Bobi Wine akamatwa punde baada ya kuidhinishwa kuwania Urais nchini Uganda

Mwanamuziki Bobi Wine wa nchi ya Uganda ambaye ni mbunge na sasa mwaniaji Urais anasemekana kukamatwa na polisi nchini humo punde baada ya kufika mbele ya Tume Huru ya Uchaguzi nchini Uganda ambapo aliidhinishwa kuwania Urais.

Kulingana na sauti ya mtu ambaye anaonyesha matukio mubashara kwenye ukurasa ulioidhinishwa wa Facebook wa Bobi Wine, haijulikani Mbunge huyo kwa jina Robert Kyagulanyi amepelekwa wapi.

Wafuasi wake wanaonekana kukusanyika kando kando ya barabara na kwa wakati mmoja wanarushiwa vitoza machozi na polisi.

Kabla ya hapo, polisi walikuwa wamemchagulia barabara ambayo angetumia hadi kwenye eneo la uteuzi na kulingana na maneno kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii alikuwa amekubaliana nao.

Kulingana naye alitaka mpango mzima wa uteuzi uende sawa hakutaka lolote liwe kikwazo.

Bobi aliidhinishwa kuwania Urais kupitia chama cha National Unity Platform “NUP” na sasa anajiunga na wengine walioidhinishwa jana ambao ni Rais wa sasa wa taifa la Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Mugisha Muntu na Henry Tumukunde.

Kwa sasa Bobi Wine anawakilisha eneo bunge la Kyandondo Mashariki bungeni na pia ni muigizaji na mhisani ambaye husaidia wasiojiweza katika jamii.
Uchaguzi mkuu wa nchi ya Uganda unatarajiwa kuandaliwa Alhamisi tarehe 18 mwezi Februari mwaka ujao wa 2021.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *