Ben Pol abadili dini

Benard Michael Paul Myang’anga ambaye anajulikana sana kama Ben Pol mwanamuziki kutoka nchi ya Tanzania amebadili dini kutoka Ukristo hadi Uisilamu.

Mwanamuziki huyo ambaye ni mume wa mfanyibiashara wa nchi ya Kenya Anerlisa Muigai alitangaza hayo ijumaa kupitia mitandao ya kijamii.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, aliweka picha akiwa amevalia kanzu nyeupe na akafunga kilemba akiwa kwenye msikiti wa masjid maamur. Picha hiyo ilikuwa na maneno “BISMILLAH-HIR-RAHMAN-NIR-RAHIM” ambayo ni dua fupi katika dini ya kiisilamu.

Wasanii wenzake nchini Tanzania kama vile Diamond Platinumz, Ommy Dimpoz, Mwana FA na Idris Sultan walionekana kuridhishwa na hatua hiyo ya Ben Pol ambapo waliongeza maoni yao chini ya picha hiyo.

Jina lake sasa ni “Behnam Paul Mnyang’anga” kulingana na picha ya cheti alichokabidhiwa cha kudhibitisha amejiunga na dini.

Akaunti ya Instagram ya mke wake Anerlisa Muigai bintiye mmiliki wa kiwanda cha pombe cha Keroche haina picha za Ben Pol na anasemekana kuzifuta baada ya hatua ya Ben ya kubadili dini.

Inasubiriwa kuona ikiwa naye atafuata nyayo za mume wake kwa maswala ya dini.

Kabla ya hapo kulikuwa na minong’ono kwamba ndoa yao ilikuwa imeingia doa jambo ambalo lilisababisha azindue kibao kwa jina “walimwengu”.

Alipokwenda kutumbuiza katika eneo la Muheza huko Tanga alikuwa amevalia kilemba ambacho wengi hukiita “Arafat” kutokana na jina la aliyekuwa kiongozi wa palestina Yasser Arafat ambaye alikuwa hakosi kukivaa.

Picha nyingine aliweka akiwa mjini Dar Es Salaam pia inamwonyesha akiwa amevaa kanzu nyeusi, kofia na hicho kilemba, anaonekana kuwa mwanafunzi mzuri wa dini kwa upande wa mavazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *