Cardi B amaliza kesi iliyoanzishwa na aliyekuwa meneja wake

Mwanamuziki wa Marekani Cardi B ana kila sababu ya kutabasamu tunapokamilisha mwaka 2020 ambao umekuwa mgumu kwa wengi ulimwenguni kote. Hii ni baada ya kutamatisha kesi ambayo alikuwa ameshtakiwa na Klenord Raphael kwa jina lingine “Shaft” ambaye alikuwa meneja wake kitambo.

Mwaka 2018 Klenord alikwenda mahakamani akamshtaki Cardi B akitaka amlipe dola milioni kumi kwa kile ambacho anakitaja kuwa kutelekezwa na Cardi baada ya kumsaidia kuanzisha fani yake kama mwanamuziki.

Cardi naye aliweka kesi ya kupinga madai ya Klenord mahakamani na kesi hizo zimekuwa zikiendelea kwa karibu miaka mitatu sasa.

Klenord ametambuliwa kwa kusaidia Cardi kuandika wimbo kwa jina ” Bodak Yellow” kwa usaidizi kutoka kwa kundi la KSR na akamsaidia pia kufika kwa kampuni ya utangazaji ya “Love and Hip Hop” lakini baadaye mwanadada huyo akamwacha na kujiandikisha na kampuni ya muziki kwa jina “Solid Foundation Management”.

Kesi za wawili hao zilitupiliwa mbali na mahakama mkesha wa siku kuu ya Krismasi huku Korti ikiarifiwa kwamba wawili hao walikuwa wamekubaliana kwamba kesi ambazo walikuwa wamewasilisha zitupiliwe mbali.

Mwanamuziki huyo anafurahi kwamba sasa yuko huru na atalipwa marupurupu yote ambayo hajakuwa akipata.

Kwenye kesi aliyoanzisha mahakamani kwa nia ya kupinga ile ya kushtakiwa na Klenord, Cardi B alielezea kwamba hakuwa na mkataba naye na kwamba alikuwa anaingilia maisha yake na hata kutaka kumchagulia mpenzi wakati huo.

Anamkosoa pia kwa kutokuwa mwaminifu kwenye hesabu za pesa ambazo walikuwa wanalipwa kutokana na kazi yake ya muziki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *