Brenda Wairimu avikwa taji ya muigizaji bora Afrika mashariki

Muigizaji wa nchi ya Kenya Bi. Brenda Wairimu alikuwa nchini Burkina Faso maajuzi kwa ajili ya tuzo za Sotigui.

Mwanadada huyo alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo kwenye vitengo vitatu lakini alishinda kwenye kitengo kimoja chini ya tuzo hizo za Sotigui.

Jukumu lake kwenye filamu kwa jina Subira ndilo lilimwezesha Brenda kushinda tuzo la muigizaji bora katika eneo la Afrika mashariki.

Kwenye filamu hiyo iliyoelekezwa na Sippy Chadha, Brenda anaigiza kama binti kwa jina Subira ambaye amelelewa Pwani karibu na bahari. Anafurahishwa na kazi ya babake ambaye ni mvuvi na anamsihi amfunze kupiga mbizi, kazi ambayo huchukuliwa kuwa ya wanaume.

Mamake Subira, sehemu ambayo imeigizwa na Nice Githinji anaonekana kutokubalina na jambo la Subira kuwa muogeleaji akiwa na shauku kwamba huenda asipate mume akikua mkubwa.

Hata baada ya kuolewa na kuhamia Nairobi, Subira anashindwa kabisa kuachana na maji na anaonekana akienda kuogelea kisiri jambo ambalo linawakera wakwe zake.

Bewnda alitangaza haya kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo aliweka video fupi inayoonyesha akitangazwa mshindi akipokezwa tuzo na anakwenda kwenye eneo la kutoa hotuba ya ushindi lakini video inakatika.

Tuzo za Sotigui huwa za nchi ya Burkina Faso ambayo iko kwenye eneo la magharibi barani Afrika na huwa zinalenga haswa waigizaji na wachekeshaji barani Afrika.

Mwaka huu, awamu ya tano ya tuzo hizo iliegemea upande wa kina dada sana, kwa lengo la kutambua mchango wa kina dada kwenye sekta ya filamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *