Mabingwa wa Ulaya Bayern Munich watakuwa wakiwinda taji ya pili ya kombe la dunia baina ya vilabu ulimwenguni watakaposhuka uwanjani Education City nchini Qatar kumenyana na mabingwa wa Amerika Kaskazini U.A.N.L Tigres kutoka Mexico .
Munich walishinda kombe la dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2013 na walifuzu kwa fainali ya Alhamisi baada ya kuwashinda mabingwa wa Afrika Al Ahly mabao 2-0 katika nusu fainali wakati Tigres ikiwabandua mabingwa wa Amerika Kusini Palmeiras bao 1-0 katika nusu fainali nyingine.
Al Ahly ambao ni mabingwa Afrika watashuka uwanjani Education City kukabiliana na Palmeiras ya Brazil katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu na nne .
Mashindano hayo yalikuwa yaandaliwe Disemba mwaka jana kabla ya kuahirishwa hadi mwaka huu kutokana na ugonjwa wa Covid 19.