Beyonce ajiunga na miito ya mabadiliko ya polisi nchini Nigeria

Mwimbaji na Muigizaji wa nchi ya America Beyonce amejiunga na kampeni inayoendelea nchini Nigeria ya kutafuta mabadiliko kufanyika katika idara ya usalama hasa polisi almaarufu #EndSARS.

Jumanne tarehe 20 mwezi oktoba Beyonce aliandika ujumbe kwenye Instagram akisisitiza haja ya kufutiliwa mbali kwa kikosi cha polisi kinachojulikana kama SARS nchini Nigeria.

Siku hiyo hiyo kulitokea ripoti kwamba polisi walifyatua risasi kwa umati wa watu ambao walikuwa wanaandamana katika eneo la lekki.

Beyonce alifichua kwamba anashirikiana na makundi kadhaa nchini Nigeria kuwapa usaidizi wanaoandamana kwa ajili ya kutafuta mabadiliko nchini humo.

Alisema nia yao kuu ni kutoa matibabu ya dharura, chakula na makazi kwa wanaohitaji.

Kikosi hicho cha “Special Anti-Robbery Squad (SARS)” kimekuwa kikimulikwa sana nchini Nigeria na hata nje kwa sababu ya kile kinachosemekana kuwa ni kutumia nguvu kupita kiasi.

Video ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha polisi wa kikosi hicho wakiwapiga risasi na kuwaua raia jambo ambalo lilisababisha maandamano katika sehemu kadhaa nchini Nigeria.

Awali Tiwa Savage ambaye ni mwanamuziki nchini Nigeria ambaye aliwahi kufanya kazi na Beyonce alikuwa amemwomba ajiunge na kampeni dhidi ya kikosi cha polisi cha SARS.

Tarehe 11 mwezi huu wa Oktoba mwaka 2020, Inspeka jenerali wa polisi nchini Nigeria Bwana Mohamed adamu alitangaza kuvunjwa kwa kikosi cha SARS na kuundwa kwa kikosi kingine kwa jina “Special Weapons and Tactics SWAT” lakini raia hawakuridhika.

Wengi walitaka wote waliokwenda kinyume na haki za binadamu katika kikosi hicho wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria jambo ambalo Rais wa taifa hilo Muhamadu Buhari aliahidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *