BBI yapata pigo la kwanza Baringo

Bunge la Kaunti ya Baringo limekuwa la kwanza kukataa mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020.

Mswada huo uliopendekezwa kupitia mpango wa maridhiano ya kitaifa, BBI, umezua mjadala mkali uliokumbwa na ghasia katika bunge la kaunti hiyo.

Ghasia hizo zimeanza mara tu baada ya Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya sheria n haki Charles Kosgei kuwasilisha mswada huo, hatua ambayo imezua mabishano makali kati ya wanaounga mkono na wanaopinga mswada huo.

Wanachama wa bunge hilo wanaopinga mswada huo walitaka ujadiliwe na kupigiwa kura mara moja, huku wale wanaouunga mkono wakitaka mjadala uahirishwe ili kutoa fursa ya ushirikishi wa umma.

Spika wa Bunge la kaunti hiyo alikuwa na wakati mgumu kurejesha utulivu huku polisi wa kukabiliana na ghasia walilazimika kutumia vitoa machozi katika  kutuliza hali bungeni humo.

Baadaye mjadala ulianza na hatimaye wawakilishi wadi wakapiga kura ambapo angalau 30 kati yao wamepiga la na kumlazimu spika kutangaza matokeo hayo hasi.

Uhasama wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Seneta wa kaunti hiyo Gideon Moi ulijitokeza wazi wazi, huku ghasia zilizokumba bunge hilo zikiwa baina ya wawakilishi wadi wanaomuunga mkono Moi dhidi ya wale wa Ruto.

Kwa sasa mswada huo umepitishwa na mabunge matatu katika Kaunti za Siaya, Kisumu na Homabay na unahitaji kupitishwa na angalau mabunge 21 zaidi ndipo uwasilishwe kwenye Bunge la Kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *