idd-ul-Fitr huadhimishwa na waislamu kote ulimwengu kuashiria mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa  Ramadhan.

Waumini wa dini ya kiislamu kote ulimwenguni walianza mfungo wa mwezi mtukufu wiki ya tatu ya mwezi Aprili baada ya kuonekana kwa mwezi.

Hata hivyo wamekuwa wakitekeleza mfingo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kuzingatia mashari ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Covid-19.