Categories
Burudani

Jose Chameleon akosa umeya wa Kampala

Uchaguzi wa Umeya nchini Uganda uliandaliwa jana tarehe 20 mwezi Januari mwaka huu wa 2021 na wala sio tarehe 14 wiki jana kama ilivyodhaniwa na wengi.

Mwanamuziki Jose Chameleone au ukipenda Joseph Mayanja alikuwa mmoja wa wawaniaji 11 wa kiti cha meya wa jiji kuu Kampala.

Hata hivyo taarifa za sasa kutoka Kampala zinaonyesha kwamba Lord Mayor Erias Lukwago wa chama cha FD ambaye kitaaluma ni wakili na amewahi kuhudumu kama mbunge amehifadhi kiti chake.

Chameleone ameshindwa kwenye kinyang’anyiro hicho kinyume na ripoti za awali kwenye mitandao ya kijamii hata kabla ya uchaguzi wa umeya nchini Uganda kwamba alikuwa ameshinda.

Kwenye shughuli hiyo ya jana iliyoshuhudia idadi ndogo ya wapiga kura, Jose Chameleone alipiga kura katika kituo cha Kiduuka huko Mitungo akiwa ameandamana na kaka zake Pius Mayanja kwa jina lingine pallaso na Douglas Mayanja kwa jina lingine Weasel.

Kaka hao wawili pia ni wanamuziki.

Chameleone aliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kama mwaniaji huru baada ya kushindwa kupata tileti ya chama cha mwanamuziki mwenza Bobi Wine cha NUP ambayo ilitwaliwa na Latif Sebaggala.

Inasemekana kwamba Jose alikosa tikiti ya NUP kwa kukosa vyeti vinavyohitajika vya masomo na kukosa kitambulisho cha kitaifa.

Hata hivyo aliahidi kuendelea kumuunga mkono Bobi Wine ambaye alikuwa akiwania Urais wakati huo lakini kulingana na matokeo, alishindwa na Rais Yoweri Museveni.

Categories
Burudani

Sukari, Zuchu

Zuchu mwanamuziki anayeangaziwa zaidi katika kampuni ya WCB nchini Tanzania ana kibao kipya kwa jina “Sukari” ambacho alikiachia rasmi kwenye You Tube tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021.

Wimbo huo ulikuwa umesubiriwa kwa hamu na ghamu kutokana na namna alikuwa amefanya matayarisho ya ujio wake kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Alitafuta usaidizi wa watu kadhaa maarufu nchini Tanzania ambao wana umuhimu kwenye jamii kwa jumla ambao walirekodi video fupi kuhusu wasifu wao na mwisho wote wanamalizia kujirejelea kama sukari.

Mamake mzazi ambaye pia ni msanii kwa jina Khadija Omar Kopa ni kati ya waliosaidia kutangaza ujio wa kibao hicho cha Sukari. Kwenye video yake, Khadija anasifia burudani yake ambayo anasema ikosekanapo watu hutaharuki na watu huwa tayari kuigharamia wakati wowote. Onyesho zuri la usaidizi wa mama kwa mwanawe hasa katika kuendeleza talanta.

Mwingine kati ya watu hao mashuhuri ni muigizaji Wema Sepetu ambaye alisema kwamba urembo wake ndio ulimjengea jukwaa analosimamia kwa sasa tangu mwaka 2006 baada ya kushinda shindano la ulimbwende wakati huo na kutawazwa “Miss Tanzania”.

Aligusia pia kipaji chake cha uigizaji ambacho anasema ni cha hali ya juu zaidi na kwamba yeye ni sukari.

Kabla ya kuachilia kibao hicho, Zuchu naye alitoa video akisema kwamba anaamini kila mwanadamu ana umuhimu wake katika jamii. Umuhimu huo ndio anafananisha na ladha ya sukari huku akijirejelea kama sukari ya Zanzibar alikozaliwa.

Zuchu alikwenda kuhojiwa katika kituo cha redio cha Wasafi Fm katika kipindi cha jioni kwa jina Mgahawa ambapo alionyesha waliokuwepo jinsi ya kuuchezea wimbo huo.

Ikumbukwe kwamba alipoingia WCB alimhusisha mkubwa wake Diamond kwenye nyimbo kadhaa ambazo zilisababisha minong’ono kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.

Walikuwa wakiandamana kwenye maonyesho kadhaa lakini zamu hii Zuchu alikuwa peke yake alipokwenda kuhojiwa. Alisema Diamond alimpa ahadi ya kumshika mkono alipokuwa akianza lakini pia alimwambia kwamba kuna wakati atamwachilia afanye kazi peke yake.

Kama ilivyo mazoea nchini Tanzania, wengi wamerekodi video wakichezea wimbo huo mpya wa Zuchu kwa jina sukari na amechapisha hizo video kwenye akaunti yake ya Instagram.

Categories
Burudani

Mshairi wa umri mdogo zaidi wa uapisho wa Rais Marekani

Mwanadada Amanda Gorman wa miaka 22 tu amezungumziwa sana na kupata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii ulimwenguni kote kutokana na jukumu lake kwenye uapisho wa Rais Joe Biden nchini Marekani.

Amanda ndiye alichaguliwa na kamati ya kusimamia uapisho wa Rais wa 46 wa Marekani Joe Biden tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021. Shairi lake lenye mada “The Hill we Climb” yaani “Kilima tunachokwea” liligusa nyoyo za wote waliofuatilia uapisho wa Biden.

Ndani ya shairi hilo alifichua kwamba yeye ni mtoto wa mhamiaji mweusi nchini Marekani na alilelewa na mama tu ilhali amepata nafasi ya kukariria Rais shairi.

Aligusia pia haja ya umoja wa watu wote nchini Marekani na uhuru wa kuchagua ambao alisema unaweza kucheleweshwa lakini hauwezi kushindwa kabisa.

Sauti yake tamu na ufasaha wa matamshi vilivutia zaidi huku wengi wakimshangilia. Amini usiamini, Amanda alikuwa na tatizo la kuzungumza akiwa wa umri mdogo.

Hata hivyo alipenda sana kuandika na kusoma na mamake ambaye ni mwalimu aliendelea kumtia moyo na hatimaye akaweza kulishinda tatizo hilo la kushindwa kuzungumza.

Gorman ambaye alifuzu kutoka chuo kikuu cha Havard anaendesha shirika kwa jina “One pen One Page” ambalo linahimiza vijana kuandika mashairi na hata hadithi.

Baada ya sherehe hiyo ya uapisho wa Joe Biden na Kamala Harris, wafuasi wa Amanda kwenye mitandao ya kijamii walikuwa wameongezeka maradufu.

Kupitia Twitter alitoa shukrani zake huku akitaja wote ambao wamemtia moyo katika safari yake kama vile aliyekuwa mtangazaji wa runinga Bi. Oprah Winfrey.

Baadhi ya Marais nchini Marekani hususan wanne, wameonekana kuupa ushairi nafasi pale ambapo wanachagua mshairi kwa ajili ya sherehe zao za uapisho. Katika Historia ya taifa hilo, washairi ambao wametumika kwa sababu hiyo ni sita tu na Bi Amanda ndiye wa sita.

Mwaka 1961 mshairi Robert Frost alikariri shairi lenye mada “The Gift Outright” kwenye uapisho wa Rais John F Kennedy. Maya Angelou akakariri “On the Pulse of Morning” mwaka 1993 kwenye uapisho wa kwanza wa Bill Clinton huku Miller Williams akikariri “Of History and of Hope” kwenye uapisho wa pili wa Clinton mwaka 1997.

Katika uapisho wa kwanza wa Rais Barack Obama mwaka 2009, mshairi alikuwa Elizabeth Alexander na shairi liliitwa “Praise Song for the day”. Richard Blanco alikariri shairi “One Today” kwenye uapisho wa pili wa Rais Obama mwaka 2013.

Na wa mwisho ni mshairi nyota wa sasa Amanda Gorman ambaye pia ameandikisha historia kwa kuwa wa umri mdogo kati ya washairi wa sherehe za uapisho wa rais nchini Marekani.

Categories
Burudani

Lady Gaga asisimua kwenye uapisho wa Rais Marekani

Sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa 46 Joe Biden nchini Marekani jana Jumatano ilikuwa tofauti kidogo ikifananishwa na sherehe sawia awali.

Kutokana na janga linaloendelea la virusi vya Corona idadi ya wageni waliohudhuria ilikuwa ndogo sana na kila mmoja alikuwa amevalia barakoa.

Katika sehemu ambayo hukaliwa na wamarekani wa kawaida zamu hii kulijazwa bendera za marekani ambazo idadi yake inasemekana kukaribia laki mbili.

Lakini zaidi ya yote, mwanamuziki Lady Gaga alisisimua wengi waliohudhuria sherehe na waliokuwa wakitizama kote ulimwenguni kupitia runinga.

Yeye ndiye alipatiwa jukumu la kuimba wimbo wa taifa la marekani na alipoitwa na lango likafunguliwa, alitokea akiwa amevaa vazi lake refu la rangi mbili.

Sehemu ya juu ya nguo hiyo ilikuwa ya rangi nyeusi na ya chini ilikuwa ya rangi nyeusi. Kifuani alikuwa amepachika kinyago cha njiwa cha rangi ya dhahabu, kishwani nywele zilikuwa za rangi hiyo ya dhahabu na alikuwa na tabasamu wakati wote.

Alishuka ngazi kwa mwendo wa kipekee akisaidiwa na mmoja wa wahudumu wa bendi ya polisi na alipofika jukwaani alipokezwa kipaaza sauti chake cha kipekee cha rangi ya dhahabu.

Mwanadada huyo alipofungua kinywa kuimba kila mmoja alitulia na kufuatilia sauti yake ya kipekee huku akigeuza macho kuangalia bendi na kuangalia bendera za Marekani zilikokuwa zimesimikwa.

Alipokamilisha uimbaji wake alishangiliwa na watu mashuhuri ambao walikuwepo na akachukuliwa tena na yule mhudumu wa bendi ya polisi aliyemwelekeza hadi kwenye kiti chake.

Stefani Joanne Angelina Germanotta wa miaka 34 amezungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii kutokana na jinsi aliimba kwenye uapisho wa rais huku wengi wakikosa kuridhika na uimbaji wa Jennifer Lopez wa wimbo, “This Land is your land”.

Categories
Burudani

Steve Nyerere akumbuka wema wa Mr. Nice

Jamaa mmoja nchini Tanzania kwa jina Steve Nyerere ambaye ni mchekeshaji amemkumbuka mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Mr. Nice kwa mema aliyomtendea.

Kulingana na Nyerere, yeye na wengine walikuwa walinzi wa Mr. Nice wakati alikuwa maarufu sana na muziki ulikuwa ukimlipa vizuri.

Nyerere anakumbuka kwamba yeye na wenzake walikuwa wakipigwa kila mara walipokuwa wakimpeleka mkubwa wao kwenye matukio mbali mbali.

Anakumbuka wakati mmoja yeye na rafiki yake Ray Kigosi walikuwa na njaa na hawakuwa na la kufanya. Wakahimizana waende nyumbani kwa Mr. Nice kutafuta usaidizi.

Anasema walibisha lango kuu wa muda bila jibu ndiposa wakaamua kuruka ua wa ukuta na kuingia ndani ambapo walimpata Mr. Nice amelala wakamwamsha.

Jambo la kwanza alitaka kujua toka kwao ni jinsi waliingia humo, wakawa wakweli wakasema waliruka ua. Akaita mlinzi kudhibitisha hayo akapata ni kweli.

Baada ya hapo aliwapa sikio ili kujua kilichowaleta kwake na wakamwambia walikuwa wanahisi njaa na hawakuwa na pesa za kununua chakula.

Hawakuamini macho yao pale ambapo Mr. Nice aliwapa kadi yake ya benki, namba za siri na akawaamrisha wakajitolee milioni moja tu pesa za Tanzania kasha wairudishe.

Steve Nyerere anasema waliimba nyimbo za Mr. Nice mwendo wote na kurudi. Anamshukuru mwanamuziki huyo ambaye sikuhizi anasuasua katika kazi yake ya muziki na kumwombea Baraka kwa mwenyezi Mungu.

Mr. Nice ni mmoja kati ya wanamuziki walioanzisha mtindo wa kizazi kipya nchini Tanzania kwa jina Bongo Fleva.

Anasemekana kupata pesa nyingi wakati huo ambazo wengi wanasema hakuwekeza ila katumia vibaya.

Categories
Burudani

Ushauri wa Professor Jay

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Tanzania ambaye pia ni mwanasiasa Professor Jay kwa jina halisi Joseph Haule ametoa ushauri kwa wanamuziki nchini Tanzania.

Ushauri huo aliupa mada ya “Shule ya Bure” kasha akaandika “Sio lazima kila siku uimbe matusi na mambo ya kitandani ili wimbo wako uwe mkubwa na upendwe, bali unaweza kuimba wimbo wenye mafunzo mema kwa jamii na wadau wakakushika mkono kwa kiwango cha juu kabisa. Kwa pamoja tunaweza kuokoa kizazi hiki.”

Jay anaonekana kukwama kwenye maadili yaliyokuwepo kwenye fani ya muziki tangu wakati walianza muziki.

Bidii yake ya kutafuta kurejesha maadili inaonekana kushabihiana na ile ya mashirika mbali mbali ya serikali nchini Tanzania kama vile BASATA.

Maajuzi Professor Jay amerejelea muziki baada ya mapumziko ya zaidi ya miaka mitano wakati akihudumu kama mbunge wa eneo la Mikumi.

Wimbo wake na Stamina kwa jina Baba unaendelea kufanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

Unagusia uhusiano kati ya mvulana na babake na maadili kwa jumla. Mvulana huyo anamkosea babake heshima kwa sababu ya ufukara na baadaye babake anamfichulia kwamba yeye sio babake mzazi ila ni baba mlezi.

Muda mfupi baada ya uzinduzi wa wimbo huo, ndipo habari zilichipuza kuhusu baba mzazi wa mwanamuziki Diamond Platnumz na wengi wanashangaa ikiwa Jay na Stamina walikuwa na habari kuhusu hilo.

Categories
Burudani

Tiffany Trump atangaza uchumba

Siku za mwisho za Rais Donald Trump mamlakani ndio wakati kitinda mimba wake kwa jina Tiffany alichagua kutangaza kwamba amechumbiwa.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Tiffany aliweka picha akiwa na mpenzi wake Michael wakiwa nje ya ikulu ya Rais maarufu kama “White House”.

Katika maelezo anasema imekuwa heshima kuu kusherehekea mengi, matukio ya kihistoria na kujenga kumbukumbu na familia yake katika hiyo ikulu lakini kuu kwake ni kuchumbiwa humo na mpenzi wake Michael. Anasema ana furaha kuingia kwenye ukurasa unaofuatia wa maisha yao pamoja.

Michael naye aliweka picha hiyo hiyo kwenye akaunti yake na kusema “Nilichumbia mpenzi wa maisha yangu. Natizamia yanayofuatia katika maisha yetu.”

Tiffany Trump amekuwa akikaa mbali na jicho la umma tofauti na ndugu zake wengine lakini aliwahi kuzungumza kwenye mkutano wa chama cha Republican mwezi Mei mwaka jana.

Wakati huo, hotuba yake ililenga kuhimiza watu wa taifa la Marekani kumchagua babake kwa mara nyingine lakini hilo halikutimia.

Alishindwa na Joe Biden wa chama cha Democratic kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana na anastahili kumkabidhi mamlaka leo tarehe 20 mwezi Januari mwaka 2021.

Tiffany ana umri wa miaka 27 na Michael ana umri wa miaka 23 na walionekana pamoja wakati Rais Trump alikuwa akitoa hotuba kuhusu hali ya taifa la Marekani.

Mamake Tiffany ni Bi. Marla Maples na wala sio Melania Trump.

Categories
Burudani

Wewe ni kakangu, ibaki hivyo! Wendy Williams azomea kakake

Mtangazaji wa runinga nchini Marekani kwa jina Wendy Williams jumatatu asubuhi alianza kipindi chake kwa njia ambayo wengi hawakutarajia.

Aliamua kumjibu kakake Tommy Williams ambaye alikuwa amedai kwamba Wendy hakuhudhuria mazishi ya mama yao mzazi mwezi Disemba mwaka 2020.

Kwenye video hiyo ya You Tube Tommy anasema “Ni nini kitamfanya mtu asihudhurie matanga ya mamake? Sielewi kutompa heshima za mwisho mtu ambaye alikuwa nawe kila wakati na akakusaidia. Unawezaje kuendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichotendeka?”

Katika kipindi cha Jumatatu tarehe 18 mwezi Januari mwaka 2021, Wendy Alisema “Nilikuwa napekua mitandao ya kijamii kuona mawazo ya watu kuhusu kipindi chetu cha Wendy Williams Show, kisha nakutana na maneno kama “Ndugu yako hakupendi” mara “Kuwa makini sana na ndugu yako”. Tommy acha nikwambie kitu, wewe ni kakangu, acha kusema unayoyasema kwani sasa yameanza kuingilia kazi zangu.”

Wendy ambaye ni mcheshi alionekana kukasirishwa sana na maneno ya kakake huku akimwonya aache kumwekelea tabia ambayo si yake la sivyo yeye atoe maneno yake ya kweli na ithibati tosha.

“Ukitaka kuzungumza kwenye mitandao sema maneno ambayo unadhani unajua kujihusu.” aliendelea kusema mtangazaji huyo wa miaka 56 sasa na mara moja akageukia kazi ambapo aliuliza watazamaji ikiwa walipenda vazi lake.

Wendy Williams alikuwa na uhusiano mzuri na marehemu mamake kwa jina Mrs Williams ambaye alikuwa akimhusisha kwenye kipindi mara kwa mara.

Wakati mmoja mamake Wendy alihadhithia jinsi kuzaliwa kwa Wendy kuliiletea familia nzima msisimuko maanake walikuwa wanapitia wakati mgumu.

Nyanyake Wendy alikuwa akiugua saratani ya utumbo na aliaga dunia miezi michache baada yake kuzaliwa.

Hata baada ya kuzomewa kwenye runinga, Tommy anaendelea kusisitiza kwamba Wendy hakuhudhuria mazishi ya mama yao. Anasema hata baba yao hakufurahia na jambo hilo linamkwaza hadi sasa.

Anasema alihadaa familia kwamba angesafiri wakati wa mazishi ya mama yao ilhali hakusafiri.

Categories
Burudani

Rayvanny kuzindua albamu

Msanii wa Bongo Fleva Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny ama ukipenda vanny Boy ametangaza kwamba ataachilia albamu yake ya kwanza hivi karibuni.

Vanny ambaye anafanya kazi ya muziki chini ya kampuni ya Diamond Platnumz Wasafi Classic Baby – WCB alianza muziki mwaka 2011 akiwa shule ya upili lakini hajawahi kuzindua albamu.

Alijiunga na WCB rasmi mwaka 2015 na mwaka 2016 akaachilia kibao “Kwetu” ambacho kilivuma sana Afrika mashariki.

Mwezi wa pili mwaka 2020 Rayvanny alizindua EP yake kwa jina “Flowers” ambayo ilifanya vyema kwenye mitandao ya kijamii.

EP au ukipenda ‘Extended Play’ ni mkusanyiko wa nyimbo ambazo hazitoshi kuitwa albamu. Mwanamuziki huyo ameteuliwa kuwania na kushinda tuzo kadhaa.

Ni kati ya wanamuziki wanaofanya vizuri katika WCB na mkubwa wake Diamond aliwahi kufichua kwamba alikuwa akijenga studio zake za muziki isijulikane kama atagura WCB alivyofanya Harmonize.

Diamond alisifia sana studio hizo akisema kwamba zikikamilika zitakuwa bora zaidi Afrika mashariki.

Rayvanny amejulikanisha ujio wa albamu hiyo kwa jina “Sound From Africa” kupitia picha na video ambazo amekuwa akiweka kwenye mtandao wa Instagram lakini hajatangaza tarehe rasmi ya kuiachilia.

Categories
Burudani

Maggy Bushiri arejea Tanzania

Mwanamuziki Maggy Bushiri amerejea nchini Tanzania kutoka Marekani anakoishi kwa ajili ya kuzindua nyimbo kadhaa.

Alikuwa ameandamana na mpenzi wake kwa jina Martin Classic ambaye pia ni mwanamuziki na wameshirikiana katika nyimbo kadhaa. Wawili hao waliwasili wakiwa wamevalia barakoa nyeusi ila walizivua mara tu walipolakiwa na wenyeji wao.

Barakoa hazitumiki nchini Tanzania hasa baada ya serikali nchini humo kutangaza mwaka jana kwamba ugonjwa wa Covid 19 ulikuwa umeisha humo.

Maggy Bushiri ni mzaliwa wa Congo, ila alilelewa nchini Tanzania kwa muda kidogo na baadaye yeye, ndugu zake na mamake wakahamia marekani kama wakimbizi.

Kulingana naye, aliondoka Tanzania akiwa na umri wa miaka miwili kuelekea Mozambique na baadaye wakaelea Marekani.

Alipohojiwa mwaka 2019 nchini Tanzania, alielezea kwamba babake aliaga dunia kabla wagure Tanzania na mamake akaaga dunia mwaka 2009 wakiwa nchini Marekani.

Kwenye mahojiano hayo pia alifichua kwamba alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Los Angeles anakoishi na anasomea mambo ya uanahabari hasa uundaji wa vipindi.

Mwaka 2018 alihojiwa na jarida la Los Angeles kwa jina “VoyageLA” ambapo alifichua kwamba haikuwa rahisi kuingilia muziki kwani mara nyingi aliambiwa hatoshi.

Wimbo wake ambao anasema ulifanya ajulikane zaidi ni “Swing Your Body”. Wakati huo alifichua mipango yake ya siku za halafu, ile ya kufungua kampuni ya mavazi ambapo rangi kuu itakuwa Zambarau au ukipenda Purple.

Anapenda sana rangi hiyo naye hujiita “The Purple Queen” ila alipowasili Tanzania jana, hakuwa na nywele za rangi ya Zambarau kama siku za awali.

Alizungumzia pia mipango ya kurejea alikozaliwa na kuanzisha kituo kikubwa ambacho kitakuwa makazi ya kuhudumia mayatima.

Inasubiriwa sasa kuona mazuri ambayo ameletea mashabiki wake wa Tanzania mwaka huu wa 2021.