Baraza la madhehebu mbali mbali laongezewa muda wa kuhudumu

Waziri wa afya Mutahi Kagwe ameongeza kwa miezi 6, muda wa kuhudumu kwa baraza linalojumuisha madhehebu mbali mbali, baada ya muda huo kufikia tamati mwezi Disemba mwaka jana. 

Baraza hilo lilikuwa limejukumiwa kubuni mikakati ifaayo kwa shughuli za kuabudu, sherehe za harusi na pia hafla nyingine za kidini kuambatana na kanuni za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Kanuni hizo ni pamoja na kudumisha umbali unaohitajika baina ya watu,kuvalia barakoa katika hafla za ibada na unawaji mikono.

Kurefushwa kwa muda wa kuhudumu kwa baraza hilo kunajiri wakati ambapo juhudi zinafanywa za kupunguza kasi ya maambukizi ya Corona.

Wizara ya afya inapanga kuzindua mpango wa chanjo ambao unalenga wahudumu wa sekta ya afya na pia makundi mengi ya watu walio kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa corona.

Kagwe, ambaye alikuwa akiwahutubia wana-habari siku ya Ijumaa  alilipongeza baraza hilo linalo-ongozwa na  Askofu Mkuu Anthony Muheria wa dayosisi ya Nyeri ya kanisa katoliki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *