Categories
Kimataifa

Bobi Wine sasa adai maisha yake yamo hatarini

Mgombeaji urais wa mrengo wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema anahofia maisha yake.

Hii ni baada ya mgombea huyo kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo ambapo Rais Yoweri Museveni alihifadhi kiti chake.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa alikataa matokeo ya uchaguzi huo, kwani hakutendewa haki, akihoji kwamba ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amesema anahofia maisha yake na yale ya mkewe.

Anasema hajaruhusiwa kuondoka  nyumbani kwake kwani nyumba hiyo imezingirwa na maafisa wa usalama.

Licha ya Bobi kudai kuwa kulikuwa na visa vingi vya udanganyifu kwenye uchaguzi huo, Rais Museveni ameutaja kuwa wa huru na haki.

Kampeni za kabla ya uchaguzi huo zilighubikwa na ghasia huku watu kadhaa wakiuawa.

Serikali ilifunga huduma za mitandao kote nchini humo siku ya kuamkia kupiga kura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *