Categories
Habari

Biashara zanoga Jomvu kufuatia kupungua kwa visa vya uhalifu

Eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, imeanza kuvutia wawekezaji kutokana na amani inayoshuhudiwa na kupungua kwa visa vya utovu wa usalama katika eneo hilo.

Kulingana na Mbunge wa eneo hilo Badi Twalib, eneo hilo limeshuhudia ongezeko la shughuli za kibiashara na kuwezesha wakazi kupata nafasi za ajira.

Twalib amesema hii ni kutokana na ushirikiano kati ya wakazi, viongozi wa eneo hilo na serikali.

“Jomvu ni eneo salama la kuishi, ndiyo sababu watu wamekuja hapa kufanya biashara. Na kama mbunge, nitahakikisha kazi yangu ni kulinda maslahi ya wananchi wangu na biashara zao,” ameeleza mbunge huyo.

Mbunge huyo alikuwa akiongea alipokabidhi gari la polisi litakalotumiwa kukabiliana na visa vya uhalifu katika eneo la Jomvu.

Amesema eneo hilo lilikuwa likikumbwa na visa vya utovu wa usalama, tatizo alilosema sasa limetokomezwa.

Twalib pia amezuru mradi unaendelea wa ujenzi wa majengo ya kisasa ya makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Jomvu huko Mikindani ambao unafadhiliwa kupitia Hazina ya Ustawi wa Eneo Bunge hilo CDF.

Kwenye ziara hiyo, Twalib amesema majengo hayo yatakuwa na afisi zote za utawala na yataimarisha utoaji huduma kwa wakazi.

“Afisi zote ambazo zinatakikana kuhudumia wananchi wa Jomvu tutaziweka katika jengo moja,” ameongeza Twalib

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *