Bunge la Seneti kujadili hotuba ya Rais

Bunge la Seneti leo linatarajiwa kujadili hotuba ya kuhusu hali ya taifa la Kenya iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi wiki iliyopita.

Kulingana na katiba, Bunge linapaswa kujadili yaliyomo kwenye hotuba hiyo kati ya siku tatu na nne baada ya Rais kuhutubu.

Maseneta wataangazia maswala mbali mbali ikiwemo ripoti ya saba ya kila mwaka kuhusu hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana katika harakati za kuafikia maadili ya kitaifa na misingi ya uongozi.

Ripoti ya kila mwaka kwa Bunge kuhusu usalama wa kitaifa na ripoti ya pamoja ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ya miaka ya kifedha ya 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020 pia zitajadiliwa.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta aliangazia maswala kadhaa ya kitaifa ikiwemo ripoti ya mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, juhudi za kupambana na janga la Corona na ufunguzi wa shule.

Rais aliwahakikishia Wakenya kwamba hali ya taifa hili iko imara licha ya changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na janga la ugonjwa wa COVID-19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *