Brigid Kosgei alenga kuboresha rekodi yake ya dunia katika mbio za marathon

Bingwa mara mbili wa London Marathon Brigid Kosgei amesema kuwa analenga kuvunja rekodi ya dunia  ya saa 2 dakika 14 na sekunde  4 aliyoandikisha mwaka 2019 katika mbio za Chicago marathon.

Kosgei aliye na umri wa miaka 26 amesema akipata maandalizi mazuri anao uwezo wa kuboresha rekodi ya dunia kwa dakika 2 au moja .

Bingwa huyo mtetezi wa Chicago na London  marathon amesema haya mapema Alhimisi aliposaini mkataba wa miaka miwili na benki ya Stanbic Kenya kuwa balozi wa benki.

Kosgei hata hivyo amesema hana uhakika ni lini atajaribu kuboresha rekodi hiyo lakini tayari alikuwa ameanza mazoezi ambapo alinuia kushiriki mbio za nusu marathon za Ras Al Khaimah maarufu kama RAK zilizokuwa ziandaliwe katika muungano wa milki za kiarabu UAE  tarehe 19 mwezi huu,kabla ya kufutiliwa mbali siku ya Jumatano kutoka na janga la covid 19.

“Nafikiria nikijiandaa vizuri naweza kuboresha rekodi ya sasa ya dunia kwa dakika 2 au tatu ingawa sina uhakika ni katika mashindano  yapi.Nilipanga kushiriki half narathon ya RAK tarehe 19 mwezi huu lakini baada ya kuskia kuwa zimeahirishwa Jumatano hadi mwaka ujao sasa nitaanza kupanga upya kwa kuwa pia mwaka huu hatuna uhakika wa mashindano mengi kutokana na Covid 19″akasema Brigid

Hata hivyo mwanariadha huyo amesema kuwa kunao wanariadha wengine walio na uwezo wa kuivunja rekodi yake akiwataja mabingwa wa dunia wa marathon na nusu marathon  Ruth Chepngetich na Peres Jepchirchir kuwa na uwezo wa kuweka rekodi mpya ya dunia.

“Mwanariadha yeyote ana uwezo wa kukimbia vizuri na kuvunja rekodi yangu au kuwa kama Brigid lakini naona Peres na Ruth wakiwa na uwezo huo”akaongeza Brigid

Brigid amesema kwa sasa yuko katika hali nzuri huku akiwa na uwezo wa kushiriki mbio zozote kuanzia mita 5000 hadi zile za barabarani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *