Categories
Habari

Shule moja yafungwa kaunti ya Kitui kutokana na maambukizi ya Covid-19

Shule nyingine imefungwa katika kaunti ya Kitui baada ya mwalimu mmoja kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19.

Shule ya msingi ya  Waasya iliyoko Mwingi ya kati ilifungwa baada ya mwalimu huyo kugunduliwa kuwa na virusi vya Corona mapema wiki hii.

Haya yamejiri majuma machache baada ya shule ya msingi ya Kithumula Kitui magharibi kufungwa baada ya walimu wawili na mwanafunzi kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Hatua ya kufungwa kwa shule hiyo ilithibitishwa na mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Kitui Salesa Adano.

Adano aliwahakikishia wazazi kwamba wanafunzi wote walipimwa na maafisa wa afya ya umma.

Kwa kujibu wa mkurugenzi huyo, shughuli za masomo zitarejelewa kufikia siku ya Jumatatu baada ya matokeo ya waliopimwa kuthibitishwa.

Mkurugenzi huyo wa elimu alisema mwalimu huyo alikuwa miongoni mwa walimu wengine kumi ambao pia baada ya kupimwa waligunduliwa kuambukizwa virusi hivyo vya Covid-19.

Categories
Habari

Sehemu za ibada zatahadharishwa dhidi ya kukiuka sheria za kudhibiti Covid-19

Baraza la dini mbali mbali kaunti ya Embu limeonya makanisa yanayokiuka kanuni za afya kuhusu ugonjwa wa Covid-19 kwamba yatafungwa.

Hata hivyo, akiongea na wanahabari wakati wa mkutano katika kaunti ya Embu Ijumaa, askofu Paul Kariuki wa dayosisi ya kanisa katoliki ya Embu, aliye pia katibu wa baraza hilo, alisema sehemu nyingi za kuabudu zinazingatia kanuni hizo.

Aidha askofu Kariuki alisema katika maeneo ya kijamii kama vile masoko na vituo vya basi, kuna ulegevu katika uzingatiaji kanuni hizo za afya.  

Kiongozi huyo wa dini alitoa wito kwa raia wahakikishe kwamba wanazingatia maongozi hayo huku taifa hili likikumbwa na msururu wa pili wa ugonjwa wa covid-19.

Askofu Kariuki pia aliwahimiza wakazi kwenda katika vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa wa covid-19.

Alisema baraza hilo linashirikiana na idara ya afya ya kaunti hiyo ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.   

Categories
Habari

Wakenya waonywa dhidi ya vyeti bandia vya COVID-19 huku visa vipya 1,554 vikiripotiwa

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametoa onyo kali kwa Wakenya wanaosafiri nje ya nchi kutumia vyeti bandia vya COVID-19.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya maambukizi humu nchini, Kagwe amesema wizara hiyo imepata habari kuhusu tabia hiyo, akihoji kwamba inaathiri uhusiano kati ya Kenya na mataifa mengine.

Haya yanajiri huku nchi hii ikiripoti idadi ya juu zaidi ya maambukizi baada ya watu 1,554 kupatikana na maradhi ya COVID-19 katika muda wa masaa 24.

Visa hivyo vimetokana na upimaji wa sampuli 9,389 na vimeongeza jumla ya maambukizi humu nchini hadi kufikia 81,656.

Walioambukizwa ni Wakenya 1,526 na raia wa kigeni 28, wa kati ya umri wa miezi mitano hadi miaka 97.

Kijinsia visa 950 ni vya wanaume huku 604 vikiwa vya wanawake.

Kaunti ya Nairobi imeongoza kwa visa vipya 546 ikifuatwa na Mombasa kwa visa 159, Kilifi 153, Kiambu 96, Kericho 68, Meru 45, Kisumu 44, Nakuru 37, Bomet 33, Kakamega 32, Machakos 30, Kajiado 29, Nyandarua 27, Busia 25, Nyeri 25, Kisii 24, Uasin Gishu 22, Siaya 18, Lamu 16, Murang’a 15, Laikipia 14, Kitui 13, Samburu 12, Taita Taveta 11, isiolo 10, Trans Nzoia 9, Bungoma 7, Nandi 6, Makueni 5, Turkana 4, Kwale 4, Vihiga 3, Homa Bay 2, Marsabit 2, Bungoma 1 na Nyamira 1.

Kufikia sasa, wagonjwa 1,200 wako kwenye vituo mbali mbali vya afya humu nchini nao 7,521 wako kwenye mpango wa kuhudumiwa nyumbani.

Wizara ya Afya pia imethibitisha kuwa wagonjwa 599 wamepona, 476 walikuwa wakihudumiwa nyumbani na 123 wakitoka hospitalini. Jumla ya waliopona imefika 54,125.

Taarifa hiyo pia imefichua kwamba wagonjwa 14 zaidi wamefariki kutokana na COVID-19 na kufikisha jumla ya maafa humu nchini hadi 1,441.

Categories
Habari

Maraga ateta kuhusu vipengee vya BBI vinavyohujumu uhuru wa Mahakama

Jaji Mkuu David Maraga amewahimiza Wakenya kukataa vipengee vya ripoti ya BBI vitakavyolemaza uhuru wa Idara ya Mahakama.

Maraga pia amemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kudinda kuwateua majaji 41 waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama nchini, JSC.

Amesema Rais hana mamlaka kisheria ya kutilia shaka au kukataa majina ya majaji yaliyopendekezwa kwake na tume ya JSC, ila kuwateua.

Jaji Mkuu huyo amesema haya kwenye hotuba yake ya mwisho kuhusu hali ya Idara ya Mahakama wakati anapojiandaa kustaafu mnamo Januari 2021 ili kutoa nafasi kwa zoezi la uteuzi wa mrithi wake.

Maraga amesema kuwa Idara ya Mahakama imetimiza mengi wakati wa kuhudumu kwake kama Jaji Mkuu licha ya pingamizi na fedheha kutoka kwa vitengo vengine vya serikali ikiwemo kutoheshimiwa kwa maagizo ya mahakama.

Amesema uhusiano mbaya kati ya Idara ya Mahakama na Mkono wa Utekelezi serikalini umeathiri pakubwa utendakazi wa idara hiyo huku asilimia 47 tu ya maombi ya kifedha yakipitishwa na Wizara ya Fedha.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya idara hiyo, Wakenya wanaripoti takribani kesi 400,000 kila mwaka na sasa kuna mrundiko wa jumla ya kesi 617,582.

Maraga amesema kuwa iwapo hakutaripotiwa kesi nyengine yoyote, kesi hizo zinaweza kuchukua hadi miaka miwili kutatuliwa.

“Mrundiko wa kesi unaongezeka katika ngazi zote za Mahakama. Mahakama ya Rufaa, kwa mfano, inatakikana kuwa na majaji 30 lakini kwa sasa iko na 16 tu, idadi ambayo ni takribani nusu ya ile inayohitajika kisheria,” amesema Maraga.

Categories
Habari

Himizo la kuunga mkono BBI lashamiri Narok huku ukusanyaji saini ukianza rasmi

Kampeni za ukusanyaji saini za mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa BBI zimeanza rasmi katika Kaunti ya Narok.

Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta, ambaye ameongoza zoezi hilo katika eneo bunge lake, amewahimiza wakazi wajitokeze kwa wingi kuunga mkono mchakato huo, akisema kuwa ripoti ya BBI itashughulikia changamoto zinazoikumba jamii ya Maasai.

Mbunge huyo wa chama cha ODM ameahidi kuwa jamii ya Maasai itakuwa msitari wa mbele kuipigia debe ripoti hiyo ambayo amedai itatoa suluhu kuhusu dhuluma za kihistoria za mashamba.

Amekariri kwamba ripoti hiyo ya BBI itakuwa ya msaada kwa uongozi wa hata vizazi vijavyo na itazuia malumbano kama yale yaliyoshuhudiwa katika Msitu wa Mau ambapo watu walivamia rasilimali hiyo muhimu kwa taifa.

Mwakilishi Wadi Mteule Christine Lemein pia ameiunga mkono stakabadhi hiyo na kuahidi kufanya jitihada za kuhakikisha kwamba BBI inapitishwa katika Bunge la Kaunti ya Narok.

Akizungumza kwenye hafla hiyo pia, Mzee wa Maasai Keelena Ole Nchoe amesema kaunti hiyo ina rasilimali nyingi zikiwemo Msitu wa Mau na Mbuga ya Maasai Mara, maswalaambayo yameangaziwa kwenye ripoti hiyo.

Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga waliongoza hafla ya uzinduzi wa zoezi la ukusanyaji saini katika Ukumbi wa KICC.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta alisisitiza kwamba BBI inalenga kuimarisha zaidi katiba ya Kenya ya mwaka wa 2010 kwa kurekebisha vipengee kadhaa.

Ili mapendekezo ya marekebisho ya katiba hiyo yafikie hatua ya maandalizi ya kura ya maamuzi, sharti wapendekezi wakusanye angalau saini milioni moja ambazo zitathibitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kabla ripoti hiyo kujadiliwa Bungeni.

Categories
Habari

Hofu yatanda baada ya abiria kufariki kwenye basi lililokuwa likielekea Mombasa

Wasi wasi umezuka miongoni mwa abiria waliokuwa wakielekea Mombasa baada ya mmoja wao kuaga dunia ndani ya basi walimokuwa wakisafiria.

Abiria huyo alikuwa safarini akiandamana na dada yake pamoja na abiria wengine 30, ambapo alipatikana ameaga dunia kwenye Barabara Kuu ya Mombasa kuelekea Nairobi.

Dereva wa basi hilo la kampuni ya Simba Coach lililokuwa limetoka Busia alikuwa ameliegesha Mjini Malili muda mchache kabla ya saa nne usiku wa Alhamisi kwa kuwa hangeweza kuendelea na safari kutokana na kafyu ya usiku.

Abiria walilazimika kulala kwenye viti vya gari hilo wakisubiri alfajiri ili kuendelea na safari ambapo waligundua abiria huyo alikuwa amefariki.

Kamishna wa Kaunti ya Makueni Maalim Mohammed alithibitisha kisa hicho huku akiongeza kuwa maafisa wa polisi walikuwa wamefunga sehemu hiyo kufuatia tukio hilo.

Inadaiwa kwamba abiria huyo, ambaye ni mwanaume mwenye umri wa makamo, alikuwa amelalamika kuhisi dalili za homa.

Kisa hicho kilisababisha taharuki kwa abiria wengine kabla maafisa wa afya kufika na kuwapa ushauri, kupulizia kemikali basi hilo na hatimaye kuuondoa mwili wa mwendazake.

“Tutawaruhusu waendelee na safari yao,” akasema Kamishna Maalim.

Hiki ni kisa cha pili ndani ya wiki moja cha mtu kuaga dunia ghafla akiwa kwenye gari baada ya kisa sawa na hicho kutokea huko Cabanas katika Kaunti ya Nairobi siku ya Jumanne.

Categories
Habari

Mahakama ‘yaidhinisha’ mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Matungu Justus Murunga

Familia ya aliyekuwa Mbunge wa Matungu Justus Murunga sasa inaweza kuanza utaratibu wa mazishi baada ya Mahakama kuondoa agizo la kusimamisha mazishi hayo.

mwili wa Murunga sasa utafanyiwa maziko tarehe 5 mwezi ujao. Awali, Mahakama ilitoa agizo la kusimamisha maandalizi ya mazishi ya Murunga hadi kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na mwanamke anayedai kuwa mpenzi wa mwendazake.

Wajane wawili wa Murunga, kupitia kwa wakili wao Patrick Lutta, pia walielekea Mahakamani kutaka agizo hilo liondolewe.

Christabel Murunga na Grace Murunga walihoji kuwa kusimamishwa kwa mazishi ya mume wao kunaendelea kuisababishia familia hiyo masaibu zaidi.

Agnes Wangui aliwasilisha kesi Mahakamani akidai kuwa Murunga ndiye baba wa watoto wake wawili na kuomba uchunguzi wa DNA ili kuhakikisha madai yake, ombi ambalo lilikubaliwa.

Hatua hiyo ilisababisha kuahirishwa kwa hafla ya mazishi ya mbunge huyo yaliyokuwa yafanyike tarehe 28 mwezi huu, huku Wangui akihoji kuwa amekuwa kwenye mahusiano na Murunga kwa miezi saba hadi kupata watoto wawili pamoja naye; mvulana na msichana.

Mwanamke huyo pia alifichua madai kwamba wawili hao walikuwa na mipango ya kuoana kulingana na tamaduni za Agikuyu kabla mbunge huyo kufariki ghafla.

Wangui anadai kwamba alikuwa amenunuliwa shamba katika eneo la Karen na mbunge huyo ambaye pia alikuwa anapanga kumjengea nyumba.

Categories
Habari

Mahakama yamkataza Itumbi kumshtaki Matiang’i

Jaribio la aliyekuwa mkuu wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu ya Rais Dennis Itumbi la kutaka kumshtaki Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt. Fred Matiang’i limegonga mwamba.

Hii ni baada ya Mahakama kutupilia mbali ombi la mwana-blogu huyo aliyenuia kumshitaki Waziri Matiang’i kuhusiana na utata wa ardhi ya Ruaraka.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu Douglas Ogoti amesema ombi la Itumbi halijatimiza kikamilifu matakwa ya kikatiba.

Kwa mujibu wa Ogoti, ushahidi iliowasilishwa kutetea ombi hilo haukuafikia kiwango kinachokubalika jinsi ilivyoelezwa kwenye sheria inayohusu ushahidi.

“Ombi la Itumbi limekosa kuafikia uzito wa kisheria ambao ungeipa mahakama mamlaka ya kumpa idhini ya kuanzisha kesi ya kibinafsi dhidi ya Waziri [Matiang’i]. Hakueleza jinsi alivyopata taarifa hizo na stakabadhi kwenye hati yake ya kiapo,” amesema Ogoti.

Itumbi aliwasilisha ombi katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi, akimtaja Matiang’i kwenye kesi anayodai kuwa Wakenya walipa ushuru walipoteza shilingi bilioni 1.5.

Anadai kwamba wakati Dkt. Matiang’i alipokuwa Waziri wa Elimu, alianzisha mchakato wa kuchukua sehemu ya shamba la Ruaraka kwa manufaa ya taasisi mbili za kiserikali; Shule ya Msingi ya Drive-In na Shule ya Sekondari ya Ruaraka.

Itumbi anamushtumu Matiang’i kwa kutozingatia ushauri wa ripoti ya upelelezi ambayo ilisema kuwa ardhi ambapo shule hizo mbili zilijengwa ni ya umma, kwa hivyo kampuni za Afrison Export-Import Limited na Huelands Limited hazikustahili kufidiwa.

Kwenye ombi lake, Itumbi pia alimtaja Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuwa anastahili kujibu kesi kwa kukosa kumfungulia mashtaka Matiang’i.

Mwaka wa 2018, Wizara ya Elimu kupitia kwa Tume ya Ardhi nchini, ilimlipa fidia ya shilingi bilioni 1.5 mwanabiashara Francis Mburu kwa ajili ya ardhi ya ekari 13.5 ambapo shule hizo mbili zilijengwa, iliyoamuliwa na mahakama kuwa ardhi ya umma.

Hata hivyo, Itumbi ameapa kuelekea kwenye Mahakama Kuu ili kushinikiza kuidhinishwa kwa ombi lake.

Categories
Habari

Washukiwa wawili kushtakiwa kwa wizi wa vifaa vya kompyuta katika Wizara ya Ardhi

Watu wawili waliopewa kazi ya kugeuza takwimu za Tume ya Ardhi nchini kuwa za kidijitali wanazuiliwa na polisi kwa madai ya wizi wa vifaa muhimu vya kompyuta.

Humphrey Wairori Wanyonyi na Pius Mutune Wambua wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka Jumatatu baada ya upande wa mshtaka kupata idhini ya kuwazuilia kwa siku tatu zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Maafisa kutoka Kitengo cha Huduma Maalum, SSU, waliwakamata wawili hao Alhamisi na kufanikiwa kupata tarakilishi na vifaa vyengine muhimu vinavyosemekana kuibiwa kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi Jijini Nairobi.

Vifaa hivyo vilivyokuwa vimefichwa kwenye nyumba ya Wanyonyi viliwiana na taarifa ya kisa cha wizi iliyoandikishwa tarehe 24 Novemba katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.

Kukamatwa kwa washukiwa hao kunajiri wakati ambapo kuna ongezeko la visa vya ulaghai kuhusu maswala ya ardhi huku serikali ikinuia kutumia mfumo wa kidijitali katika uhifadhi wa takwimu muhimu kuhusu ardhi ili kupunguza ulaghai huo.

Mfumo huo wa kidijitali unalenga kuleta uwazi katika uhifadhi wa takwimu na kurahisisha upatikanaji wa habari muhimu za maswala ya ardhi ili kukabiliana na ufisadi uliokithiri katika Wizara hiyo.

Aidha, serikali imeanzisha mpango wa kutoa hati miliki za ardhi katika juhudi za kukabiliana na visa vya watu kushirikiana na maafisa wa maswala ya ardhi na kupata hati hizo kwa njia isiyo halali.

Categories
Habari

Wabunge wahitilafiana kuhusu pendekezo la BBI la kubuni Maeneo-Bunge 70 zaidi

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Kitaifa wameibua wasi wasi kuhusiana na mfumo mpya unaopendekezwa wa kugawanya maeneo-bunge mapya yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya BBI.

Wabunge hao hasa kutoka kaunti zilizo nje ya Nairobi, wakiongozwa na Mbunge wa Mwingi Magharibi Charles Nguna, wanapinga pendekezo la kuongeza maeneo bunge 12 mapya katika kaunti ya Nairobi wakisema ipo haja ya kuendeleza maeneo yote ya kijiografia.

Amesema ataendesha kampeini ya kupinga mpango wa BBI iwapo mfumo huo wa kugawanya maeneo mapya ya ubunge hautachunguzwa upya.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya amesema kuwa kubuniwa kwa maeneo mane mpya katika Kaunti ya Kilifi hakutasuluhisha changamoto ya uwakilishi akisema kuwa kulingana na takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Kaunti ya Kilifi inahitaji maeneo bunge sita mapya.

Amesema kuwa mpango huo wa BBI pia haujashughulikia jinsi ya kugawanya pesa za Hazina ya Usawazishaji Maendeleo.

Hata hivyo Mbunge wa Funyula Oundo Ojiambo ameunga mkono kubuniwa kwa maeneo bunge 70 mapya akisema ni bora kuliko kuunganisha maeneo bunge madogo.

Mbunge wa Endebbes Robert Pukose amekosoa pendekezo la kuongeza idadi ya wabunge bila kuelezea jinsi usawa wa kijinsia utakavyoafikiwa katika Bunge la Kitaifa.