Bobi Wine aangaziwa kwenye Spotify

Mwanamuziki wa nchi ya Uganda Bobi Wine ameangaziwa kwenye kipindi fulani cha sauti tu ambacho kimewekwa kwenye jukwaa la muziki na vipindi vya sauti kwa jina Spotify.

Mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Marekani kwa jina Bas ndiye mtangazaji katika kipindi hicho kilichopatiwa jina la “The messenger” na kitaangazia maisha ya Bobi Wine.

Mbunge huyo wa eneo bunge la Kyandondo Mashariki nchini Uganda ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu anaangaziwa kwa sababu anawania urais nchini Uganda kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 14 mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Safari yake ya uanaharakati na kampeni za urais haijakuwa rahisi na kwa sasa anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa rais wa sasa Yoweri Museveni.

Jukwaa la kimitandao la Spotify linatoa fursa kwa watu kupakua na kusikiliza muziki na vipindi popote walipo lakini barani Afrika, linapatikana katika nchi chache.

Afrika Kusini, Morocco, Misri, Algeria na Tunisia ndizo nchi pekee ambazo zimekubalia Spotify kufikia sasa na haijulikani litasambaa lini kwenye nchi nyingine za Afrika.

Hii ina maana kwamba hata Uganda ambayo ni nchi muhimu kwa kipindi hiki cha Bobi Wine haitapata kukisikiliza.

Kipindi kuhusu maisha ya Bobi Wine kimeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Dreamville Studios na Awfully Nice Productions na kilikuwa kipatikane kwa mara ya kwanza kwenye Spotify tarehe 5 mwezi Januari mwaka 2021 siku chache kabla ya uchaguzi mkuu nchini Uganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *