Bobi Wine mahakamani

Mwanamuziki wa Uganda ambaye pia ni mbunge na mwaniaji Urais Robert Ssentamu Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine amefikishwa mahakamani hii leo katika mji wa Iganga ulioko mashariki mwa nchi hiyo ya Uganda.

Bobi alikamatwa siku jumatano akiwa kwenye kampeni na anashtumiwa kwa kukiuka masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Wakili wa mbunge huyo wa Kyandondo mashariki akiomba mteja wake aachiliwe huru kwa dhamana, aliiambia mahakama kwamba mteja wake ni raia mwadilifu, kiongozi na atajitokeza mahakamani atakapohitajika kufanya hiyo.

Alilalamikia mahakama pia kuhusu tukio la leo ndani ya mahakama ambapo polisi wanasemekana kukiuka haki za Bobi Wine pale ambapo walimpokonya mavazi yake.

Wakili huyo alisema kwamba mtu aliyekamatwa na polisi anakoma kuwa chini yao mara tu anapofikishwa mahakamani na akashangaa ni kwa nini walikuwa wanamdhalilisha.

Aliitaka mahakama iwashurutishe polisi wamrejeshee nguo zake na vyote ambavyo walichukua kutoka kwake.

Bobi naye alizungumza mbele ya mahakama ambapo alisema kesi yake inastahili kuwa ‘Museveni dhidi ya Uganda’ na sio ‘Kyagulanyi dhidi ya Uganda’ na akamshtumu Rais wa taifa hilo kwa vifo ambavyo vimetokea nchini humo kutokana na rabsha zilizozuka baada yake kukamatwa.

Mwanamuziki huyo ambaye anawania urais kupitia chama cha National Unity Platform, NUP, aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni tano pesa za nchi ya Uganda na akaagizwa kuhakikisha kwamba anazingatia kanuni zote za kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Mikutano ya kampeini kulingana na jaji haifai kuwa na watu zaidi ya 200 na wote wanaohudhuria lazima wavalie barakoa na kuweka umbali unaohitajika kati yao.

Alipotoka kizimbani Bobi, alikwenda moja kwa moja hadi alipokuwa ameketi mke wake Barbara, akamkumbatia na kuketi na kuanza kusema naye akisubiri kujua iwapo dhamana ingelipwa ili awe huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *