Categories
Burudani

Nandy na Billnass wameachana

Wanamuziki Nandy na Billnass wametengana baada ya uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu. Mara ya kwanza kwa watu kukisia kwamba mambo sio mazuri, ni wakati Nandy alijitokeza kutangaza kwamba pete ya uchumba aliyovishwa na Billnass ilikuwa imepotea.

Wengi walihisi kwamba Nandy alivua pete hiyo mwenyewe lakini amekuwa akijitetea akisema kwamba alivuliwa na mashabiki bila kujua kipindi cha kutumbuiza kwenye mikutano ya Kampeni mwaka jana.

Mara nyingine ni wakati alikwenda kumlaki mwanamuziki Koffi Olomide kwenye uwanja wa ndege yapata mwezi mmoja uliopita na alikuwa amemwalika kwa ajili ya kufanya kibao naye.

Nandy hakuwa na Billnass jinsi wengi walitarajia lakini Nandy alisema kwamba mpenzi huyo wake alikuwa naye kwenye mipango yote hata ingawa hakuonekana huko kwenye uwanja wa ndege.

Baadaye Nandy na Koffi walitumbuiza tena kwenye tamasha lililokuwa limeandaliwa na Clouds Media kwa ajili ya siku ya wapendanao lakini Billnass hakuonekana huko. Mamake Nandy alipohojiwa siku hiyo alisema mambo kati ya wanawe yalikuwa sawa na alikuwa anasubiri tu wampe siku ya arusi.

Billnass na Nandy

Siku ya kuzindua kibao chake na Koffi kwa jina “Leo Leo” kwenye kipindi cha “Leo Tena” cha Clouds Tv Billnass pia hakuonekana na Nandy aliendelea tu kumtetea akisema anamuunga mkono kwa kazi yake.

Nandy mwenyewe alitangaza utengano wake na Billnass wakati alikuwa anajibu shabiki mmoja ambaye alimwita mke wa Billnass kwenye picha aliyopachika kwenye Instagram.

Shabiki huyo kwa jina carinamarapachi aliandika “Mrs Billnass love uu more” naye Nandy akamjibu “Single”.

Categories
Burudani

Firirinda Weekend!

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini Kenya KFCB Daktari Ezekiel Mutua ametangaza Wikendi inayoanza kesho kuwa wikendi ya Firirinda.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook Dakta Mutua aliandika, “Nimetangaza wikendi ijayo kuanzia kesho Ijumaa hadi Jumapili kuwa wikendi ya Firirinda kwa heshima yake na kwa ajili ya kusaidia mwandishi na mwimbaji wa wimbo huo ambaye anaugua Mzee Dickson Munyonyi. Wapiga muziki kwenye hafla zote za wikendi hii wanaombwa wacheze wimbo huo na kuhimiza mashabiki wao kuchanga fedha za kusaidia kulipa ada ya hospitali ya mwanamuziki huyo mkongwe ambaye anaendelea kupokea matibabu. Nambari ya kutuma fedha hizo kwa njia ya simu itatangazwa baada ya sisi kuwasiliana na familia na mimi nitaanzisha mchango kwa shilingi laki moja. Tuujulikanishe wimbo huu lakini zaidi na la maana ni kuutumia kusaidia mwimbaji wake ambaye anatupa kumbukumbu huku tukisherehekea utamaduni wetu.”

Dakta Mutua anasema changamoto ya Firirinda kwenye mitandao ya kijamii inafaa kuchukua mahala pa ile ya Jerusalema!

Alitumia nafasi hiyo pia kuomba yeyote ambaye anafahamu familia ya mzee huyo awasiliane naye ili amuunganishe nayo.

Kulingana na Mutua, Firirinda ni neno ambalo linatokana na maneno mawili Free la kiingereza na Rinda la kiswahili kuashiria vazi la kike.

Categories
Burudani

Nkechi Blessing aomba msamaha hadharani

Kwa muda sasa kumekuwa na mtindo wa kushangaza nchini Nigeria, ambapo mashabiki sugu wa watu maarufu wanachora picha za watu hao maarufu kwenye miili yao au kuandika majina yao na wengi wa watu hao maarufu wanaonekana kushukuru mashabiki hao kwa kuwapa pesa.

Kisa kama hicho kilitokea kwa muigizaji wa filamu za Nollywood Nkechi Blessing Sunday na akawa mwepesi wa kusuta shabiki huyo wake ambaye aliandika herufi za kwanza za jina lake kwenye mkono wake.

Blessing alimkaripia msichana huyo ambaye alitambuliwa tu kama Oyindamola kwa kuandika herufi hizo kwa wino wa kufutika kwa nia ya kupata pesa kutoka kwake.

Muigizaji huyo ambaye pia ni mwanabiashara amejipata pabaya kwenye mitandao ya kijamii nchini Nigeria ambapo amekashifiwa kwa jinsi alimchukulia shabiki wake na amelazimika kuomba msamaha hadharani.

Nkechi Blessing Sunday ametumia akaunti yake ya Instagram kuomba msamaha ambapo amepachika picha ya mazungumzo yake na shabiki huyo wake ambayo yanaonyesha kwamba tayari walikuwa wamezungumza kwa simu.

Nkechi anasihi wafuasi na mashabiki wengine wamsaidie kuomba msamaha na pia wamsamehe kwa kosa alilotenda na kutelekeza shabiki wake sugu na hata kumtusi badala ya kumwonyesha mapenzi.

Haijulikani hatua atakayochukua Nkechi kwa kushukuru shabiki huyo wake kwa kumwonyesha mapenzi.

Mwanadada mwingine kwa jina Ewatomi Gold alichora sura ya Bobrisky kwenye mwili wake jambo ambalo lilisababisha babake mzazi amkane na Bobrisky pia hakuwa amemtambua kwa hatua hiyo.

Baadaye Bobrisky alimtafuta na kumzawadi pesa na kuahidi kumpa zawadi nyingine nyingi.

Categories
Burudani

Jennifer Lopez asifia mwanadada maarufu kwenye Tik Tok

Charli D’Amelio ni binti wa umri wa miaka 16 ambaye sasa ni maarufu nchini Marekani kutokana na wingi wa wafuasi wake kwenye mtandao wa Tik Tok ambao ni wafuasi milioni 108.7.

Jambo hilo limesababisha atambuliwe na wengi na wa hivi karibuni ni mwanamuziki wa muda mrefu Jennifer Lopez au ukipenda J’Lo.

J’Lo alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alisema Charli kwa sasa ndiye kijana maarufu zaidi nchini Marekani na sio tu kwa sababu anasakata densi kwenye TikTok bali pia kwa sababu anajua anachokifanya na anajua pia kuvutia wengi ambao wanataka kuwa kama yeye.

Lopez alifichua kwamba mara ya kwanza kukutana na Charli ni wakati wa shindano la mpira wa miguu kwa jina Super Bowl mwaka 2020 ambapo alipata nafasi ya kutumbuiza naye jukwaani.

Charli D’Amelia anasema kusifiwa na nyota mkubwa kama J’Lo ni jambo zuri na hajui aseme nini. Msichana huyo alipata fursa ya kuwa kwenye orodha ya Time100 ambapo J’Lo alikuwa ameandika makala hayo.

Time 100 ni makala ya kila mwaka ya jarida maarufu la “Time” na huwa yanaorodhesha watu 100 ambao ni maarufu kwa mwaka huo na ambao wana ushawishi mkubwa.

Kwenye makala hayo J’Lo aliandika, ” kufikisha wafuasi milioni 100 kwenye TikTok sio jambo dogo. Nilipokutana na Charli D’Amelio kwenye Super Bowl LIV mwaka 2020, niliona ana mvuto wa kipekee ambao kila msanii anahitaji ili kuvutia umati.”

Mwaka jana, Lopez alimhusisha D’Amelio kwenye mojawapo ya video zake za nyimbo.

Categories
Burudani

Mzee Abdul afungua akaunti ya Instagram

Mzee Abdul ambaye alipata kujulikana na wengi kama baba mzazi wa mwanamuziki Diamond Platnumz sasa amefungua akaunti kwenye mtandao wa Instagram na anataka wafuasi na biashara.

Kwenye video ambayo iliwekwa kwenye akaunti ya Amber Ruty, mzee huyo anasikika akitangaza akaunti yake mpya ambayo ni “Mzee_Abdul_Official” huku akisihi mashabiki wamfuatilie huko na wanaotaka kutangaza biashara zao pia wamtafute huko.

Utangazaji wa bidhaa au huduma kupitia mitandao ya kijamii umegeuka kuwa kitega uchumi kwa watu wengi maarufu ulimwenguni na sasa mzee huyo naye ameamua kufuata njia hiyo.

Mzee abdul Juma amejaribu pia muziki ila inaonekana fani hiyo hakuipendelea maanake imekuwa muda wa mwaka mmoja sasa tangu kibao kwa jina “Dudu la Yuyu” ambacho alimshirikisha Sungura Madini kizinduliwe.

Picha ya kwanza ambayo alipachika kwenye akaunti yake mzee Abdul ni yake akiwa amebanwa na kina dada wawili na mmoja ni Amber Ruty.

Anamshukuru Ruty kwa kumjali siku zote na kukashifu wasiomjua kwa undani kwani yeye ni mtu mzuri hayuko vile wengi wanamdhania.

Amber Ruty, mume wake na rafiki yao wa kiume waliachiliwa kutoka gerezani maajuzi baada ya kuweza kulipa faini kwa koosa la kuchapicha video yao ya ngono.

Tangazo la akaunti ya Mzee Abdul limejiri yapata mwezi mmoja tangu mamake Diamond akiri kwamba yeye siye baba mzazi wa mwanamuziki huyo Diamond Platnumz.

Kabla ya hapo wengi walikuwa wamemsuta Diamond sana kwa kutosaidia babake Mzee Abdul ambaye picha zake zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo alionekana akiabiri gari la uchukuzi wa umma akiwa amebeba gunia.

Categories
Burudani

Mejja afurahia baada ya wimbo wake kuchezwa nchini Marekani

Mwanamuziki wa mtindo wa Genge Mejja ana kila sababu ya kutabasamu baada ya wimbo wake mpya kuchezwa kwenye ukumbi wa mchezo wa mprira wa kikapu nchini Marekani shindano likiendelea.

Wimbo huo kwa jina “siskii” ameuzindua hivi karibuni na tayari umependwa ulimwenguni kama tu nyimbo zake za awali. Mwanamuziki huyo ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa mtindo wa Genge amekuwa akikashifiwa na wengi kwa kufanya kazi na wanamuziki wengi hasa wanaoibukia.

Mejja hata hivyo alifafanua kwamba hiyo ndiyo njia yake ya kusaidia wanamuziki wapya ili wajiendeleze na wapate kujulikana.

Mejja alipachika video fupi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii ambayo inaonyesha mchezo wa mpira wa kikapu ukiendelea huku kibao chake kikichezwa.

Alishukuru mpiga muziki ambaye alikuwa kazini katika sehemu hiyo ambaye anajiita @poizonivythedj kwenye mitandao ya kijamii na anasema amekuwa akiinua na kujulikanisha muziki wa Genge nchini Marekani.

Poison Ivy The Dj kwa jina halisi Ivy Awino ni mpiga muziki wa Marekani mwenye asili ya Kenya.

Haya yanajiri wakati ambapo Mejja na Madtraxx wamejipata pabaya kutokana na shutuma kutoka kwa Kid Kora ambaye alikuwa mwenzao chini ya kundi la “The Kansoul”.

Kupitia mitandao ya kijamii, Kora amekuwa akishtumu wawili hao kwa kile ambacho anakitaja kuwa ulaghai na sasa anataka wamlipe pesa zake.

Madtraxx na Mejja hawajajibu madai hayo kufikia sasa na haijulikani kama Kora ataamua kutumia vyombo vya sheria kupata haki yake.

Categories
Burudani

Baba Levo amshukuru Diamond Platnumz

Mwanamuziki na mtangazaji wa kituo cha redio cha Wasafi Fm nchini Tanzania Revokatus Kipando maarufu Baba Levo anamshukuru mwanamuziki Diamond Platnumz kwa kumsaidia kuendelea umaarufu wake jambo ambalo limemletea mengi mazuri.

Kupitia Instagram mtangazaji huyo aliandika, “KUWA KARIBU NA WEWE IMETOSHA KUNIPA PESA AMABAYO SIKUTEGEMEA KUJA KUISHIKA NA UZEE HUU.. Naomba Niweke wazi Kwa Mashabiki Wangu Kwamba Kabla Ya Mwezi Huu Kuisha Nitakuwa Nimesain Mikataba Na MAKAMPUNI TISA MAKUBWA Yote Yanataka Niwe BALOZI Wao Kwenye Bidhaa Zao Tofauti Tofauti… Niseme Tena ASANTE @diamondplatnumz Asante Sanaaa..”

Diamond alijibu usemi huo wa Baba Levo akimwita “Fundi Majumba” na kisha kuweka ishara ya moto na kilipuzi kuonyesha kwamba amekubali shukrani zake.

Wiki tatu zilizopita msanii huyo alizua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii kwa kusema kwamba yeye angekuwa mwanamke kama Zuchu, angemzalia Diamond watoto watatu.

Usemi huo ulisababisha wengi kumrejelea Baba Levo kama chawa jina ambalo analikubali kwa kuwa mara nyingi huwa yuko karibu sana na Diamond Platnumz ambaye ni mkubwa wake kikazi.

Huwa anazungumzia utajiri wa Diamond Platnumz hadharani huku akisema kwamba anakubali kamzidi kifedha lakini atatumia umaarufu wake ili naye aendelee.

Categories
Burudani

Davido azuru makazi yake ya awali nchini Marekani

Mwanamuziki wa nchi ya Nigeria David Adedeji Adeleke maarufu kama Davido amezuru makazi yake ya miaka 12 iliyopita nchini Marekani akisema aliishi kwenye nyumba hiyo na binamuze wawili.

Kulingana naye, wakati huo ambao ni mwaka 2009, yeye na binamu zake wawili hawakua na pesa ila walikuwa na ndoto ya kuwa bora siku za usoni.

Hata ingawa wazazi wa Davido walikuwa na uwezo mkubwa kifedha, anasema hawakupata uungwaji mkono wakati huo, walijisimamia tu na kupigania ndoto zao na sasa hata kama hawajakwenda mbali sana wanajiweza.

Wengi wa wafuasi wa Davido kwenye mtandao wa Instagram hata hivyowalipuuza maneno yake kwani wanaamini kwamba alikuwa na uwezo kwa kutizama uwezo wa wazazi wake kifedha.

Davido aliendelea kwa kuhimiza mashabiki wasije wakakata tamaa maishani ila wajikakamue na siku za usoni wataafikia ndoto zao.

David adedeji Adeleke anachukuliwa kuwa m- Marekani na m-Nigeria kwani alizaliwa huko Atlanta, Georgia nchini Marekani lakini akaamua kurejea walikozaliwa wazazi wake kwa ajili ya kufanya kazi yake ya muziki.

Alipenda muziki sana kiasi cha kuacha kusomea kozi ya biashara ambayo wazazi wake walitaka asomee kwenye chuo kikuu cha Oakwood na kuingilia muziki.

Alifanikiwa kununua ala kadhaa za kisasa za muziki akiwa kwenye chuo hicho kikuu na kuanda kuunda muziki punde baada ya kuacha masomo na alishirikiana na binamu zake B Red na Sina Rambo kwenye muziki.

Baadaye alihamia London Uingereza kwa ajili ya kujifunza kutumia sauti yake vizuri kama mwanamuziki na mwaka 2011 akarejea kwenye mizizi yake nchini Nigeria.

Ilibidi asimamishe kazi ya muziki kwanza ili kutimiza agizo la babake mzazi la kusoma katika chuo kikuu na kufikia mwaka 2015 akafuzu kutoka chuo kikuu cha Babcock nchini Nigeria na shahada ya muziki.

Amini usiamini babake alilipa chuo hicho kikuu hela nyingi ili kuanzisha kozi hiyo ya muziki na Davido alikuwa mwanafunzi pekee wa kozi hiyo wakati huo.

Categories
Burudani

Erica na Safaree kuachana

Muigizaji wa vipindi vya runinga nchini Marekani Erica Mena amekubaliana na maneno ya mume wake Safaree Samuels baada ya kusema kwenye mitandao ya kijamii kwamba ndoa yake ni kosa kubwa.

Safaree Samuels ambaye ni mwanamuzuki wa mtindo wa rap kutokea Jamaica aliamua kutumia Twitter jana kutangaza hisia zake ila kufikia sasa amefuta maneno hayo.

Alisema ” Namaanisha hili kutoka moyoni, kuoa ni mojawapo ya makosa makubwa ambayo nimewahi kufanya maishani na halitawahi kujirudia.”

Samuels aliongeza kusema kwamba ameamua kuondoka kabla ya kuchukua hatua ambayo itasabisha afungwe jela kwa sababu za kijinga na kwamba hakuna mwanadamu anatosha kwake kupoteza uhuru wake.

Mena naye aliamua kujibu kupitia Twitter ambapo alisema kwamba aliamua hivyo kwa sababu mume wake alikimbilia mitandao ya kijamii kama msichana mdogo.

“Nakubaliana nawe kwa hili. Wewe ndiye mtu mchoyo zaidi, mtu bure na mtu asiyefikiria wengine na sio kwangu tu bali kwa binti yetu pia”. Aliandika Erica.

Mwanadada huyo aliendelea kwa kusema kwamba kwa heshima ya binti yao na kwa kuheshimu kukua kwake kama mwanamke ameamua kurejelea kazi yake ili aunde pesa na ajali maisha yake.

Jambo lingine ambalo alisema ni kwamba yeye hapendi kufurahisha watu kwenye mitandao ya kijamii na mambo yake ambayo yanastahili kuwa ya siri.

Nyota hao wawili walifunga ndoa mwaka 2019 na wana mtoto msichana wa umri wa mwaka mmoja kwa jina “Safire Majesty”.

Hii sio mara ya kwanza kwa mwanamuziki Samuels kutishia kumtaliki Mena, mwezi Novemba mwaka jana, aliandika kwenye Twitter kwamba alikuwa ameamua kumaliza mwaka huo kwa njia nzuri ambayo ni kuwa Kapera.

Categories
Burudani

Idris Elba atangaza ujio wa kibao chake na Megan Thee Stallion

Muigizaji, mwanamuziki na mpiga muziki au ukipenda Dj Idris Elba amefichua kwamba amekuwa akiunda muziki na mwanamuziki Megan Thee Stallion.

Idris aliyasema hayo kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Uingereza kwa jina “Capital Fm” na aliongeza kusema kwamba kibao hicho ni cha uzuri wa hali ya juu.

Alisema pia kwamba amefanya kibao kingine na Franky Wah nawatakizindua hivi karibuni. Muigizaji huyo amewahi kufanya kazi ya muziki na wanamuziki tajika kama vile Wiley, Sean Paul na MC Kah-Lo na anatumai kwamba atafanikiwa kushirikiana na Taylor Swift pia.

Anasema amemfahamu Taylor kwa muda sasa huku akisema wengi hawajui jinsi anajikaza wao huona tu albamu, mauzo na tuzo wasijue msanii anavyojikakamua.

Kulingana naye, itakuwa raha kushirikiana na Taylor.

Idrissa Akuna Elba, wa umri wa miaka 48 sasa, ni mzaliwa wa London Uingereza lakini ana asili ya Sierra Leone Barani Afrika. Mamake mzaliwa wa Ghana na babake mzaliwa wa Sierra Leone, walikutana na kuoana nchini Sierra Leone kabla ya kuhamia Uingereza.

Wengi walimfahamu Idris kutokana na fani ya uigiizaji wa filamu lakini baadaye aliingilia kazi ya muziki.