Baraza la vyombo vya habari nchini laomboleza kifo cha mwanahabari Betty Barasa

Baraza la vyombo vya habari hapa nchini limetuma risala za rambi rambi kwa marafiki na familia ya mhariri wa ngazi za juu wa video wa shirika la utangazaji hapa nchini KBC Betty Barasa.

Kwenye taarifa kwa vituo vya habari, afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo ameshtumu mauaji ya Betty yaliyotekelezwa usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake katika sehemu ya Ololua huko Ngong kaunti ya Kajiado .

Omwoyo amesema huku polisi wakichunguza mauaji hayo , visa vya dhuluma dhidi ya wanahabari havikubaliki na ukiukaji wa uhuru wa vyombo vya habari jinsi ilivyoratibishwa chini ya vifungu vya 34 na 35 vya katiba.

Baraza hilo la vyombo vya habari sasa limetoa wito wa kuharakishwa kwa uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwanahabari huyo kwa lengo la kukamata na kuwashtaki wahusika.

Kifo cha Betty kimesababisha kumiminika kwa risala za rambi rambi huku wale waliomfahamu wakimtaja kuwa mwanahabari mkakamavu na mfanyakazi aliyejitolea ambaye kumbu kumbu zake zitasalia mioyoni mwao milele

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *