Bomu la ardhini laangamiza maafisa saba wa Tume ya Uchaguzi nchini Niger

Maafisa saba wa Tume ya Uchaguzi ya Niger (CENI) wameuawa wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa urais wakati gari lao lilipokanyaga bomu la kutegwa ardhini katika sehemu ya Tillaberi.

Taifa hilo hukumbwa mara kwa mara na mashambulizi kutoka kwa makundi ya watu waliojihami kwa silaha.

Mojawapo ya makundi hayo lilikuwa linamlinda mgombea wa urais wa chama tawala Mohamed Mazoum ambaye anapambana na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mahamane Ousman.

Sehemu ya Tillaberi inapakana na nchi tatu ambazo ni Niger, Burkina Fasso na Mali, ambako vikundi vya wanamgambo wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na lile la ISIL hufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la jangwa la Sahel.

Maelfu ya askari walipelekwa kote nchini Niger kulinda usalama wakati wa kura hiyo ili kuhakikisha kipindi salama cha mpito, ambacho kitakuwa cha kwanza tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1960.

Rais anayeondoka Mahamadou Issoufu ameng’atuka kwa hiari baada ya kukamilisha vipindi viwili vya utawala vya miaka mitano kila kimoja.

Uamuzi huo ulipongezwa na wengi hasa katika sehemu hiyo ambako viongozi hung’ang’ania kusalia mamlakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *